|
Ukumbi wa Bunge, Dodoma |
DODOMA/DAR ES SALAAM. WABUNGE 160 wa CCM wamejiorodhesha kuomba kuitishwa kwa kikao cha Kamati ya Wabunge hao kwa lengo la kuwajadili mawaziri wanaotajwa kuwa mizigo.
Pia wabunge hao wanataka Katibu Mkuu wa CCM, Abdurahaman Kinana naye awepo kwenye kikao hicho.
Mjumbe wa Kamati ya Uongozi wa Kamati ya Wabunge wa CCM, Hussein Mussa Mzee, alimwambia mwandishi wetu kuwa wamepokea barua iliyoambatana na orodha ya majina ya wabunge zaidi ya 160 waliotia saini kutaka kuitishwa kwa kikao hicho.
“Hata kama wangesaini wabunge 10 tu tungeitisha kikao. Bahati nzuri walisaini zaidi ya 160, kwa hiyo kikao kitaitishwa kwa kuwa ni haki yao kikanuni kutaka kukutana,” alisema.
Alipoulizwa kwa nini kikao hicho hakikuitishwa ndani ya wiki moja ambao ndiyo muda wabunge hao walioutaka kabla ya Kamati Kuu ya CCM kukutana wikiendi iliyopita, Mzee alisema hiyo lilitokana na Mwenyekiti wa Kamati ya Wabunge wa CCM, Waziri Mkuu Mizengo Pinda, kutokuwapo bungeni.
Mzee alisema pia kikao hicho kilishindwa kufanyika mara ya kwanza kutokana na Kinana kuwa safarini Afrika Kusini ambako alihudhuria mazishi ya Rais wa zamani wa Afrika Kusini, Nelson Mandela.
Hata hivyo, alisema hawezi kujua ni lini kikao hicho kitafanyika lakini aliahidi kuwa itakuwa mara baada ya Kinana kurejea nchini.
Wiki iliyopita, gazeti hili liliandika kuhusu wabunge wa CCM kujiorodhesha ili kushinikiza kufanyika kwa kikao hicho.
Chanzo kimoja cha kuaminika kilisema kuwa fomu hiyo iliwasilishwa katika Ofisi ya Katibu wa Wabunge wa CCM ikiambatana na barua inayotaka kuitishwa kwa kikao kitakachowakutanisha.
“Tuliwaomba waitishe kikao cha wabunge wa CCM ili mawaziri ambao tunawaona hawatimizi majukumu yao kikamilifu waweze kuhojiwa lakini wakawa wanasuasua,” kilisema chanzo hicho.
Kikao hicho kilitakiwa kufanyika Alhamisi iliyopita ili kuwahoji mawaziri hao kabla ya kikao cha Kamati Kuu.
Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Nape Nnauye alikaririwa wikiendi hii akieleza kuwa mawaziri saba walihojiwa katika kikao cha Kamati Kuu na kumuachia Rais Jakaya Kikwete jukumu la kuamua kuwafukuza kazi, kuwahamisha au kuwataka kutekeleza majukumu yao kikamilifu. MWANANCHI