Tuesday, July 19, 2011

Mfumo Dume bwana,, wilaya ya Namtumbo kiboko!

HAPA NI BAADHI YA WANAWAKE WALIOTELEKEZWA NAMTUMBO WAKIWA NA WATOTO WAO KAMA WALIVYOKUTWA NA KAMERA YETU.


Wanaume watelekeza familia, kukwepa majukumu

Na Juma Nyumayo, Namtumbo.

UMEZUKA mtindo wa wanaume hasa vijana kuwakimbia wasichana waliowapatia ujauzito na kutelekeza familia kuwaweka wanawake na watoto katika hali ngumu kimaisha wilayani Namtumbo mkoa wa Ruvuma.

Wasichana na akina mama waliohojiwa na mwandishi wa habari hii wamekili kutelekezwa na kuamua kuishi kwa wazazi walikotoka baada ya vijana hao kuwakimbia wakiwa wajawazito na wengine wakiwa wamejifungua na kuwaachia majukumu yote ya kugharimia matunzo ya mamba na hatimaye watoto.

Mmoja wa aliyekimbiwa akiwa na ujauzito na sasa amejifungua, Blandina Mbawala (17) alisema anapata shida na mtoto wake hasa akipata homa wakati wa usiku, kwani hivi sasa huduma zote zinatolewa na dada yake Donatha Mbawala ambaye naye analea kachanga ka mwezi mmoja na katorokwa na mumewe.

“Huyo Bwana kanikimbia, naishi na dada yangu anayenisaidia kulea mwanangu,” alisema Blandina ambaye bado hana ujuzi wa malezi kulingana na umri wake mdogo.

Akizungumzia tatizo hilo ambalo linaweza kusababisha kuporomoka kwa ustawi wa familia wilayani Namtumbo, Rashidi Tuppa mkazi wa Mjini Namtumbo alisema vijana wengi wilayani hapo wanamtindo wa kukwepa majukumu ya kutunza familia na kuwaachia wazazi wao au wanawake.

“Vijana wengi wa kiume wanaotelekeza familia hawapendi kufanya kazi ili wajikimu kimaisha, na hivyo kukwepa majukumu ya kuhudumia wachumba waliowapatia ujauzito au watoto,” alisisitiza Tuppa.

Fairuna Runje mkazi w Minazini Namtumbo anailalamikia tabia hiyo si kwa vijana wa kiume tu bali kwa wanaume watu wazima pia wana mtindo huo wa kukwepa majukumu ya kazi na kungojea kuhudumiwa na wake zao.

“Hawa wanaume waliotuoa ni kama njiwa wanasubiri kulishwa kwenye tundu, hawafanyi kazi kazi ya kuoa wanawake wawili hadi watano ili tushindane kuwahudumia,” alisema Fairuna.

Mkuu wa wilaya ya Namtumbo, Saveri Maketta, amekili kuwa licha ya mfumo dume unowakabili wakazi wa wilaya hiyo wa kuwakandamiza wanawake katika shughuli za uzalishaji mali na malezi bado wananchi wa wilaya hiyo wanahitaji elimu ya uamsho wa usawa wa kijinsia ili kuleta maendeleo na maisha bora kwa kila mwana Namtumbo.

“Mfumo dume ni tatizo kubwa wialayani kwangu na hivi mwanamke anabebeshwa kila shughuli wakati wanaume hutumbua maisha,” alisema Maketta.

Alisema hivi sasa katika kila kikao anachohutubia anawaeleza madhara ya mfumo dume katika kuchachamua maendeleo ya wakazi wa wilaya hiyo.

Mwisho.

No comments:

Post a Comment