Tuesday, July 19, 2011

Wasichana 50 kurejeshwa nchini toka Msumbiji


Usafirishaji binadamu kutumikishwa nje kukomeshwa

Na Juma Nyumayo, Songea

SERIKALI mkoani Ruvuma imepania kukomesha kabisa biashara ya usafirishaji binaadamuna kuhakikisha inawarejesha wasichana wapatao 50 waliosafirishwa kinyume na sheria kwenda nchini Msumbiji kwa ushirikiano na vyombo vya usalama vya nchi hiyo jirani.

Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Ruvuma Michael Kamuhanda, alisema hilo alipohojiwa na Mwaandishi wa habari hii ambaye ni mwanachama wa mtandao wa kufuatilia masuala ya usawa wa Jinsia mikoa ya Nyanda za Juu Kusini.

Kamanda Kamuhanda, alisema hivi sasa wanahabari za kiintelijensia ambazo zitatumika kuwakamata wote waliopo kwenye mtandao huo hapa nchini na wale wanaoshirikiana nao Nchini Msumbiji kufanya biashara hiyo haramu inayodhalilisha utu.

“Tutatumia sheria ya kupinga biashara ya kusafirisha binaadamu, Sheria ya kutumikisha watoto na kwakuwa Tanzania na Msumbijji tunashirikiana kupitia Interpol na Ujirani mwema tulionao tutakomesha biashara hii,” alisema kamanda Kamuhanda.

Inasadikiwa kuna zaidi ya wasichana nje ya shule na wanafunzi wa shule za msingi na sekondari zaidi ya 50 waliosafirishwa kwenda maeneo ya Machimbo nchini Msumbiji kufanyishwa kazi za ukhaba katika madangulo na wakati mwingine kuchukuliwa picha za uchi.

Hata hivyo Kamanda Kamuhanda aliziomba taasisi mbalimbali wakiwemo, watu binafsi na Mtandao wa Jinsia nchini (TGNP) kushiriki kutoa elimu kwa wazazi na walezi wa watoto hao madhara ya kukubali kuwakabidhi watu kwa ulaghai wa kupata mshahara mnono huko nchi jirani jambo ambalo amethibitisha kuwa ni vigumu kupatikana.

“Kule hakuna mshahara ni mateso matupu, na tukibaini mzazi au mlezi ameshiriki tutamchukulia hatua za sheria,” alisema Kamuhanda.

Wakati huohuo, Mkuu wa wilaya ya Namtumbo Saveri Maketta amechukua hatua ya kuwaelimisha watu waishio mpakani kandokando ya mto Ruvuma kuhakikisha wanatoa taarifa kwa vyombo vya dola au maafisa watendaji pale watakapoona wasichana wanavushwa ng’ambo ya Msumbiji kwa lengo la kwenda kufanya kazi zisizojulikana.

“Tumewaambia huyo mwajiri awe mwafrka au mzungu lazima serikali yetu ifahamu, na kwamba Kivuko cha Magazini kinaimarishwa kuzuia usafirishaji wa binadamu,” alisema Maketta.

Hivi karibuni Jeshi la Polisi mkoani Ruvuma likishirikiana na polisi wa Msumbiji waliwarejesha wasichana wanafunzi wa sekondari wawili waliosafirishwa kinyume na sheria kwenda machimbo ya Tulo nchini Msumbiji.

Mwisho.

No comments:

Post a Comment