Wednesday, October 19, 2011

AHIMIZA HAKI ZA BINADAMU

MKUU WA MKOA AHIMIZA WANANCHI KUHESHIMU HAKI ZA BINADAMU
Na Stephano Mango,Mbinga
WANANCHI Wilayani Mbinga mkoani Ruvuma wametakiwa kuheshimi haki za binadamu kwa kuzingatia kanuni,taratibu na sheria ili kila mtu aweze kuishi kwa amani na upendo katika jamii yake na nchi kwa ujumla
Wito huo umetolewa jana kwenye Viwanja vya Magereza Kitai na Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma Said Mwambungu mara baada ya kupokea taarifa ya maendeleo ya Halmashauri ya Wilaya ya Mbinga iliyosomwa na Mkurugenzi wa Halmashauri hiyo Shaib Mnunduma
Mwambungu ambaye yupo kwenye ziara ya kikazi ya siku moja Wilayani Mbinga alisema kuwa kila siku ninaposoma taarifa ya maendeleo ya mkoa nakutana na taarifa ya vifo vya kujinyonga,kupigana,kuchinjana kutokanana na mahusiano ya kimapenzi na matatizo mengine ya kijamii na kwamba takwimu za vifo vingi vinatoka Wilaya ya Mbinga
“Nasikitishwa sana na taarifa hizo kwani mtu unayempenda huwezi kumuua kwa sababu za kukunyima penzi au kumkuta mpenzi wako na mwanaume mwingine au na mwanamke mwingine hivyo kama kweli unampenda utamlinda na vishawishi vinavyoweza kupunguza upendo wake kwako na sio kumuua”alisema Mwambungu
Alisema kuwa haki ya kuishi ni haki kubwa kuliko zote na kwamba hakuna mtu mwenye mamlaka ya kuondoa uhai wa mwenzake kwa sababu yoyote ile kwani mwenye uwezo na mamlaka hayo ni mwenyezi mungu pekee yake ni vema kazi yake tukamuachia
Alisema kuwa jambo hilo halipaswi kuvumiliwa hata kidogo hivyo ni vema viongozi wa dini na wakijamii pamoja na Serikali kushirikiana kikamilifu kudhibiti jambo hilo kwani kabla vifo havijatokea kunakuwepo na dalili za kutokuwa na amani miongoni mwa wapenzi hao tujaribu kusuluhisha migogoro kwa taratibu za mila na desturi na kwamba ikishindikana basi sheria itumike kudhibiti vifo hivyo
Awali akisoma taarifa ya maendeleo ya Wilaya ya Mbinga Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya hiyo Shaib Mnunduma alisema kuwa katika mwaka wa fedha wa 2011/2012 Halmashauri imekadilia kutumia Tsh 39,600,654,467.00 kwa ajili ya kutekeleza miradi ya maendeleo na shughuli za utawala
Mnunduma alisema kuwa vipaumbele katika kutekeleza bajeti hiyo ni kuimarisha ukusanyaji wa mapato na kufikia lengo lililopangwa,kuimarisha utoaji wa huduma za afya kwa kufanya ukarabati wa Zahanati,Vituo vya Afya,Kupanua Hospitali ya Wilaya na kuhamasisha ujenzi wa Zahanati kwenye kila Kijiji
Aliitaja miradi mingine ni kuendeleza kilimo cha umwagiliaji na kuongeza uzalishaji wa mazao ya chakula na biashara,kuimarisha sekta ya mikopo kwa kuendeleza vyama vya kuweka na kukopa9Saccos),kufanikisha adhima ya kuwezesha wanafunzi wote waliofaulu elimu ya msingi kujiunga na elimu ya sekondari
Mnunduma aliongeza zaidi kuwa miradi mingine ni ya kuboresha huduma za jamii na kusaidia miradi iliyoibuliwa kwa mbinu shirikishi jamii hasa ile ya elimu,afya,kilimo,maji na barabara na kuimarisha shughuli za hifadhi ya mazingira na hasa upandaji miti,kuzuia uchomaji moto misitu na kuhamasisha kilimo cha ngoro na makinga maji
MWISHO

No comments:

Post a Comment