Toka kulia: Rais wa sasa Afrika kusini, Jacob Zuma , Rais wa kwanza mweusi wa Afrika kusini, Mzee Nelson Mandela (enzi ya uhai wake) na Rais wa pili wa Afrika Kusini, Thabo Mbeki |
Ndugu Zangu.
Nahitimisha simulizi za Mzee Wetu Madiba. Najisikia nimechukua jukumu langu la kugawana nanyi kile kidogo nilichoweza kukusanya kumhusu Mzee wetu Madiba.
Natumaini nitapata muda siku zijazo, nisimulie zaidi juu ya yale yenye kufanya maisha ya Madiba kuwa simulizi endelevu kwetu Waafrrika na watu wa dunia.
Lakini, ukweli unabaki, kuwa leo dunia imemzika Mzee Madiba kijijini kwao Qunu. Yaliyobaki nyuma yake ni yale mema aliyoishi akayahubiri. Nasi tunapaswa kujifunza kutoka hayo.
Yumkini Mungu amechagua kupumzisha Mandela wakati muafaka. Maana, ni katika kipindi ambacho, Afrika Kusini inaelekea kwenye Uchaguzi Mkuu wa mwakani.
Chama kikuu cha ANC kinakabaliwa na changamoto za ndani ya chama na kwenye jamii. Kinapaswa sasa kijiandae kufanya mabadiliko makubwa yatakayorudisha imani ya wapiga kura wake wengi. Wapiga kura ambao wameanza kukata tamaa. Hawana furaha ya maisha yao. Wamekata tamaa ya kuona kuwa kesho yao yaweza kuwa bora zaidi.
ANC kihistoria imekuwa ikitegemea sana Jumuiya yake ya Vijana na Shirikisho la Wafanyakazi ( Cosatu) Jumuiya zote hizo zinaonekana kugawanyika. Kuna wanaoipa mgongo ANC.
Na Mandela anausia;
" The leader must keep the forces together, but you can't do that unless you allow dissent. People should be able to criticise the leader without fear of favour. Only in that case are you likely to keep your colleagues together"- Nelson Mandela. It is when Mandela gave a piece of advice to newly elected Party Leader, Thabo Mbeki at the ANC Congress in Mafikeng, 1997.
Kwamba kiongozi unapaswa kuyaunganisha makundi, lakini, huwezi kufanya hivyo kama huruhusu sauti kinzani. Sauti za wenye kukupinga. Watu wawe huru kumshutumu kiongozi bila ya woga. Ni kwa namna hiyo tu kiongozi unaweza kuyaunganisha makundi. Mandela aliyasema hayo kule kwenye Mkutano Mkuu wa ANC uliompitisha Thabo Mbeki kuwa Rais wa ANC, ni mwaka 1997.
Naye Askofu Desmond Tutu alipata kusema;
"Kuna tofauti ya kimsingi kati ya kuwa huru na kuwa katika hali ya kukandamizwa. Kuwa huru ni pamoja na kupata huduma za msingi za kijamii, kuwa na ajira, maji ya bomba, umeme, makazi bora na huduma za msingi za afya. Kuna maana gani basi ya kuwa huru wakati ubora wa maisha ya watu haujaimarishwa? Kama sivyo, hata kura nazo hazina maana yoyote!" (Desmond Tutu- William Gumede; Thabo Mbeki And The Battle For The Soul Of The ANC, Uk. 67).
Nkosi Sikelel i Afrika
Kwa hisani ya Juma Mtanda
No comments:
Post a Comment