Monday, May 13, 2013

" AZIMIO LA ARUSHA BADO LIPO? "

Ya Kinana na Miiko ya Azimio la Arusha

 
Mwl. Julius K. Nyerere
 
Kabla hata mjadala wa kufa kwa Azmio la Arusha uliojadiliwa katika tamasha la Kigoda cha Mwalimu Nyerere hivi karibuni katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam haujapoa, tayari mfano hai umeibuka.

Kimsingi Azimio la Arusha lililotokana na mkutano wa Halmashauri Kuu ya Tanu Januari 1967 na kuzinduliwa Februari mwaka huo, liliambatana na miiko ya uongozi ambapo iliamuliwa kuwa kiongozi wa Tanu au wa Serikali sharti awe mkulima au mfanyakazi na asishiriki katika jambo lolote la kibepari au kikabaila.

Ilipofika mwaka 1991, CCM chini ya uongozi wa Rais Ali Hassan Mwinyi walilifanyia mabadiliko azimio hilo na kulegeza masharti yake kwa kisingizio cha kwenda na wakati na hali ya siasa na uchumi wa kimataifa.

Kutokana na unafuu huo waliojiwekea, viongozi wengi walianza kujilimbikizia mali na kushiriki biashara.

Tunaona kwa msingi huo, hata Rais Jakaya Kikwete alipokuwa akijaribu kukisafisha chama kwa ule msamiati wa kujivua gamba ambao sasa umeyeyuka, aliweka pia sharti la viongozi kujitenga na biashara, japo hadi sasa halijatekelezwa.

Sasa linapokuja la Katibu Mkuu wa chama hicho Abdulrahman Kinana kuhusishwa na ujangili wa pembe za ndovu kwa sababu tu ya kumiliki kampuni ya usafirishaji mizigo nje ya nchi, inatoa picha hiyo ya madhara ya kiongozi wa chama na Serikali kuwa mfanyabiashara.

Wakati msemaji wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni katika Wizara ya Maliasili na utalii, Mchungaji Peter Msigwa akilipua bomu hilo, mwenzake Waziri wa wizara hiyo, Balozi Khamis Kagasheki, na Waziri wa Mambo ya Ndani, Dk Emmanuel Nchimbi wamemtetea Kinana wakisema alikuwa wakala wa meli iliyosafirsha mzigo huo unaolalamikiwa.

Kagasheki alitoa mfano wa mashirika ya ndege ya ATCL na Precision Air kulaumiwa kwa mzigo iliyobebwa na abiria wake. Lakini labda nimuulize Kagasheki, kwani mizigo inaposafirishwa na meli haikaguliwi bandarini? Au abiria wanaposafiri na ndege hawakaguliwi mizigo yao?

Ni kweli kuna mizigo ambayo ni vigumu kuigundua, kwa mfano mtu akiwa amemeza dawa za kulevya, lakini kontena zima lipite bandarini bila kukaguliwa? Kwa nini linapofika nchi za wenzetu ligunduliwe?

Hili liwe fundisho kwa viongozi wa umma kuchagua uongozi au kufanya biashara. Kama Serikali ya CCM bado inaamini katika Sera ya Ujamaa na Kujitegemea iliyoundwa na Azimio la Arusha, basi ifuate misingi yake.

---
gazeti la MWANANCHI


Source: http://www.wavuti.com/

No comments:

Post a Comment