MATREKTA YAKIWA KAZINI KUCHIMBA MAKAA YA MAWE HUKO KIJIJI CHA MTUNDUWALO, KATA YA RWANDA WILAYA YA MBINGA- RUVUMA |
Na Nathan
Mtega,Mbinga.
MKUU wa Mkoa wa Ruvuma Said Mwambungu
amelazimika kuufunga kwa muda mgodi wa makaa ya mawe wa kampuni ya
TANCOAL baada ya wananchi wa kijiji cha Mtunduwalo
kata ya Ruanda Wilaya ya Mbinga kumtaka aufunge mgodi huo mpaka watapolipwa
madai yao ya muda mrefu ya fidia pamoja na kuyaweka mazingira yao katika hali
inayostahili kwa matumizi ya binadamu.
Mwambungu alichukuwa uamuzi huo kwenye mkutano
wa hadhara uliofanyika kwenye viwanja vya shule ya msingi Mtunduwalo ambao
ulihudhuriwa na mamia ya wanakijiji hicho wakiwemo viongozi wa kamati za ulinzi
na usalama za Wilaya ya Mbinga na Mkoa pamoja na viongozi wa vyama
vya siasa.
Mapema Mkuu wa Wilaya ya Mbinga Senyi Ngaga
akimkaribisha Mkuu wa Mkoa Mwambungu ili aweze kuongea na wananchi kuhusu
mgogoro uliopo kati ya wananchi na mwekezaji wa mgodi huo ndipo
alipoanza kwa kusema wananchi wa Mtunduwalo hoyee!wananchi
wakajibu hoiiii!mpaka kieleweke kadhalika kwa mkuu wa Mkoa ambapo aliwataka kuwa
watulivu wakati anapotaka kuwaambia nini serikali yao imefanya katika kulimaliza
tatizo hilo.
Pamoja na Mkuu wa Mkoa kujaribu kuwatuliza
wanakijiji hao lakini bado hali iliendelea kuwa mbaya baada ya wananchi hao
kumshinikiza mkuu huyo wa Mkoa waende nae mpaka kwenye eneo la mgodi akaufunge
na kama haitawezekana basi wapo tayari kufa kwa kupigwa risasi kuliko kufa kwa
njaa wakati haki zao zipo zinadhurumiwa na viongozi wa serikali huku baadhi yao
wakiugua magonjwa mbalimbali kutoka kunywa maji yenye chembechembe ya sumu ya
madini ya makaa yam awe yanayochimbwa eneo la kijiji hicho.
Akitoa kero mbele ya Mkuu wa Mkoa Mwambungu
mwananchi Erick Mapunda alisema kuwa wamechoka na ahadi hewa za mwekezaji ambazo
kila kukicha imekuwa ni siasa hivyo ujio wa Mkuu wa Mkoa huyo uwe ni hitimisho
la kwenda kuufunga mgodi huo mpaka hapo watapotimiziwa ahadi walizoahidiwa
pamoja na kuwalipa fidia wanazoidai kampuni ya TANCOAL.
Joseph Messa alieleza kuwa yeye kama mwananchi
wa kijiji hicho ameshakata tama ya maisha kwa sababu hali ya kijiji chao ni
mbaya kutokana na kukosekana kwa miundo mbinu ya barabara,maji,shule pamoja na
zahanati kwani watoto wao wamekumbwa na magonjwa ya kichocho ambayo hawajui
yanasababishwa na nini na kwamba wamekuwa wakinywa maji ya sumu tangu mgodi huo
uanze kufanya kazi licha ya kuwa malalamiko hayo walishapewa viongozi wa
serikali ya kijiji,Wilaya na Mkoa.
Kwa upande wake Benedina Komba alisema kuwa
tangu mgodi huo uanze kufanya kazi wananchi wa kitongoji cha Nkaya walipewa
ahadi ya kuhama maeneo yao kwa muda kwa madai kuwa wataonyeshwa maeneo mengine
ambayo wangepewa fidia ili wakajengee mahali pengine jambo ambalo mpaka sasa
halijatekelezeka huku wakiangaika na watoto kutokana na njaa kwa kuwa eneo
walilokuwa wakilima kuchukuliwa na kampuni hiyo.
Wosteri Mapunda alielekeza shutuma nzito kwa
waandishi wa habari wa Mkoa wa Ruvuma kwa kutoandika habari za mgogoro huo
tofauti na waandishi wa Mkoa wa Arusha ambao wamekuwa wakiandika habari za
mgogoro wa Loliondo ambapo serikali baada ya kusikia kwenye vyombo vya habari
ilihamia Loliondo ili kumaliza tatizo lililopo na kwa nini Mtutunduwalo
ishindikane kwa muda wa miaka mitatu sasa.
Aidha Johoni Nyimbo alimnyooshea kidole Mbunge
wa jimbo la mbinga mashariki Gaudensi Kayombo na kumkumbusha ahadi aliyowaahidi
wananchi wa kijiji hicho mei 19 mwaka 2011 kwenye mkutano wa hadhara kuwa endapo
wanakijiji hao hawatalipwa fidia wanazodai atajiuzuru nafasi aliyonayo ya ubunge
na kumtaka ajiuzulu nafasi ya ubunge mara moja jambo ambalo lilimpandisha hasira
na baada ya kauli iyo alilazimika kusimama ili kutoa ufafanuzi wa
kauli yake hali ambayo isababisha kuwapandisha hasira wananchi hao na kuanza
kumzomea.
Hata hivyo
Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Ruvuma ambaye pia ni Mwenyekiti wa halmashauri ya
Wilaya ya Mbinga Oddo Mwisho naye alikumbwa na adha ya zomea zomea hiyo baada
kusimama na kuanza kujieleza kuhusiana na jitihada za chama cha CCM na Serikali
yake ya Wilaya na Mkoa kuwa kwa muda mrefu wamekuwa wakifanya mazungumzo kupitia
Wizara ya nishati na madini,Shirika la maendeleo ya Taifa (NDC) pamoja na
mwekezaji wa kampuni hiyo ya TANCOAL kwa lengo la kumaliza mgogoro uliopo kati
ya mwekezaji na wananchi.
Kufuatia vurugu zilizojitokeza kwenye mkutano
huo mkuu wa Mkoa Mwambung alilazimika kusitisha mkutano huo kwa muda na
kuwataka wananchi hao warudi eneo la mkutano baada ya nusu saa ili apate nafasi
ya kujadiliana na kamati yake ya ulinzi na usalama na baadae baada ya nusu saa
kupita mkutano ulianza ambapo Mkuu wa mkoa Mwambungu aliwaeleza wanakijiji hao
kuwa amesikia maoni yao na amefikia hatua ya kuufunga mgodi huo kwa muda hadi
hapo madai yao mbali mbali yatakapofanyiwa kazi na kutekelezwa.
Mwisho.
No comments:
Post a Comment