Thursday, June 6, 2013

DC - ALIA NA KUIMARISHA MIFUMO YA UTEKELEZAJI MAJUKUMU - SONGEA



Mkuu wa Wilaya ya Songea, Joseph Joseph Mkirikiti, akisoma Utekelezaji wa ilani ya CCM 2010 kwa wanachama viongozi wa Chama  Cha Mapinduzi katika Mkutano uliofunguliwa na Katibu Mkuu wa CCM taifa, Abdurahman Kinana na kufungwa na Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, ambaye ni Mbunge wa Jimbo la Songea Mjini, Dkt. Emmanuel Nchimbi Jumapili 2, Juni 2012

Na Juma Nyumayo, Songea
KUELEKEA kumaliza mwaka mmoja wa kuwepo madarakani, Mkuu wa Wilaya ya Songea, Bw Joseph Joseph Mkirikiti amesema anaendelea na mkakati wa kutathimini kazi yake kwa mitindo mbalimbali ikiwa ni pamoja na tathimini anayoifanya ofisini kwake kwa kuwauliza watumishi mmoja mmoja, makundi na kuangalia namna ya utendaji wa watu na taasisi wilayani Songea.
 
DC Mkirikiti,  alipoteuliwa  kushika wadhifa huo, alikutana na waandishi  wa Habari mkoani hapa na  kuwaambia mikakati yake ikiwa ni pamoja na kumtaka kila mtu kwa nafasi yake wilayani Songea kuwajibika, sasa anakaribia kumaliza mwaka mmoja akiwa kazini kwa wadhifa huo na kupima utendaji wake.
 
Akijibu swali la waandishi wa habari Ofisini kwake jana kama ameridhishwa na malengo aliyojipangia hasa kuhusu uwajibikaji, DC Mkirikiti, amesema ameridhishwa na atawaita waandishi wa habari kutoa tathimini yake na sasa amefikia hatua ya kuimarisha mifumo ya kiutendaji.
 
"Kumbukeni wakati ule mara kwa mara nilikuwa natembelea vituo vya afya, maeneo machafu, machinjio ... na ikumbukwe huko kote kuna watendaji wahusika, shida ni kuimarisha mifumo hii kiutendaji na upashanaji habari," alisema Mkirikiti .
 
Akiueleze Mgogoro wa wachinja ng'ombe na maafisa wa mifugo wa Manispaa ya Songea, DC huyo aliendelea kusisitiza kuwa shida kubwa ya kuzuka kwa mgogoro huo ni kukosekana kwa mfumo imara wa mawasiliano ili kulishughulikia tatizo hilo bila kukwazana.
 
"hapa tuwangoje wenzetu wa Chama cha wachinjaji na Uongozi wa Manispaa wakae kesho (akimaanisha leo) tupate ufumbuzi," alisema.
Mgogoro wa wachinjaji na maafisa wa Mifugo wa Manispaa ya Songea uliibuka juzi usiku baada ya maafisa hao kuvunja zizi la  kuhifadhia ng'ombe kabla ya kuchinjwa katika Machinjio ya Msamala Manispaa ya Songea ambapo wachinjaji hao walitishia kusitisha kuchinja ng'ombe na kusababisha wananchi kukosa kitoweo hicho.  


No comments:

Post a Comment