Pages

Tuesday, May 7, 2013

ALIYERUSHA BOMU KANISANI HUYU HAPA.

  

DEREVA wa pikipiki maarufu kama bodaboda, Victor Ambrose, anatuhumiwa kurusha bomu katika Kanisa Katoliki la Mtakatifu Joseph Mfanyakazi, Parokia ya Olasiti jijini Arusha, lililosababisha vifo vya watu wawili na wengine karibu 70 kujeruhiwa.

Ambrose mwenye umri wa miaka 20 na mkazi wa Kwa Mrombo, Arusha, anashikiliwa pamoja na watuhumiwa wengine tisa, wakiwemo raia wanne wa Saudi Arabia kwa mahojiano zaidi ya kuhusika na tukio hilo.

Taarifa zilizopatikana jana jioni, zilieleza kuwa raia hao wa Saudi Arabia,
waliingia nchini Jumamosi usiku kwa ndege kupitia Uwanja wa Kimataifa wa Kilimanjaro (KIA), na baada ya tukio Jumapili, waliondoka nchini kupitia mpaka wa Tanzania na Kenya, Namanga.

Serikali kupitia kwa Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Dk Emmanuel Nchimbi, ilitoa taarifa hiyo jana bungeni na kueleza namna uhalifu huo ulivyotendeka kanisani hapo juzi, muda mfupi baada ya ibada kuanza.

Kwa mujibu wa Waziri Nchimbi, uchunguzi wa awali unaonesha kuwa mlipuko huo ni bomu. Hata hivyo uchunguzi wa kubaini aina ya bomu lililotumika, unaendelea kufanywa na Polisi na wataalamu wa Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ).

“Hadi sasa watuhumiwa sita wanashikiliwa na Jeshi la Polisi. Miongoni mwao ni Victor Ambrose mwenye umri wa miaka 20 dereva wa bodaboda...ambaye anatuhumiwa kurusha bomu hilo. “Watuhumiwa wengine watano waliokamatwa ni raia wa kigeni na Mtanzania mmoja ambao wanashikiliwa kwa mahojiano,” alisema Dk Nchimbi.

Waziri alitaja waliokufa katika tukio hilo kuwa ni mtoto mwenye umri wa miaka 16, James Gabriel, aliyefariki usiku wa jana na Regina Kurusei (45), mkazi wa Olasiti aliyefariki siku ya tukio wakati akipatiwa matibabu katika Hospitali ya Mount Meru.

Hata hivyo, Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Magesa Mulongo, alisema waliokamatwa wamefikia 10, na raia hao wa nje ni wa Saudi Arabia.

Alisema pia mtu wa tatu alifariki lakini hakumtaja jina. Kaimu Mganga Mkuu wa Hospitali ya Mount Meru, Dk Mariam Murktadha, alifafanua kuwa kijana Gabriel, alifia Uwanja wa Ndege wa Arusha, akiwa njiani kupelekwa Hospitali ya Taifa ya Muhimbili kwa matibabu zaidi.

Aliongeza kuwa majeruhi walikuwa 66 na hivi sasa wamebaki 34 na wengine wameruhusiwa.

Kwa mujibu wa Dk Nchimbi, majeruhi walikimbizwa Hospitali ya Mount Meru, wengine Hospitali ya St Elizabeth kwa Father Babu, Hospitali ya Selian na mwingine alipelekwa katika Hospitali ya Dk Wanjara, Mianzini.

Bomu lilivyorushwa
Akielezea tukio hilo, Waziri Nchimbi alisema lilirushwa wakati mgeni rasmi, Balozi wa Vatican nchini na Mjumbe wa Baba Mtakatifu, Askofu Fransisco Padilla, akiwa ametoka nje ya kanisa akijiandaa kukata utepe kama ishara ya uzinduzi.

Alisema mtu huyo alirusha kitu chenye ukubwa wa ngumi, kwenda eneo kulipokuwa na mkusanyiko wa watu na baada ya kutua, kulitokea kishindo na mlipuko mkubwa. Inakadiriwa uzinduzi huo wa Kanisa, ulihudhuriwa na watu zaidi ya 2,000.

Alisema viongozi wa dini na Serikali waliohudhuria ibada hiyo, hawakupata madhara yoyote kutokana mlipuko huo. Udini Amewasihi Watanzania kuwa watulivu wakati vyombo vya dola vikiwasaka walihusika na shambulio hilo.

Aidha ametaka kila mwenye taarifa za kuwezesha kukamatwa wahalifu hao azitoe Polisi. Kwa mujibu wa Waziri Nchimbi, siku za hivi karibuni kumekuwepo jitihada kubwa za watu wachache wasioitakia mema nchi, kutaka kupandikiza chuki za kidini miongoni mwa Watanzania na kuleta mapigano na mauaji.

“Sina shaka kuwa shambulio la Arusha ni sehemu ya mikakati hiyo miovu,” alisema bungeni na kusisitiza kwamba Serikali itachukua hatua kali kwa mtu yeyote bila kujali hadhi na nafasi yake katika jamii.

Wanasiasa waonywa
Wakati huo huo, Waziri Nchimbi amekemea wanasiasa wanaotafuta umaarufu wa kisiasa kupitia tukio hilo, akisisitiza kwamba Serikali isilaumiwe kwa hatua kali za kisheria itakazochukua dhidi ya viongozi wa aina hiyo.

“Kokote duniani tukio la kushitukiza linalosikitisha na kuhuzunisha kama hili linapotokea, wananchi wote huungana na kuwa wamoja kama taifa na kulaani wahusika na kuwafariji waathirika wa tukio hilo,” alisema Dk Nchimbi.

Akikemea wanasiasa wanaotumia matukio kujinufaisha, huku akitoa mfano wa Marekani na kusema mgombea mmoja wa urais wakati wa uchaguzi mkuu wa mwaka 2012, aliishutumu Serikali kutokana na kulipuliwa kwa ubalozi wa Marekani nchini Libya.

“Ni wazi kuwa mgombea huyo alichukua tatizo lile kama ajenda ya kisiasa. Hata hivyo alishutumiwa vikali na Wamarekani wenzake kwa kuelezwa kuwa ni mtu mwenye kukosa kabisa misingi ya uaminifu na uzalendo kwa taifa lake.”

“Serikali inasikitishwa sana na wanasiasa wa aina hii, ambao wanajitokeza nchini na kutafuta umaarufu wa kisiasa kwa gharama za maisha ya Watanzania…Serikali isilaumiwe kwa hatua kali za kisheria itakazochukua dhidi ya viongozi wa aina hii, ambao maslahi yao ni muhimu kuliko maisha ya Watanzania,” alisema.

Dk Nchimbi alilaani waliohusika kufanya uhalifu huo na kusema Serikali kwa nguvu zote itahakikisha watuhumiwa wote waliohusika na kushiriki kwa namna yoyote katika tukio hilo, wanasakwa popote walipo na kufikishwa katika vyombo vya sheria.

“Tunawataka viongozi wa kisiasa, kidini na wananchi wote kwa ujumla kila mmoja kwa nafasi yake kuwajibika, ili kuhakikisha kuwa nchi yetu inaendelea kuwa kisiwa cha amani na utulivu,” alisema.

Imeandikwa na Stella Nyemenohi, Dodoma na Veronica Mheta, Arusha.

Source: Habari leo

No comments:

Post a Comment