Sunday, June 2, 2013

ACHENI DHULUMA WANA CCM - ASEMA KINANA



Katibu Mkuu CCM Taifa, Kinana akihutubia Uwanja wa Majimaji leo



Na Nathan Mtega,Songea

 VIONGOZI wa chama cha mapinduzi wametakiwa kuacha kusimamia vitendo vya dhuluma ndani ya chama na nje ya chama kwa sababu kufanya hivyo ni kukiua chama kama ilivyotekea katika baadhi ya maeneo hapa nchini ikiwemo wilaya ya Songea mjini ambapo chama cha mapinduzi kimepoteza kata sita katika chaguzi mbali mbali za udiwani.

 Hayo yamesemwa na katibu mkuu wa chama cha mapinduzi taifa Abdulraman Kinana wakati akizungumza na viongozi wa chama cha mapinduzi kuanzia ngazi ya shina hadi mkoa kwenye ufunguzi wa mkutano wa wajumbe wa mkutano huo ambao ni pamoja na mabalozi wa nyumba kumi uliofanyika kwenye uwanja wa Maji maji mjini Songea ambapo alisema kuwa vitendo vya dhuluma ambavyo vimekuwa vikifanywa na baadhi ya viongozi na watendaji dhidi ya wanachama ndivyo vinavyokigharimu chama.

 Alisema kuwa vitendo hivyo vya dhuluma vimekuwa vikijitokeza zaidi nyakati za uchaguzi kwa kutumia lugha ya kupanga safu kwa ajili ya manufaa ya kundi fulani bila kuzingatia matakwa ya wanachama na hivyo wanachama huamua vinginevyo na kusababisha chama kushindwa katika chaguzi ambazo vitendo hivyo viliendekezwa na mfano ni jimbo la Songea mjini mkoani Ruvuma.

 Aidha katika hatua nyingine Kinana aliwataka watendaji wa chama kuacha tabia ya umangimeza kwa kutumia muda mwingi kukaa ofisini na kutatua matatizo na kero za wananchi wakiwa ofisini bila kufika kwenye maeneo ambayo wanachama na wananchi wapo na kero za muda mrefu zinazohitaji utatuzi wao.

 Alisema kuwa watendaji wanapaswa kwenda mara kwa mara kwa wanachama kuwailikiliza maoni na mawazo yao badala ya kukaa ofisini na kukutana na kundi dogo ambalo hutoa taarifa zisizo sahihi kuhusu mwenendo wa chama kwenye baadhi ya maeneo aliongeza kuwa yeye ameamua kuzunguka nchi nzima kwa ajili ya kuona na kufuatilia utekelezaji wa ilani ya uchaguzi ya chama cha mapinduzi na mkoani Ruvuma atarudi tena kwa ajili ya kazi hiyo.

 Naye Mbunge wa jimbo la Songea mjini na Waziri wa mambo ya ndani Emmanuel Nchimbi akifunga mkutano huo alisema kuwa nchi ya Tanzania ni moja na inatakiwa iendelee kuwa moja bila kujali iktikadi za kidini na kisiasa lakini kundi ambalo halitaki nchi iendelee kuwa moja na serikali haitavumilia vitendo vya aina hiyo.

 Alisema kuwa utawala wa sheria ndiyo unaopaswa kuungwa mkono na kila mmoja mwenye mapenzi mema na nchi kwa sababu ndiyo msingi wa nchi ulioasisiwa na waasisi wa taifa na ndiyo uatakaoendeleza utaifa na si vinginevyo,pia alimshukuru katibu mkuu Kinana kwa kazi nzuri anayoifanya ya kurudisha na kuimarisha uhai wa chama.

Mwisho.

No comments:

Post a Comment