Wednesday, June 12, 2013

MAAJABU YA LWAKATARE ALIWEKWA LUPANGO MARCH 11 APATA DHAMANA JUNI 11 MWAKA HUU

ANGALIA PICHA: Ndugu,marafiki, viongozi wa Chadema wakishangilia kupewa dhamana: KUMBUKA wakati Lwakatare apata dhamana, Ludovick akwama.
Dar es Salaam. Baada ya kusota rumande kwa takriban miezi mitatu, hatimaye Mkurugenzi wa Ulinzi na Usalama wa Chadema, Wilfred Lwakatare ameachiwa kwa dhamana.
Hata hivyo, mwenzake Joseph Ludovick ambaye wanashtakiwa pamoja, alikwama kupata dhamana baada ya wadhamini wake kushindwa kuwa na vielelezo vyenye vigezo kulingana na masharti ya dhamana
hivyo alirejeshwa rumande.Baada ya Lwakatare kuachiwa, alipokewa kwa shangwe na wafuasi wa Chadema waliokuwa na mabango yenye maandishi mbalimbali ya kuelezea furaha yao na mengine yakikiponda chama tawala CCM, huku wakimshangilia kwa kuimba: “peoples’ power... peoples’ power!” wakiwa na maana ya nguvu ya umma.
Akitoa uamuzi kuhusu dhamana hiyo, Hakimu Mkazi wa Mahakama ya Kisutu, Aloyce Katemana alisema imetolewa baada ya kuzingatia kigezo cha washtakiwa kufutiwa mashtaka ya ugaidi ambayo yalikuwa yanaangukia kwenye sheria inayozuia dhamana.
Aliwataka washtakiwa kuwa na wadhamini wawili wanaoaminika na wanaotoka katika taasisi zinazotambulika kisheria.
Sharti lingine ni kila mdhamini kutia saini hati ya udhamini ya Sh10 milioni pamoja na washtakiwa wenyewe.
Hakimu huyo pia aliwataka washtakiwa kusalimisha hati zao za kusafiria mahakamani na kutokutoka nje ya Dar es Salaam bila ya kuwa na kibali cha Mahakama.
Hakimu Katemana aliiahirisha kesi hiyo hadi Juni 24, mwaka huu itakapotajwa tena kwa lengo la kujua iwapo upelelezi umekamilika ili ipangiwe tarehe ya kuanza kusikilizwa.
Awali, uamuzi huo wa dhamana ulipangwa kutolewa Mei 13, mwaka huu lakini ulikwama baada ya Katemana kuripotiwa kuwa likizo na badala yake, Hakimu Mkazi Sundi Fimbo aliitaja tu kesi hiyo na kuiahirisha.
Mei 27, mwaka huu ilitajwa tena hata hivyo uamuzi wa dhamana haukutolewa.
Awali, Lwakatare kupitia kwa mmoja wa mawakili wanaomtetea, Peter Kibatala aliwasilisha maombi ya dhamana mahakamani hapo Mei 13, mwaka huu wiki moja baada ya Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam kumfutia mashtaka matatu ya ugaidi yaliyokuwa yakimkabili.
via/jumamtanda blog

No comments:

Post a Comment