Sunday, May 5, 2013

BOMU LA ARUSHA , BABA ASKOFU NA MWAKILISHI WA PAPA WASALIMIKA

 
UPDATE/TAARIFA MPYA   saa 12:13 jioni

Majina ya waliojeruhiwa katika tukio hilo ambao wamelazwa katika hospitali za  maunt Meru, na hospitali teule ya jiji la Arusha ya St Elizabeth wametambulika kuwa ni:-

John Thadei, Regina Fredirick, Joram Kisera, Novelt John, Rose  Pius, John  James, Anna Kessy, Joan Temba, Neema Kihisu, Gloria Tesha, Innocent Charles, Fatuma Haji, Fikiri Keya, Simon Andrew, Anna Edward, Lioba Oswald, Rose Pius, Philemon Gereza, Kisesa Mbaga, Neema Daudi, Beata Cornell na Debora Joachim.


UPDATE/TAARIFA MPYA saa 12:47 mchana

  1. Baba Askofu Mkuu wa Jimbo la Kanisa Katoliki Arusha, Mhashamu Josephat Louis Lebulu na Mwakilishi wa Papa, Nuncio, Francisco Montecillo Padilla wameondoshwa katika eneo la tukio na kikosi cha ulinzi na usalama.
  2. Kikao cha dharura cha ulinzi na usalama kimeafikiana kusitisha shughuli ya leo hadi hapo itakapotangazwa upya.
  3. Padre Simon Mtengesi amefunga rasmi ibada kwa sala fupi na kuwaomba watu warejee majumbani mwao.
  4. Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Magesa Mulongo amefika na kutizama maeneo ya Kanisa, kisha akazungumza kwa kusema kuwa mwakilishi wa Papa alikuwepo Arusha tangu tarehe 2 Mei mwaka huu akitembelea maeneo kadhaa ya mkoa huo, ikiwemo Ngorongoro na leo akiwa katika kilele cha ziara yake kwa kuzindua Parokia mpya, ndipo mlipuko huo ukatokea na kusababisha shughuli nzima kuahirishwa. Mulongo amesema wataalamu wa uchunguzi kutoka Makao Makuu ya Jeshi la Polisi wanatarajiwa kuwasili mkoani Arusha kuungana na kikosi cha Mkoani hapo ili kufanya shughuli ya uchunguzi.
  5. Mkuu wa kikosi cha Polisi cha usalama Mkoani Arusha, RPC Kamanda Liberatus Sabas amefika katika eneo husika na kuzungumza akisema kuwa walipokea taarifa za tukio kwa maelezo kuwa mlipuko ulitokana na kitu cha kurushwa kutoka kwa mtu mmoja aliyefika eneo hilo kwa gari. Hadi sasa Polisi inamshikilia mtu mmoja kwa mahojiano zaidi na inaomba wananchi wenye taarifa zaidi waziwasilishe katika vyombo husika.
  6. Mbunge wa Arusha Mjini, Godbless Lema amefika katika eneo na kuzungumza na wananachi. Amesema hili ni tukio la kushitua sana kwa kuwa limetokea kwenye eneo la ibada, wakati misa ikiendelea... (mawasiliano ya redio yamekatika wakati Lema anazingumza. Baada ya muda mtangazaji wa Radio Maria ameomba samahani kuwa kuna mtu alizima swichi. Baadaye mwandishi alimpata Lema akiwa na Mbunge wa Arumeru Mashariki, Jashua Nassari na kuwapa nafasi ya kuzungumza na kutoa ujumbe wao kwa wananchi.) Baadaye Lema na Nassari walikwenda hospitalini na kujitolea damu na kuhamasisha vijana kufanya hivyo, zoezi ambalo waliliunga mkono na kuanza kushiriki.
  7. Padre wa Parokia ya Moyo Mtakatifu wa Yesu, Sombetini katika Jimbo Kuu la Arusha, Moses Mwaniki amewapa pole majeruhi na kuwaomba watu kujitolea kwa maji na vyakula kwa ajili ya kuwajali majeruhi zaidi ya 30 waliolazwa katika hospitali mbalimbali za ndani na nje ya mkoa huo.

---

Mwendo wa kuelekea saa tano adhuhuri ya leo katika iliyokuwa iwe Parokia ya Mpya ya Yosefu Mfanyakazi iliyokuwa inafunguliwa leo, pametokea mlipuko uliojeruhi watu kadhaa, watatu wakiwa wamejeruhiwa vibaya sana.

Kwa mujibu wa taarifa zinazosikika moja kwa moja kupitia Radio Maria, Tanzania, mlipuko huo umetokana na kitu ambacho kinasadikika kuwa lilikuwa ni bomu. Hata na hivyo haijafahamika ikiwa kama ndivyo, lilikuwa ni bomu la kutegwa ama kurushwa kwa mkono. Ni vigumu na mapema sana kuthibitisha kilicholipuka. Tafadhali tuvute subira kwa kuisubiri taarifa ya Polisi.

Inaripotiwa kuwa wengi wamejeruhiwa miguuni na kulazimika kuwahishwa hospitalini kwa matibabu zaidi. Hakuna taarifa zozote za kifo zilizoripotiwa. Majeruhi wamepelekwa katika hospitali mbalimbali za mkoa huo kwa matibabu zaidi.

Kwa muda huu, viongozi mbalimbali wa Kanisa akiwemo mwakilishi wa Papa aliyekuwa anatabaruku Kigango hicho kilichozaliwa mwaka 2008 kuwa Parokia, Nuncio, Francisco Padilla na viongozi wa jeshi la polisi na usalama, wanaendelea na kikao ili kuamua hatima ya misa iliyokatizwa.

Hizi ni taarifa za awali tu, kwa ajili ya kukupasha kinachoripotiwa redioni. Taarifa kamili itawekwa itakapopatikana. Tafadhali endelea kusikiliza Redio Maria Tanzania (inasikika pia online, tizama kwenye menu ya Redio hapo juu) muda huu wakiwa wanatangaza kuhusu tukio hili.
 

Kanisa mlimotokea shambulio la mlipuko





Source: http://www.wavuti.com/

1 comment: