Monday, August 29, 2011

Maskini Diwani akamatwa akitetea ardhi ya wananchi



MASIKINI! POLISI WAMKAMATA DIWANI ANAYETETEA WANANCHI WASIPOKONYWE ARDHI MSHANGANO SONGEA

Na, Juma Nyumayo, Songea

JESHI la Polisi mkoani Ruvuma liliwakamata na kuwahoji zaidi ya masaa matatu wakazi wawili wa Kata ya Mshangano na Diwani wa kata hiyo Mheshimiwa Faustin Mhagama kupitia Chama cha Mapinduzi(CCM) (Pichani) kwa tuhuma za kutangaza maandamano ya amani ya wananchi wa kata hiyo wakidai kupimiwa ardhi yao na Kampuni ya Ardhi Plan na kumtaka Waziri mkuu Mizengo Pinda kuwatimua kazi Mkurugenzi wa Manispaa ya Songea na Afisa Mipango Miji wa Manispaa hiyo ambao wameonyesha dhahili kutaka kuwadhulumu maeneo yao.

Wakazi hao waliokamatwa na polisi ni Suzo Luoga ambaye alikuwa ni dereva wa gari ya matangazo lenye namba za usajili T 295 AJS aina ya Chesar mark II,Joseph Haule ambaye alikuwa mtangazaji na Faustine Mhagama ambaye ni Diwani wa kata hiyo ambao wote walikamatwa wakiwa kwenye gari hilo ambalo lilikuwa linapita kwenye mitaa ya kata hiyo kuwatangazia uwepo wa maandamano makubwa

Mmoja wa watuhumiwa hao Haule ambaye alikuwa mtangazaji alisema kuwa kazi hiyo alipewa na viongozi ambao wenyeviti wa serikali ya mitaa ya Namanyigu,Mshangano na Mitendewawa na kwamba shughuli hiyo ya utangazaji ilisimamiwa kikamilifu na Diwani wa kata lengo kuhakikisha ujumbe unawafikia wakazi wote wa kata hiyo

Naye wa Diwani wa Kata hiyo Mhe. Mhagama akizungumza na Mwandishi wa habari hii alikili kukamatwa na alidai kuwa yeye pamoja na wenzake walikamatwa na Polisi majira ya saa tatu usiku huko katika eneo la Bombambili Kadogoo wakitaka kuelekea Mshangano mara baada ya kumaliza matangazo yao na waliamriwa kuingia kwenye gari la Polisi wakiwa chini ya ulinzi mkali na kupelekwa kwenye kituo kikubwa cha Polisi

Alisema kuwa mara baada ya kufikishwa kituoni hapo waliamliwa kuvuliwa viatu,mkanda na kuanza kupekuliwa na kasha kuwekwa mahabusu ambapo baadae alifika Kaimu Mkuu wa Polisi wa Wilaya akiwa ameongozana na Askari Kanzu wawili ambao walianza kuwahoji hadi saa tano na nusu usiku ndipo walipoambiwa wawatafute watu wa kuwadhamini ambapo Mwenyekiti wa Kamati ya Mipango Miji wa Halmashauri ya Manispaa ya Songea James Makene pamoja na Diwani wa Viti maalum Rehema Milinga walifika kituoni hapo na kuwadhamini

Kwa upande wake Makene ambaye pia ni Diwani wa Kata ya Matarawe aliuambia mtandao huu kuwa kitendo cha kuwakamata Diwani na wenzake ni uonevu mkubwa na kinyume na utawala bora kwa kuwa Serikali ya Kata ya Mshangano ilipeleka barua ya kuomba kibali cha maandamano toka tarehe 19.8.2011 ambapo mpaka wanakamatwa walikuwa hawajapewa barua wala maelezo ya aina yoyote jambo ambalo liliashiria kukubaliwa

Naye Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Ruvuma Michael Kamuhanda alisema kuwa wananchi wa kata ya Mshangano waliomba kibali cha kutaka kufanya maandamano makubwa ya amani lakini katika barua yao ilionyesha mapungufu mengi ikiwa ni pamoja na kutoeleza tarehe,muda na njia ambayo maandamano yatapita

Kamuhada alisema kuwa tayari Serikali ya Kata ilipewa barua ya maelekezo na Jeshi la Polisi yenye kumbukumbu namba.SOA.3.6/65 ya tarehe 25.8.2011 ambayo ilipokelewa na Diwani wa kata hiyo majira ya saa mbili usiku
MWISHO


No comments:

Post a Comment