Friday, June 21, 2013

PINDA ASEMA MUWAPIGE TU! WAAMBIWA WANAOKAIDI


Kauli ya Waziri Mkuu Pinda: "Nasema wapigwe tu,...tumechoka..."


DODOMA/DAR ES SALAAM.
WAZIRI Mkuu, Mizengo Pinda (Pichani) ameagiza vyombo vya dola kuwashughulikia kwa kuwapiga wale watakaokataa kutii amri wakati wakifanya vitendo vya uvunjifu wa amani.

Akizungumza katika Kipindi cha Maswali ya Papo kwa Hapo kwa Waziri Mkuu, bungeni Dodoma jana, Pinda alisema watu wanapokaidi wanajitakia matatizo na vyombo vya dola.

Alisema hayo alipokuwa akijibu swali la nyongeza la Mbunge wa Kilwa Kaskazini (CCM), Murtaza Mangungu aliyeuliza: “Serikali ipo tayari kiasi gani kubainisha na kuch
ukua hatua stahiki, badala ya kusakama makundi fulani, tujue chanzo halisi cha vurugu hizi na matatizo haya na jinsi gani vyombo vya dola vinavyoshughulikia kwa sababu yapo malalamiko katika baadhi ya maeneo kama Mtwara kwamba wananchi wanapigwa na vyombo vya dola?”

Waziri Mkuu alijibu: “Ni lilelile nililosema... mwishowe unaona anasema vyombo vya dola vinapiga watu. Ukifanya fujo, umeambiwa usifanye hiki, ukaamua kukaidi, utapigwa tu... hamna namna nyingine, maana wote tukubaliane kwamba nchi hii tunaiendesha kwa misingi ya kisheria.

“Sasa kama wewe umekaidi, hutaki unaona kwamba ni imara zaidi... wewe ndiyo jeuri zaidi watakupiga tu.... Mimi nasema muwapige tu, kwa sababu hakuna namna nyingine... maana tumechoka.”

Pinda alisema Serikali imedhamiria kurejesha amani nchini ikiwamo mkoani Mtwara na kuwataka Watanzania waiache Serikali ifanye kazi hiyo. Alisema Serikali ina orodha ya watu wanaosemekana kuwa ni vyanzo vya vurugu na matatizo yaliyotokea Mtwara na kushangaa wale wanaopinga kukamatwa kwao.

“Lazima tuwakamate na kama katika kuwakamata watafanya jeuri, jeuri, watapigwa tu kabla ya kupelekwa tunapotakiwa kuwapeleka, kwa sababu hatuwezi kuendelea na hali hii, mkadhani kwamba tutafika tunapokwenda. Nami nasema vyombo vya dola vijipange imara vihakikishe vinadhibiti hali hii,” alisema.

Hata hivyo, jibu hilo lilipata upinzani wakati Mbunge wa Konde (CUF), Khatibu Said Haji alipomwuliza Waziri Mkuu: “Hapo awali umetoa kauli nzito ya kuliambia taifa hili kwamba wale raia wote, ambao watakaokuwa wakaidi wapigwe tu na watapigwa tu; naomba ninukuu Katika Ibara ya 13 na Kifungu cha 6B cha Katiba ya Jamhuri ya Muungano.

“Ni marufuku kwa mtu yeyote aliyeshtakiwa kwa kosa la jinai kuteswa kama mtu mwenye kosa, mpaka itakapothibitika anayo hatia kwa kutenda kosa hilo.

“Pia ibara hiyohiyo Kifungu cha 6 E; kinasema ni marufuku kwa mtu yoyote, kuteswa, kuadhibiwa kinyama au kupewa adhabu zinazoweza kumdhalilisha. Kwa kauli yako uliyoitoa huoni kwamba umevunja Katiba?” Akijibu swali hilo, Pinda alisema ni lazima kutofautisha kati ya mtu aliyekwishakamatwa na kufikishwa mbele ya vyombo vya sheria... 

“Mimi ninayemzungumza hapa ni mtu yule ambaye ameamua kufanya vitendo hajakamatwa na ndiyo maana nilikwambia usiandamane... hapa mahali hutakiwi kwenda wewe ukaamua kutumia mabavu kwa sababu mko wengi, ndiyo maana nikasema, hawa watu tutashughulika nao hivyohivyo.”

Mbunge huyo hakuridhishwa na majibu hayo na kumtaka Waziri Mkuu kuyafuta.

Hata hivyo, Spika wa Bunge, Anne Makinda aliingilia kati na kumweleza mbunge huyo kuwa kila mtu alikuwa amemwelewa Waziri Mkuu na hakukuwa na haja ya kuendelea na hoja hiyo
Via /jumamtandabog

No comments:

Post a Comment