Friday, May 17, 2013

DK. WA MOYO MASAU AFARIKI DUNIA

 
Kuna taarifa kuwa yule mtaalamu wa magonjwa ya moyo ambaye pia alikuwa anamiliki Taasisi ya Magonjwa ya Moyo nchini (THI), Dk Ferdinand Masau, amefariki dunia.

Dkt. Ferdinand Masau.
Imeelezwa kuwa Dk Masau aliaga dunia usiku wa kuamkia leo akiwa katika Hospitali ya Aga Khan, iliyopo Upanga jijini Dar es Salaama alikokuwa anatibiwa.
Habari hizo zilithibitishwa na marafiki wa karibu wa daktari huyo bingwa ambao hata hivyo hawakuwa tayari kutajwa majina kwa maelezo kuwa, wasemaji wa tukio hilo ni wanafamilia.
Maelezo kama hayo yalitolewa pia na mmoja wa maofisa wa hospitali ya Aga Khan, akisema wanafamilia ndio wanaoweza kuzungumzia taarifa za kifo cha mpendwa wao.
Enzi za uhai wake, baada ya kufanya kazi kwa miaka kadhaa nje ya nchi, alirejea nchini mwanzoni mwa miaka ya 2000 na kuanzisha taasisi ya moyo, akilenga kuwasaidia Watanzania wengi ambao kwa muda mrefu walikuwa wakikosa tiba ya uhakika nchini, hivyo kukimbilia nje ya nchi, hasa India.
Hata hivyo, ndoto zake ziliyumba kwa kiasi fulani kutokana na kukosa majengo ya uhakika kwa ajili ya taasisi yake, hivyo kulazimika kupanga katika majengo ya Shirika la Taifa la Hifadhi ya Jamii (NSSF) ambako baada ya kudaiwa kushindwa kulipa kodi, mali zake ikiwa ni pamoja na vifaa na samani zote zilizokuwa katika taasisi hiyo zilipigwa mnada. Baadaye aliripotiwa kuibuka upya na kuanza kuwekeza taasisi nyingine ya magonjwa hayo eneo la Mbweni nje kidogo ya jiji la Dar es Salaam.
 
Source. Lukwangule Blog

No comments:

Post a Comment