Saturday, May 25, 2013

MAPACHA WATANO WALIOZALIWA JANA WAFARIKI NA KUZIKWA BILA MAMA YAO KUSHUHUDIA


 
 Mwalimu Sofia Mgaya akiwa amelala na watoto wake wote watano  kitandani  mara baada ya kujifungua jana.

Na Juma Nyumayo, Songea
WATOTO  mapacha watano waliozaliwa hai jana wamefariki baada ya kuishi takribani saa 10 tu toka wazaliwe na kuzikwa bila kushuhudiwa na mama yao..
Watoto hao wamekwisha zikwa katika makaburi ya Lilambo nje kidogo ya Manispaa ya Songea njia ya kuelekea Peramiho kwa Shangazi yake mama yao wakati mama yao akiendelea kupata matibabu Hospitali ya mkoa, Songea.
Mkuu wa Shule ya Sekondari ya Luwawazi, Mwl. Msigwa, ameuambia mtandao huu mara baada ya kutoka mazikoni kuwa watoto hao wote watano wamefariki jana saa tatu usiku.
Vifo hivyo, vimethibitishwa na Mganga Mkuu Mfawidhi wa Hospitali ya Mkoa wa Ruvuma hapa Songea,  Dkt Benedict Ngaiza kuwa wote walifariki jana.
Akizungumzia mazishi hayo, Mwl. Msigwa amesema  kila mtoto amezikwa katika kaburi lake.
"Tumewazika kila mmoja na kaburi lake, nilishaamua nikawazike nyumbani kwangu Msamala, lakini kwa bahati alijitokeza Shangazi yake mwalimu anayeishi huko Lilambo ambako tumefanya maziko hayo," alisema Mwl. Msigwa.
 Alifafanua kuwa licha ya kupewa miili ya marehemu hao mapema walichelewa kuzika kwa  kuwasubiri wazazi wa mwalimu Sofia, wakitokea huko Ludewa mkoani Njombe kushiriki Mazishi hayo," alisema Mwl Msigwa ambaye ameendelea kupata simu za pongezi za kupata watoto watano kwa mpigo kwa mwalimu wa shule yake.
Wakati maziko hayo yanaendelea tayari mipango katika taasisi na Ofisi ya Manispaa ya Songea ilikuwa ikifanywa namna ya kumsaidia mwalimu huyo namna ya kuwale watoto hao wakiongozwa na Meya wa Manispaa Mhe. Charles Muhagama.
Watoto hao watano walipatikana jana kwa wakati mmoja baada ya kufanyiwa upasuaji wa uzazi katika Hospitali ya Rufaa ya mkoa wa Ruvuma iliyopo mjini Songea.
 Awali akizungumza na waandishi wa habari,  Mganga Mkuu mfawidhi wa hospitali hiyo,  Dkt. Ngaiza alimtaja mwanamke huyo aliyejifungua watoto hao watano kuwa ni Mwalimu wa Shule ya Sekondari, Sophia Mgaya (28) ambaye ni mkazi wa Ruhuwiko mjini Songea na kuwa hali za watoto hao ziliendelea vizuri pamoja na kuzaliwa chini ya umri wa kawaida wa kuzaliwa ambao ni miezi tisa.
 Alisema kuwa mama huyo alipokuwa akihudhuria kliniki hospitalini hapo uchunguzi uliokuwa ukionyesha kuwa tumboni mwake kuna watoto wanne ambao walikuwa wakiendelea vizuri tumboni humo lakini mnamo Mei 24 mwaka huu majira ya saa 4 asubuhi alianza kusikia uchungu na kufikishwa hospitalini hapo na kufanyiwa upasuaji na kukutwa akiwa na watoto watano hai tumboni mwake.
 Dkt. Ngaiza alisema kuwa watoto watatu ni wa kiume na wawili ni wa kike na wote wako hai na wamewekwa katika chumba maalumu kwa sababu wamezaliwa wakiwa na umri wa wiki thelathini na nne(miezi nane) na siyo miezi tisa kama ilivyo kawaida.
 Aidha alisema kuwa watoto hao wamezaliwa wakiwa na uzito mdogo huku mwenye uzito mkubwa akiwa gramu 730 na mwenye uzito mdogo akiwa na gramu 430 na huo ukiwa ni uzazi wake wa pili huku mama mzazi wa mwanamke huyo aliwahi kujifungua watoto watatu na wote wako hai na mmoja ni mtoto wa kiume anasomo kidato cha sita katika shule ya wavulana ya Songea.
 Alisema kuwa tukio hilo ni la kihistoria kutokea katika hospitali hiyo kwa sababu kumekuwepo na matukio ya akina mama kujifungua watoto wawili au watatu na siyo zaidi ya idadi hiyo kama ilivyotokea kwa mama huyo.
Watoto hao walikuwa na uzito mdogo kuanzia kuanzia wa kwanza aliyekuwa na uzito wa gramu 730, wa pili gramu 810, wa tatu gramu 670, wa nne gramu 820, na watano alikuwa na uzito wa gramu 43o. 




 

No comments:

Post a Comment