Monday, April 22, 2013

JUMBA LA KIFAHARI LA MCHUNGAJI,. MHE. GETRUDE LWAKATARE KUVUNJWA?

Wabunge walia na hekalu la Mchungaji Lwakatare
NYUMBA YA MCHUNGAJI GETRUDE LWAKATARE, MHESHIMIWA MBUNGE (VITI MAALUM - CCM)
Mchungaji Getrude Lwakatare (MB) Katikati akiw na MC siku ya Ufunguzi wa Jumba lake.

WABUNGE wamemtaka Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais, Mazingira Terezya Huvisa kuzivunja nyumba mbili zilizopo Mbezi Beach jijini Dar es Salaam zilizojengwa katika fukwe ya bahari ya Hindi ikiwemo ya mbunge licha ya kwamba kuna zuio la Mahakama.

Bila kutaja majina ya wamiliki hao, wabunge hao walitaka hatua hizo zichukuliwe kwa haraka kwa nyumba hizo zilizojengwa kwenye fukwe kinyume cha sheria zivunjwe kwa maelezo kuwa hazina ofa wala hati.

Sambamba na hilo wametaka watendaji wa Serikali waliohusika kutoa vibali kuruhusu ujenzi huo kwa maelezo kuwa walichukua rushwa wachukuliwe hatua.

Mbunge wa kwanza kuanza kuzungumzia hilo ni wa Viti Maalumu, Esther Bulaya (CCM) aliyetaja viwanja viwili vyenye namba 2019 na 2020 kikiwemo cha mbunge ambaye ni kiongozi wa kiimani waliojenga nyumba zivunjwe licha ya kuwepo zuio la Mahakama.

“Mwaka jana Waziri wa Ardhi, Profesa Anna Tibaijuka alivunja nyumba za kawaida licha ya zuio la Mahakama, lakini nyumba zilizo kwenye viwanja namba 2019 na 2020 hazikuvunjwa kwa sababu ya zuio la Mahakama hii ni double standard (ndumilakuwili) hatuwezi kuvumilia.

“Wengine wenye nyumba ni viongozi tupo nao humu tena wa kiimani, lakini kwa nini viongozi tunafanya hivi wakati tunatakiwa tuwe wa mfano na tunawafanya viongozi wenzetu washindwe kufanya kazi zao?… hakuna haja ya kuogopa Waziri Huvisa (Mazingira) vunja nyumba, haiwezekani kuwa na nguvu ya fedha.

“Wabunge wenzangu tuazimie Manispaa ya Kinondoni na NEMC (Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira), wakavunje nyumba hizo ndani ya wiki moja , naomba kutoa hoja,” alisema.

Hata hivyo, Spika Anne Makinda alimweleza; “Haiwezekani kutoa hoja kwa kuingilia vyombo vingine”.

Mbunge ambaye ni kiongozi wa kiimani mwenye nyumba katika eneo hilo la Mbezi Beach aliyejenga katika fukwe ya bahari kwa kuondoa mikoko na kuweka kifusi na kujenga nyumba ni Mbunge wa Viti Maalumu, Mchungaji Dk Getrude Lwakatare (CCM). Hata hivyo wakati wa michango hiyo mbunge huyo hakuwa ndani ya Bunge.


Naye Mbunge wa Viti Maalumu, Grace Kiwelu (Chadema) akichangia bajeti ya Ofisi ya Makamu wa Rais, alisema Kamati yake ya Ardhi na Mazingira ilitembelea eneo hilo la Mbezi Beach na kukuta aliyejenga katika kiwanja 2019 hakuwa na ofa wala hati.

“Ametumia pesa kuwarubuni watendaji akaondoa mikoko, akaweka kifusi na akajenga nyumba naomba Wizara ya Ardhi na ya Mazingira wawachukulie hatua watendaji hao,” alisema.

Akijibu hoja ya Bulaya, kuwa kwanini nyumba ya Mchungaji Lwakatare haikuvunjwa wakati nyingine zilivunjwa, Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Frederick Werema alisema: “Sisi ni wajibu wetu twende mahakamani kusema watu hao wamevunja sheria kujenga hapo.

Wao wanaruhusiwa na Katiba na Mahakama itafuata sheria. “Nashauri Bulaya usitoe Shilingi kuzuia Bajeti ya Waziri, uje tuone huyo kigogo itakuwaje.” Hata hivyo, Huvisa alisema: “Nyumba tulizovunja hazikuwa na kesi na hii tuliyoiacha ilikuwa na kesi.”

Jumba la kifahari linalodaiwa kuwa la Mchungaji Lwakatare ambalo lilizinduliwa mwaka jana, limekuwa likitajwa kuwa lina thamani ya takribani Sh bilioni 1.5.

chanzo; HABARILEO 

No comments:

Post a Comment