Tuesday, April 16, 2013

KESI YA LWAKATARE, MBOWE NA SLAA MAHAKAMA KUU

Mbowe, Slaa Watinga Mahakama Kuu kesi ya Lwakatare

Mwenyekiti wa Taifa Chadema, Freeman Mbowe, Katibu Mkuu wa Chadema, Wilbroad Slaa na Wakili wa Chama hicho Tundu Lissu wakitoka Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam kufuatilia kesi ya Lwakatare na Ludovick.Katika Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam watu mbalimbali wakiwamo wanachama na wafusi wa Chadema walifurika katika mahakama hiyo kufuatilia kesi Mkurugenzi wa Ulinzi na Usalama wa Chadema, Wilfred Lwakatare na mwenzake Ludovick Rwezahula Joseph wanaokabiliwa na kesi ugaidi.

Baada ya kufika katika mahakama hiyo wanachama hao wakiwamo waandishi wa habari walizuiliwa kuingia katika chumba maalimu kwa ajili ya kusikiliza kesi hiyo.

Maofisa wa mahakama hiyo wamesema chumba hicho hakina nafasi ya kutosha isipokuwa Mwenyekiti wa Taifa wa Chadema, Freeman Mbowe na Katibu Mkuu wa Chadema, Wilbroad Slaa ndio walioruhusiwa kuingia kusikiliza kesi hiyo.

Awali Lwakatare  na Joseph walipandishwa kizimbani katika mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu Machi 18 na kusomewa mashtaka manne yakiwamo ya ugaidi, katika kesi namba 37 ya mwaka 2013, wakituhumiwa kula njama na kupanga kumteka Dennis Msacky na kkumdhuru kwa kutumia sumu.

Pia Machi 20, 2013, Mkurugenzi wa mashtaka (DPP), aliwafutia mashtaka, lakini muda mfupi baada ya kutoka nje ya ukumbi wa mahakama walikamatwa na kufunguliwa mashtaka hayohayo katika kesi namba 6, ya mwaka 2013.

Baada ya watuhumiwa hao kufunguliwa mashtaka, mawakili wanaomtetea Lwakatare hawakukubaliana na uamuzi huo wa DPP, na kuwasilisha maombi Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam, wakipinga uamuzi wa DPP, na kuiomba  mahakama itengue uamuzi huo.

Maombi hayo yalisikilizwa jana na Jaji Lawrence Kaduri, lakini waaandishi wa habari na wafuasi na wanachama wa Chadema walizuiliwa kuingia ndani ya ofisini ya Jaji Kaduri yalimokuwa yakisikilizwa maombi hayo.

Mawakili waliokuwapo ni mawakili watatu wa Serikali, mke wa Lwakatare na Karani wa Jaji Kaduri.
Mbali na hayo baada ya waandishi kung’ang’ana sana kutaka kuingia, askari hao walimruhusu mwandishi mmoja tu kuwakilisha wandishi wengine.

Kwa kawaida kesi za jinai na hasa kesi zenye mvuto kwa umma kama hiyo huwa zinasikilizwa vkatika mahakama ya wazi, lakini jana haikufahamika kwanini waliamua kesi hiyo isikilizwe kwenye chumba kidogo (chamber).
 
Uamuzi wa kusikiliza maombi hayo katika chamber badala ya mahakama ya wazi ulizuwa manung’uniko na malalamiko kutoka kwa waandishi, wanachama wa Chadema na wafuasi wao, huku baadhi ya wafuasi wa Chadema wakiwaporomoshea matusi makali askari Polisi waliokuwa wakilinda usamalama mahakamani hapo.

Haya ndio yaliojadiliwa katika chumba hicho
Katika hatua nyingine, wakati wa kusikiliza maombi hayo upande wa mashtaka katika kesi ya msingi, ambao ni wajibu maombi, ulibainisha sababu mbili za DPP kuwafutia mashtaka Lwakatare na mwenzake.

Katika Mahakama hiyo wakili wa Serikali Mkuu, Prudence Rweyongeza aliyekuwa akisaidiana na mawakili wa Serikali waandamizi, Peter Maugo na Ponsiano Lukosi alizitaja sababu hizo kuwa ni kesi ya awali kufunguliwa katika masjala isiyostahili.

Wakili Rweyongeza alidai kesi ya kwanza ilisajiliwa katika kitabu cha kesi zinazosikilizwa na Mahakama za chini , badala ya kitabu cha kesi zinazosikilizwa na Mahakama Kuu.

Sababau ya pili alidai Mahakama kukosea kwa kuwaruhusu washtakiwa kujibu mashtaka ambayo husikilizwa na Mahakama Kuu tu.Mkurugenzi wa Ulinzi na Usalama wa Chadema, Wilfred Lwakatare akitoka Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam leo.

Alikuwa akijibu hoja za mawakili wa Lwakatare zilizotolewa na Wakili Peter Kibatala kuwa DPP alikosea kuchukua uamuzi huo kwa kuwa madaraka yake yana mpaka na kwamba hapakuwa na sababu wala mazingira yanayoelezwa katika sheria ya DPP kuchukua uamuzi huo.

Pia Wakili Kibatala akisaidiana na Wakili Tundu Lisu walihoji uhalali wa mashtaka hayo ya ugaidi wakidai kuwa hakuna maelezo yalionyesha kuwa mashtaka yanayomkabili Lwakatare na mwenzake ni ya Ugaidi. Kutoakana na hali hiyo waliiomba Mahakama Kuu iyatupilie mbali mashtaka hayo.

Hata hivyo Wakili Rweyongeza alidai ni mapema sana kutoa hoja za  uhalali wa mashtaka kwa kuwa kesi hiyo bado iko katika hatua ya uchunguzi na kwamba  baada ya uchunguzi inaweza kuwa na mabadiliko yoyote.

Hatima ya maombi hayo imebaki mikononi mwa Jaji Kaduri ambaye baada ya kusikiliza hoja za pande zote aliahirisha shauri hilo hadi atakapotoa uamuzi wake kwa tarehe ambayo atawajulisha wahusika wa kesi.
        Source: w.w.w. habarimasasi.com

No comments:

Post a Comment