Thursday, April 11, 2013

VIONGOZI WANAPOTETA KUHUSU MAENDELEO...UMAKINI HUTAWALA

Mkuu wa Wilaya ya Namtumbo, Bw. Abdallah Rutavi (Kulia) akisisitiza jambo wakati akiongea na Mheshimiwa Diwani wa Katata ya Namtumbo wilaya ya Namtumbo,  Bw. Alpius Mchucha, walipokutana ghafla eneo la Songea Club mjini Songea leo alipokuja kumpokea Balozi wa China nchini anayefanya ziara ya kikazi Mkoani Ruvuma. (Picha na Juma Nyumayo)

Na Muhidin Amri, Namtumbo.
WAZAZI washitakiwa kwa Mwenyekiti wa Maendeleo wa kata ya namtumbo kwa kushindwa kusimamia elimu ya watoto wao waliochaguliwa kujiunga sekondari.
mashitaka hayo yametolewa na Mkuu wa Shule ya Sekondari  ya kata ya Narwi wilaya ya Namtumbo, mkoani Ruvuma, Mwalimu  Bertha Kapinga, kwa Mheshimiwa Alpius Mchucha (Pichani juu).
Mwalimu Kapinga alisema wazazi wenye watoto wao shuleni hapo wana tabia ya  kuwakataza watoto  kuhudhuria masomo kwa muda muafaka kwa kile alichokieleza kuwa ni njia ya  wazazi hao kutaka kukwepa majukumu yao pindi watoto wao watakapoteuliwa kuendelea na masomo ya juu  na kusababisha shule hiyo kuwa na idadi ndogo ya wanafunzi wanaohudhuria masomo madarasani.
" hii ni njama ya kukwepa majukumu endapo wanafunzi hawa watateuliwa kuendelea na masomo ya juu," alilalamika Mkuu huyo wa shule ambayo wanafunzi wake wanatoka eneo lote la Namtumbo mjini.
Mwalimu Kapinga alisema hayo hivi karibuni shuleni hapo wakati akipokea msaada wa meza na viti hamsini toka kwa Benki ya NMB tawi la Namtumbo kufuatia shule hiyo kukabiliwa na upungufu wa samani na vifaa vya kufundishia na kujifunzia.
Alisema kuna baadhi ya  wanafunzi katika shule hiyo kuchagua siku za kuhudhuria masomo  na wanapobanwa wanatoa visingizio ambavyo moja kwa moja vinaelekezwa kwa wazazi wao.
Kutokana na malalamiko hayo, Mhe. Mchucha ameahidi kuchukua hatua ya kuzungumza na wazazi hao na kuona namna ya kuhamasisha ili kuleta mwamko wa elimu na matumizi ya sheria ya mahudhurio ya lazima kama ilivyo katika Sheria ya elimu na miongozo ya sharia za halmashauri hiyo.
Mkuu wa shule pia alisikitika kukosa michango mbalimbali ya shule na kusema kuwa ni ngumu kupata kutoka kwa wazazi hao jambo linaloifanya shule hiyo  kuwa na matatizo mengi ikiwemo nyumba za kuishi walimu,vyumba vya madarasa,ofisi za utawala ambapo wamelazimika kutumia hata  nyumba iliyojengwa kwa ajili ya mkuu wa shule kutumika kama ofisi  ya walimu hivyo mkuu wa shule kukosa  nyumba ya kuishi shuleni hapo jambo ambalo sio sahihi kitaaluma.

                      MWISHO

 

No comments:

Post a Comment