Pages

Tuesday, May 7, 2013

"UONGOZI NI UNOKO" ASEMA DKT. HOSEA

Dkt. Edward Hosea
Na Juma Nyumayo, Songea

MKURUGENZI Mkuu wa TAKUKURU, Dkt. Edward Hosea, amesema kanuni za utawala bora zikifuatwa na wananchi wote wakazitekeleza kutapunguza rushwa na kuleta maendeleo ya haraka.

Dkt. Hosea ameyasema hayo leo Manispaa ya Songea akitoa mada kwa viongozi wa Dini za kiislamu na kikristu  zaidi ya 50 toka mikoa ya Iringa, Njombe na wenyeji Ruvuma katika Ukumbi wa Hoteli ya Herritage Cottage, Manispaa ya Songea leo.

Amesema, kuna mambo kadhaa yanayosababisha kuchochea rushwa ikiwa ni pamoja na mikataba ya kazi kama ile ya Kudumu na Pensheni ambayo humfanya mwajiriwa kutoleta tija akiamini afanye asifanye yeye ni mwajiriwa wa kudumu na atalipwa pensheni akistaafu.

"hivi mtu ameajiriwa kwa Mktaba wa kudumu na pensheni ataleta tija huyu?, aliwauliza viongozi wa Dini na kuwatolea mfano wa wale wanaoajiriwa kwa mikataba ya muda mfupimfupi na kwamba mtu anaweza kuajiriwa tena kama ataleta tija na kuzingatia utawala bora kwa kuwahudumia wananchi.

Dkt. Hosea, amekerwa sana na tabia ya wafanyakazi kutosimamiwa vizuri na viongozi wao kwa kuogopa kuitwa "wanoko" na kuacha mambo yaende hovyo hovyo.

"Angalia pale Dar es Salaam, kuna baadhi ya watumishi wanakwenda kazini muda wowote hakuna anayejali na usitegemee tija pale," akaongeza kuwa hata viongozi wao wanaowasimamia hawawakalipii kwa kuogopa kuitwa wanoko.

Alisema hata Misikiti na Makanisa kama hayatasimamiwa, na viongozi wa Dini ambao wapo makini hayatasimama na hivyo nadiriki kusema Uongozi ni "unoko" wanaoukataa wafanyakazi wazembe.

Akaendelea kusema ili kudhibiti rushwa kuna vigezo vya uwajibikaji, uwazi, ubashiri wa sharia, sera uwezo wa mtu binafsi na taasisi ni muhimu.
Dkt. Hosea amesisitiza umuhimu wa ushirikishwaji wa watu kuwa ni msingi muhimu katika kupinga rushwa na kuleta maendeleo, amani na utulivu katika nchi.

Awali viongozi hao wa Dini walimbana maswali Dkt. Hosea kama kweli Taasisi yake inawatumishi wasafi, jambo alilokiri kuwa baadhi yao siyo wasafi kama binadamu wengine na kwamba tayari amekwisha wafukuza kazi watumishi 12 katika kipindi cha miaka hii miwili waliotuhumiwa kwa makosa mbalimbali.

Mkurugenzi Mkuu huyo, amewathibitishia viongozi hao kuwa hivi sasa anajenga uwezo wa watumishi na taasisi yake kwa kuwapeleka watumishi katika masomo ya muda mrefu na mfupi pia kuwaboresha kimaslahi.

"jamani mkiwaona watumishi wetu wanavaa vizuri wanaendesha magari si kwa bahati mbaya na si wala rushwa tunawakopesha kuwapunguza tamaa," alithibitisha Dkt Hosea.
Mwisho

No comments:

Post a Comment