Wednesday, May 8, 2013

DKT. EDWARD HOSEA ALIA NA SHERIA KUSHINDWA KUPELEKA KESI RUSHWA KUBWA MAHAKAMANI


Mkurugenzi Mkuu wa TAKUKURU, Dkt. Edward Hosea, akijibu maswali ya waandishi wa habari mkoa wa Ruvuma, nje ya Ukumbi wa Herritage Cottage, Songea alipotoa mafunzo kwa viongozi wa dini Mikoa ya Njombe, Iringa na Ruvuma.


Dkt. Edward Hosea (Kushoto) akijibu maswali ya waandishi wa habari mkoa wa Ruvuma.


Picha za juu na chini zinaendelea kuonyesha mahojiana ya Mkurugenzi mkuu wa Takukuru, na waandishi wa habari Mkoa wa Ruvuma jana.







Na Juma Nyumayo, Songea

MKURUGENZI Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa nchini (TAKUKURU), Dkt. Edward Hosea, ameendelea kusisitiza kuwa Taasisi yake kimuundo wa sheria haina uwezo wa kupeleka kesi za rushwa kubwa mahakamani hadi zipitie kwa Mwendesha mashitaka wa serikali, (DPP na mpaka sasa amepeleka mezani kwake mafaili ya kesi kama hizo.

Hayo ameyasema wakati wa Mkutano wake na waandishi wa habari Mkoani Ruvuma, wakati akijibu maswali ambayo waandishi wa habari walipaza kilio cha wananchi kuilalamikia TAKUKURU kuwa inashughulika na rushwa kwa dagaa na kuacha mapapa yakitamba ( dagaa ni watu wadogo na rushwa ndogo ndogo mapapa ni wala rushwa kubwa ).

"Mimi na DPP hatuna ugomvi kama mnavyofikiria, tatizo hapa ni mfumo wa muundo wa taasisi na sharia  Kifungu namba 5 na 7 kinachoitaka tasisi kuchunguza na sio kushitaki "Grand Corruption," alisema Dkt. Hosea, na kutamba kuwa tayari wamechunguza rushwa kubwa na kupeleka mafaili kwa DPP kwa hatua za kushitaki mahakamani.

Alibeza kauli mbalimbali zinazotolewa dhidi ya tasisi yake kuwa hazina mashiko kwakuwa watu wengi hawafahamu mafanikio ya TAKUKURU na ndio maana ameanzisha kutoa mafunzo kwa makundi mbalimbali ili wajue kinachoendelea.

TAKUKURU imefanikiwa sana kwa kuajiri na kuwajengea uwezo mkubwa watumishi wake ambao wameenea nchi nzima.

"Tumejenga majengo ya Ofisi, vifaa vya kufanyia kazi katika ngazi za mikoa na tutaendelea katika ngazi za wilaya kadri bajeti itakavyoruhusu," alifafanua Dkt. Hosea na kusema kuwa maneno hayo ni moja ya mafanikio ya watu kuielewa taasisi hiyo ambayo inahitaji nguvu za pamoja kuitokomeza rushwa hapa nchini.

Aliwaahidi waandishi wa habari kote nchini kutoa mafunzo kwao yeye mwenyewe kama alivyofanya kwa viongozi wa dini, wanafunzi na wakuu wa shule za sekondari na ataanzia kuwanoa waandishi wa habari wa mkoa wa Ruvuma.
 

No comments:

Post a Comment