Wednesday, June 5, 2013

'DEMOKRASIA' CHAMA CHA 21 CHA SIASA CHAPATA USAJILI WA KUDUMU TANZANIA

 
 
untitled2 a04a9
Msajili wa Vyama vya Siasa Nchini, John Tendwa (kulia) akizungumza na wana CHAUMMA
 untitled4 54d1f
Tendwa akikabidhi cheti cha usajili CHAUMMA
untitled b177f
Baadhi ya wanachama cha CHAUMMA pamoja na viongozi wao wakishangilia baada ya kupewa usajili
 
Na Thehabari.com
  MSAJILI wa Vyama vya Siasa nchini, John Tendwa amekipa usajili wa kudumu Chama cha Ukombozi wa Umma (CHAUMMA) huku akivitaka vyama vya siasa kufuata sheria na kuepuka kuwa vyanzo vya vurugu na uchochezi wa migogoro.
Tendwa ameyasema hayo leo jijini Dar es Salaam alipokuwa akiwakabidhi cheti cha usajili wa kudumu viongozi wa chama kimpya cha kinachojulikana kama Chama cha Ukombozi wa Umma.

Alivitaka vyama vya siasa kuhakikisha vinatimiza malengo yao ya kushika dola na hata kama itashindikana kwao, basi kuhakikisha wanapata nafasi za uwakilishi wa wananchi zikiwemo za udiwani, ubunge pamoja na uongozi wa serikali za mitaa kwa mujibu wa taratibu za nafasi hizo.

Alisema kwa sasa vipo vyama vya siasa ambavyo licha ya kuwa na usajili wa kudumu na uongozi mzuri usio na migogoro vimeshindwa kutimiza malengo ya msingi ya chama kwa kushika nafasi za uwakilishi maeneo anuai kwa mujibu wa utaratibu.

"...Vyama hivi unakuta hawana mbunge, hawana diwani, hawana viongozi serikali za mitaa, kijiji na kwingineko lakini ukiangalia wana viongozi wazuri hawana migogoro ndani ya chama, haya sio madhumuni ya chama cha siasa," alisema Tendwa.

Aidha aliwataka viongozi wa CHAUMMA kuhakikisha wanajipanga vizuri ili waweze kutimiza malengo ya chama na kuwawakilisha wananchi maeneo mbalimbali ya uongozi kisiasa. Alisema katika mapendekezo mapya ofisi yake inafikiria kuanza kuvipunguza vyama ambavyo licha ya kuwa na usajili havifanyi chochote kama ilivyo kwa madhumuni ya kuanzisha chama.

"Sheria inafanyiwa marekebisho, chama kikikaa ndani ya miaka mitano hakijafanya chochote tunafikiria kukifuta, kiongozi wa chama akitukana miezi sita unafungiwa kwa muda...maana hatuwezi kuruhusu matusi, vurungu na masuala mengine yasiokuwa na msingi ndani ya vyama vya siasa," alisema Tendwa.

Hata hivyo amesema katika mapendekezo yao ya mabadiliko ya katiba wamependekeza mambo mengi ikiwemo sasa kuruhusu vyama kujiunga na kufanya shughuli za siasa kama ilivyo kwa nchi za Kenya, Afrika Kusini, Lethoto na nchini Namibia.

Akizungumza mara baada ya kukabidhiwa cheti cha usajili wa kudumu Mwenyekiti wa muda wa CHAUMMA, Wallance Mayunga alisema wamejipanga vizuri katika kuwatumikia wananchi na chama chake kinatambua changamoto zilizopo nchini katika uongozi, utendaji na utawala hivyo kina nia ya kuleta mabadiliko.

Nafasi ya Katibu Mkuu wa muda wa CHAUMMA inashikiliwa na Shaffii Abed huku Hamad Tao akiwa ni miongoni mwa wanachama waanzilishi wa nchama hicho

No comments:

Post a Comment