Thursday, February 6, 2014

SABUNI INAYODAIWA KUREJESHA UBIKIRA YAPIGWA "STOP"

WANAWAKE wameshauriwa kuacha kutumia sabuni za kunawia sehemu za siri ambazo hudaiwa kurejesha ubikira kwani zina madhara makubwa ikiwemo kusababisha kansa ya shingo ya kizazi.

Mkaguzi wa Dawa na Mfamasia wa Manispaa ya Dodoma Daria Mwanuka alisema hayo mwishoni mwa wiki katika mahojiano na mwandishi wa habari hizi wakati wa uteketezaji dawa, vipodozi na vyakula visivyofaa kwa matumizi ya binadamu.

Kazi hiyo ilifanywa na Mamlaka ya Chakula na Dawa (TFDA) Kanda ya Kati. Alisema kumekuwa na sabuni mbalimbali ikiwamo Kaisiki ambapo wanaoziuza wanadai zimekuwa zikisababisha bikira iliyopotea kurudi kitu ambacho si kweli.

“Sabuni hizo zinapunguza tu majimaji yaliyo sehemu za siri za mwanamke jambo ambalo husababisha wakati wa kufanya mapenzi mwanaume kupata ugumu kwenye muingiliano kwa vile mwili unakuwa umekataliwa kutoa maji na hivyo kuleta michubuko kitu ambacho ni hatari hasa wenye maambukizi ya magonjwa,” alisema.

Alisema michubuko inapotokea ni rahisi mwanamke kuambukizwa magonjwa ya zinaa hata virusi vya Ukimwi. Mtaalamu huyo alisema sabuni hizo zinatengeneza hali fulani ukeni lakini haiwezi kurejesha hali ya maumbile iliyopotea.

Alisema wanaotumia sabuni hizo wako katika hatari kubwa ya kuambukizwa magonjwa na hata kupata saratani ya shingo ya uzazi kwani kemikali zinazotumika katika kutengeneza sabuni hizo zina athari kubwa kiafya.

Alisema ni vyema wanawake wakatambua thamani yao na kuachana na matumizi ya sabuni hizo ambazo hazina manufaa yoyote na badala yake zimekuwa na madhara makubwa kwao.

Kwa upande wake, Fredrick Luyangi , Mkaguzi wa dawa kutoka TFDA alisema matumizi ya sabuni hizo huleta athari kubwa mwilini na wakati mwingine kutengeneza kansa taratibu bila mhusika kufahamu.

Alisema sabuni hizo husababisha kansa ya kizazi na kubainisha sabuni hizo licha ya kupigwa marufuku zimekuwa zikiuzwa kwenye maduka ya vipodozi.

Alisema mara nyingi kwenye operesheni zinazofanyika zimekuwa zikiondolewa sokoni lakini hata hivyo zimekuwa zikiingizwa kwa wingi hali inayofanya zoezi la kudhibiti kuwa gumu.

Alisema ni muhimu kwa wanawake kuacha matumizi ya sabuni hizo ambazo zina madhara makubwa sana kwao kwani zikikosa wanunuzi zitaondoka sokoni.
Source: Habari Leo

No comments:

Post a Comment