KUJIAMINI:
Jumamosi ya leo haitaonekana tena. Jumamosi hii inaweza kuwa ni ukombozi kwako. Ni Jumamosi ambayo unaweza ukaitumia kupanga namna ya kufanikiwa kwa kutumia kichwa cha habari hapo juu cha kujiamini kwa lolote unalotaka kulifanya.
Kwanza, amini wewe ni wewe. Hakuna mwingine kama wewe. Kama unamuamini Mungu, na pia naomba umuamini Mungu.
Kama hujaaanza. Anza sasa, ili upate walao chembe ya kuijiamini kwa lolote unalofanya.
Mungu hafananishwi na chochote katika kujiamini na ndio maana akaumba alivyotaka na atakavyovitaka kwakuwa anajiamini kupita maelezo unayosoma hapa.
Kama umesoma au kusimuliwa Historia ya Utumwa, uliambiwa Muarabu mmoja aliweza kuwafunga minyororo watumwa kibao waafrika licha ya waafrika hao kuwa na maumbile makubwa, nguvu nyingi lakina walikosa KUJIAMINI kukataa biashara hiyo ya udhalilishaji.
Katika uchunguzi biashara hiyo bado inaendelea saana katika fikra zetu hasa waafrika.
Hatujiamini kwa shughuli tuzifanyazo ikiwa ni pamoja na mambo ya utawala, chakula tulacho na mambo kadha wakadha tunayoyafanya na kuyaona. Mfano: mtu kunywa togwa au kunywa pombe za kienyeji anaonekana kama mshamba vile mbele ya watu wa rika la sasa. Sio hivyo tu hata mitindo ya ngozi na nywele imeingizwa katika mfumo wa kuwafanya watu wengi hasa afrika wazalishe fikra za kutojiamini .
Ni kutojiamini kifikra. Bahati mbaya fikra ndiyo hutawala matendo na maono ya mtu.
TUFANYE NINI: Kwanza fikra huzalishwa na mtu mwenyewe. Unaweza kuzalisha fikra za woga, ukatili, hofu, kuonewa, kutumwa bila kujituma, umbea na wengine wanaweza wakazalisha fikra za kufanikiwa ambazo hujenga kujiamini kwa ambopo inategemea akili yako unaielekeza wapi.
Akili huelekezwa kutafuta kufikiri kulingana na mazingira uliyopo na wale wanaokuzunguka.
Ukifikiria huwezi, hutaweza kamwe. Maana hutatamani hata kujaribu hilo unalofikiria kuwa hutaliweza.
Mfano ni kijijini kwetu kuna familia ambazo hazijawahi kupanda chochote wakati wa msimu kwa kufikiria watashindwa kupata mbolea na visingizio vingine kibao.
Maisha yao ni shida. wamejiegemeza katika fikra za kushindwa kila kitu. hawataki kujaribu. Wanazalisha woga wa kutenda hivyo hawawezi kufanya badiliko lolote. Nilipoanza kazi miaka ya 80 huko vijijini wilaya ya Tunduru, nilishuhudia mtu amezalisha fikra za woga kuwa akinunua nguo mpya sharti aivae ndani ya nguo chakavu. Alikuwa anaogopa 'kurogwa' .
Alikuwa anazalisha woga uliomsababishia awe mchafu muda wote hata kama amenunua nguo mpya. Hakujiamini miaka njoo miaka nenda. Mtu kama huyo wapo pia katika familia zetu, jamii yetu. Wakiwa wengi hatutashuhudia mabadiliko ya kimaendeleo kwakuwa wengi hawatajiamini na wafanyacho matokeo ni kuzalisha fikra za kushindwa, woga, wivu, wasiwasi na kuamini kuwa hivyo walivyo ndio walivyo.
Tukatae hili kwa kuanza mabadiliko ya kujiamini kufikiri vyema na kutenda ili kuleta mabadiliko. yatupasa kuanza sasa.
Chao. Juma Nyumayo, Songea.
No comments:
Post a Comment