Lory lililopata ajali na kusababisha vifo |
Na Nathan Mtega,Songea
WATU
nane wamefariki dunia kwa ajali ya gari iliyotokea Mei 27 mwaka huu
majira ya saa 7 usiku katika kitongoji cha Bombambili kata ya Hanga wilayani
Namtumbo mkoani Ruvuma.
Kwa mujibu wa mashuhuda wa ajali hiyo walisema
kuwa watu zaidi ya ishirini walikuwa wakisafiri kwenye gari la mizigo aina ya
Isuzu lenye namba za usajili T 697 ABC lililokuwa likitoka wilayani Namtumbo
kuelekea Songea likiwa limebeba magunia zaidi ya thelathini ya ufuta pamoja na
abiria hao wakiwemo wamiliki wa mzigo huo.
Walisema kuwa baada ya gari hilo kufika eneo
hilo ghafla liliacha njia na kugonga karavati na kupinduka na baada ya
kupinduka mzigo huo wa magunia ya ufuta uliwafunika watu hao na kusababisha
vifo vya watu saba papo hapo huku mwingine mmoja akifariki baada ya kufikishwa
hospitali ya rufaa ya mkoa wa Ruvuma.
Kamanda wa polisi wa
mkoa wa Ruvuma Deusdedit Nsimeki akithibitisha kutokea kwa ajali hiyo alisema
kuwa uchunguzi wa awali unaonyesha kuwa chanzo cha ajali hiyo ni mwendo kasi wa
dereva wa gari hilo uliosaababisha ashindwe kuumudu usukani ingawa uchunguzi
zaidi unaendelea kufanyika.
Aidha aliwataja watu waliofariki dunia kuwa ni
Bakali Bakali,Athman Awaja,Matola Gwaja,Jawadu Ntambo,Adamu Hamimu,Raika
Abediul na wengine ni Musa Mdalali,na Abdalah Magongoni
Naye Mganga Mkuu mfawidhi wa hospitali ya
rufaa ya mkoa wa Ruvuma Dkt Benedict Ngaiza alithibitisha kupokea majeruhi kumi
na moja wa ajali hiyo ambapo majeruhi wawili walitibiwa na kuruhusiwa huku
majeruhi tisa akiwemo mtoto mwenye umri wa miaka 11 akiwa amevunjika miguu yote
miwili wanaendelea kupatiwa matibabu hospitalini hapo.
Mwisho.
No comments:
Post a Comment