Monday, April 8, 2013

JELA MIEZI SITA KISA KUWAKATAZA WATOTO WASIJIUNGE SEKONDARI ZA KATA


Na Steven Augustino, Tunduru

MWENYEKITI wa Serikali ya Kijiji cha Mchekeni  kata ya Marumba Wilayani Tunduru Mkoa wa  Ruvuma,  Saidi Ally Makunganya,  amehukumiwa kutumikia kifungo cha miezi 6 Jela baada ya kupatikana na hatia katika kosa la uchochezi na kuwaachisha watoto shule.

Akitoa hukumu hiyo, hakimu wa Mahakama ya mwanzo  Mlingoti,  Bw. Kavula James  Kayabu,  alisema kuwa katika shauri hilo Mahakama yake imejiridhisha na ushahidi uliotolewa na upande wa mashitaka ulioongozwa na Diwani wa Kata hiyo,  Mhe. Said Msenga na Mtendaji wa Kijiji hicho,  Bw.Omari Mpinga.

Mheshimiwa Hakimu  Kayabu, aliendelea kufafanua kuwa katika shauri hilo  kuwa pamoja na mambo mengine pia mahakama hiyo ilichukua maamuzi hayo baada ya Mtuhumiwa huyo kuidharau Mahakama yake na kumtuma Mtoto wake kwenda kuitika kwa niaba yake na kusema uongo kuwa mlengwa hakuwepo Kijijini hapo na baada ya kumfuatilia wakamkuta akiwa nyumbani kwake.

Kwamujibu wa maelezo yaliyotolewa mahakamani hapo,  Makunganya alituhumiwa kuwashawishi na kuwashinikiza wazazi na walezi wa  watoto 43   kati ya watoto 45 waliochaguliwa kujiunga na masomo kidato cha kwanza  kutoka katikia Shule ya Msingi iliyopo Kijijini hapo kwa madai kuwa Shule za kata zimekuwa hazioneshi mafanikio mazuri katika ufaulu kwa watoto wao hivyo hata wakiwapeleka itakuwa ni kazi bure tu.

Kesi hiyo ni utekelezaji wa kesi 1, 064 zinazo wahusu wazazi na walezi walioshindwa kupeleka Watoto waliochaguliwa kujiunga na masomo ya Sekondari mwaka 2012 zikiwa ni juhudi za serikali kuhakikisha kuwa watoto wote waliochaguliwa kujiunga na masomo wanapelekwa shuleni.

Kwa mujibu wa taarifa zilizo tolewa na Mkuu wa Wilaya hiyo Bw. Chande Nalicho jumla ya watoto 2,764 walichaguliwa kujiunga na masomo hayo lakini cha kushangaza hadi sasa ni wanafunzi 1, 710 pekee ndio walioripoti na kuanza masomo ikiwa ni sawa na asilimia 63 % ya wanafunzi wote waliochaguliwa kijiunga na masomo mwaka 2013.         

 

 

No comments:

Post a Comment