Tuesday, August 30, 2011

Gari lapinduka laua sita na kuwaunguza moto wawili wajeruhiwa



Sita wamekufa na kuteketea kwa moto baada ya gari lao kupinduka Mbinga
Na Juma Nyumayo, Songea

WATU sita wamefariki papo hapo na wengine wawili akiwemo mtoto wamejeruhiwa vibaya baada ya gari walilokuwa wakisafiria kupinduka na kuwaka moto katika kijiji cha Chunya kilichopo wilayani Mbinga mkoani Ruvuma.
Kamanda wa polisi mkoa wa Ruvuma Machael Kamuhanda (Pichani) amesema kuwa tukio hilo limetokea juzi (28.8.2011) majira ya saa 12 jioni.
Kamuhanda amebainisha miongoni mwa waliofariki miili yao kuwa imeuungua vibaya huku maiti hizo zikiwa hazitambuliki.
Kamuhanda alisema kuwa tukio hilo limehusisha Gari lenye namba za usajili T 270 BDG Landrover likiwa linaendeshwa na Dereva Stevin Ngoko (32) kupinduka na kuwaka moto na kusababisha vifo vya watu sita papo hapo katika kiji cha Chunya barabara iendayo Mbambabay toka Mbinga.
Kamanda Kamuhanda amewataja waliojeruhiwa katika ajari hiyo kuwa ni Jeremia Masalo (38) mkazi wa nchi jirani ya Msumbiji na Anna Godrfei (3) mkazi wa Mbambabay ambao wote wamelazwa katika Hospitali ya Serikali ya Wilaya ya Mbinga kwa matibabu.
Alisema kuwa watu waliokufa majina yao hayajaweza kufahamika kutokana na maiti hizo kutotambulika kwa kuwa zimeungua vibaya na zote zimepelekwa katika chumba cha kuhifadhia maiti katika hospitali ya wilaya hiyo.
Kamanda Kamuhanda alisema kuwa chanzo cha ajali hiyo ni mwendo kasi ambao ulimsababishia dereva wa gari hilo kushindwa kumudu usukani na kwamba jeshi lake linaendesha msako wa kumtafuta dereva wa gari hilo Bw. Ngoko ambaye alitoroka mara tu baada ya kutokea ajali hiyo.
MWISHO.

1 comment:

  1. Kwa masikitika makubwa napenda kutoa pole zangu kwa wafiwa wote na pia pole wote waliojeruhiwa. Mungu awape nguvu na matuini. Pia pole sana wanaruvuma. Tujirekebishe jamani kwa kuendesha polepole la sivyo tutakufa .....

    ReplyDelete