Thursday, May 16, 2013

BABA ASKOFU AVUNJA UKIMYA, ASEMA AMESTAAFU KWA MANUFAA YA TAIFA LA MUNGU



Baba Askofu Mstaafu wa Jimbo Kuu la Songea, Norbert Mtega akizungumza na wanahabari leo jioni hii.


Na Juma Nyumayo, Songea.
 
KUTOKANA na kupokelewa kwa Mshtuko, habari za kustaafu kwa Baba Askofu  Norbert Mtega wa Jimbo Kuu la Songea na waumini na watu mbalmbali wakiwemo viongozi wa Dini, Serikali na Mashirika yasiyokuwa ya Kiserikali katika Jimbo Kuu la Songea jana.
Baba Askofu Mtega amevunja  ukimya na kuwaondoa wasiwasi waumini na wananchi wa Jimbo Kuu la Songea na Taifa kwa ujumla kuhusu kutangazwa ghafla kustaafu kwake kulikokubaliwa na Papa Mtakatifu Francis.
"naamini watu wamestuka kwakuwa tangazo hili la kustaafu kwangu lilikuwa katika usiri mkubwa, nimeomba kwa hiari yangu kwa manufaa ya taifa la mungu na Jimbo Kuu la Songea," alisema Akofu huyo ambaye ana siku moja katika jina la Askofu Mstaafu.
Aliwaambia waandishi kuwa amekuwa na shida kubwa kiafya siku za karibuni na kwa hiari yake bila kushauriana na mtu yeyote kutokana anavyoona mwelekeo wa afya yake alimuandikia Papa kuomba kustaafu mapema.
Umri wa kawaida uliowekwa na kukubalika kwa Kustaafu Askofu ni miaka 75. Askofu Mtega anaumri wa miaka 67 sasa.
Amesema pamoja na kwamba alikuwa akifanya jkazi za kitume, amekabiriwa na tatizo la kiafya ambalo ni sababu tosha ya Askofu yeyote kuruhusiwa kustaafu kama alivyofanya yeye.
Amewathibitishia waandishi wa habari kuwa kwa muda mrefu wa zaidi ya miaka 6 akiwa askofu wa jimbo la Iringa na Miaka 22 Jimbo Kuu la Songea amefanya mengi ya ki-utume na maendeleo ya watu wote katika Nyanja za Elimu, Afya, Uchumi na Mazingira.
"Nashukuru nimestaafu mwaka wa Imani, nilipokea Jimbo hili na kuitangaza imani na kupokelewa vizuri, kazi iliyobaki ni kuimarisha Imani," alisema na kufafanua kwamba ni katika jimbo la Songea ambalo lina waumini wengi na kuwa na Abasia mbili ya wanaume kule Hanga na Peramiho.
Alipoulizwa atakwenda kuishi wapi baada ya hapa, Baba Askofu Mstaafu Mtega amechagua kuishi Jimboni Songea, na kuwaomba waumini wote wafunge Novena ili Papa Francis aweze kumchagua Askofu mwenye uwezo zaidi yake na kwamba yeye kama afya yake itatengemaa ataendelea kufanya kazi za kitume na kushauri.
"Nitaendelea kufanya kazi za kitume, hata hivyo nitatoa kipaimara na  Mei 30 nategemea kusoma misa ya Upadrisho nikiwa Askofu Mstaafu," alisema.
Alimalizia kwa kusema kuwa anawaomba watu wote waungane katika imani, umoja na kuhimiza utunzaji wa mazingira yanayoharibiwa kwa kasi. Na kwamba anatazamia Jimbo kuu la Songea litapata Mchungaji atakayesimamia vema maagizo ya kanisa na mabo ya kijamii kama yalivyopangwa na yale atakayoanzisha akisaidiwa na mapadre wa Jimbo Kuu la Songea 
 


No comments:

Post a Comment