Pages

Tuesday, May 7, 2013

ASASI ZA KIRAIA ZAPINGA KUFUTWA MATOKEO YA MTIHANI KIDATO CHA NNE 2012 SOMA TAARIFA

 TAARIFA YA ASASI ZA KIRAIA KWA UMMA KUHUSU KUFUTWA KWA MATOKEO YA KIDATO CHA NNE 2012: 07 Mei 2013

Tarehe 03 Mei 2013, serikali ilitangaza Bungeni kuwa imeyafuta matokeo ya Kidato cha Nne ya mwaka 2012 ili yafanyiwe maboresho (standardization) na baadaye kupangwa upya kwa kutumia utaratibu uliotumika mwaka 2011. Akiwasilisha tamko la serikali bungeni, Mh. William Lukuvi, ambaye ni Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Uratibu na Bunge), alisema kuwa uamuzi wa serikali unalenga kutenda haki kwa walimu na wanafunzi ambao juhudi zao za kufundisha na kujifunza zimepimwa kwa kutumia mfumo mpya ambao hawakupata fursa ya kushirikishwa na kuandaliwa. Hivyo, Baraza la Mitihani Tanzania (NECTA) limeagizwa kuandaa na kutoa matokeo mapya kwa kuzingatia maelekezo hayo ya serikali.

Baada ya kutafakari uamuzi huu wa serikali, Asasi za Kiraia zinatoa tamko lifuatalo:

1. Asasi za Kiraia hazikubaliani na uamuzi wa kufuta matokeo ya kidato cha nne ya mwaka 2012. Kwa kuwa uamuzi huu wa serikali, umetokana na mapendekezo ya Tume ya Waziri Mkuu iliyoundwa kuchunguza matokeo ya kidato cha nne ya 2012, Asasi zinaomba ripoti hiyo itakapokuwa tayari iwekwe wazi mapema na wadau wa elimu wapate fursa ya kuona sababu zote zilizochangia kushuka kwa ufaulu katika mitihani hiyo. Ripoti hiyo, itatoa mwanga zaidi kuhusu mchango na uzito wa kila sababu katika matokeo hayo. Kwa kufuta matokeo hayo, serikali inawaaminisha watanzania kwamba sababu nyingine, hata kama zipo ziliathiri kwa kiwango kidogo matokeo hayo-na suala la upangaji wa madaraja kuonekana ni sababu kubwa zaidi kuliko nyingine.

Asasi za Kiraia na watanzania kwa ujumla wanatambua kwamba matokeo ya kidato cha nne yamekuwa mabaya kwa miaka kadhaa iliyopita. Kwa mfano; mwaka 2009, asilimia 27.5 ya watahiniwa walipata daraja sifuri; na mwaka 2010, sifuri walifikia asilimia 49.6; na 2011 ni asilimia 46.4. Na kwa miaka hiyo ya 2009 mpaka 2011, asilimia 86.9 ya watahiniwa walipata daraja la nne na sifuri; ambayo ni matokeo mabaya pia. Kwa mtiririko huu wa matokeo, ni bayana kuwa zipo sababu nyingine zenye uzito mkubwa zaidi zilizochangia kushuka kwa ufaulu kwa miaka kadhaa iliyopita zisizohusiana na upangaji wa matokeo kwa utaratibu tofauti. Hivyo basi, hakuna uhusiano wa moja kwa moja kati ya kubadili utaratibu wa kupanga matokeo na ufaulu duni wa 2012.

Kama ambavyo Asasi na watafiti wengine walivyokwisha kubaini miaka kadhaa iliyopita, mazingira ya utolewaji wa elimu nchini ni mabaya. Hakuna walimu wa kutosha-hasa kwa masomo ya sayansi, shule zina upungufu mkubwa wa vitabu na vifaa mbalimbali vya kujifunzia na kufundishia, bajeti ya maendeleo shuleni ni ndogo, ruzuku shuleni inafika ikiwa pungufu na tena ikiwa imechelewa, mihutasari ya kufundishia ina mkanganyiko mkubwa na huku mtaala mpya wa 2005 ukiwa mgeni kwa walimu walio wengi, msingi mbovu wa lugha ya Kiingereza ambayo ndiyo lugha ya mawasiliano darasani. Aidha, walimu hawana hamasa ya kufundisha kutokana na madai ya muda mrefu na kufanya kazi katika mazingira magumu.

Pia kukosekana kwa mafunzo kazini ya kuwaimarisha walimu katika ufundishaji wao hamasa ndogo miongoni mwa wazazi na walezi kufuatilia elimu ya watoto wao na ukaguzi shuleni kufanyika kwa kusuasua na shule nyingi hukaa bila kukaguliwa kwa muda mrefu ni baadhi ya sababu zilizochangia matokeo haya mabaya achilia suala la upangaji wa madaraja.Hizo ndizo sababu kubwa zilizosababisha matokeo kuporomoka kwa kasi kuanzia mwaka 2009. Hivyo, hakukuwa na haja ya kuunda Tume kwani sababu hizi zinajulikana.

Asasi zinaitaka serikali kuwaeleza watanzania kuwa huo mfumo mpya uliotumika ukoje, na hoja zilizozingatiwa wakati wa kuleta mfumo huo mpya ni zipi? Isitoshe, nani aliyepitisha mfumo huo mpya utumike kuwapima watahiniwa? Mfumo huo mpya una mapungufu gani? Na kwa upande mwingine, je mfumo huo una faida gani? Haya ni maswali ya msingi yanayohitaji majibu. Kuhamisha lawama kwa Baraza la Mitihani bila kueleza mchakato wa kupitisha matumizi ya mfumo mpya ni kuukwepa ukweli.

2. Ikumbukwe kwamba, baadhi ya wanafunzi walijiua baada ya kupata matokeo mabaya. Hivyo basi, matokeo yatakapopangwa upya, huenda baadhi yao wakatoka kwenye daraja sifuri. Nani ashitakiwe kwa kusababisha vifo hivi? Asasi zinatambua kwamba, pamoja na waliopoteza maisha yao kutokana na kushtushwa na matokeo hayo; wapo ambao mpaka sasa hawakubaliani na matokeo hayo.

Serikali ilipaswa kutafakari kwa kina kabla ya matokeo kutangazwa kwa mara ya kwanza; ili kwamba yatakapotangazwayabaki kuwa ndiyo matokeo halisi, kama ilivyokuwa miaka mingine iliyopita. Uamuzi wa kurekebisha na kupanga upya matokeo, unajenga taswira hasi juu ya mfumo wa elimu ya Tanzania kimataifa na mitihani yake kwa ujumla. Miaka ijayo, wanafunzi wa Tanzania wanaotaka kujiendeleza katika shule au vyuo vya nje wanaweza kutiliwa shaka uwezo wao kutokana na kuwepo kwa mfumo wa elimu usioaminika nchini na hata nje ya nchi.

3. Kuna baadhi ya wanafunzi na wazazi wameshafanya maamuzi mbalimbali mpaka sasa. Wapo ambao wamekata tamaa na wamepata madhara makubwa kisaikolojia. Wengine wamekubali kurudia mitihani-na wazazi wao wamekwishalipia ada za masomo na za kurudia mitihani kama watahiniwa binafsi. Je, serikali itatoa fidia gani kwa wanafunzi na wazazi kutokana na uamuzi huu?

4. Ikumbukwe kwamba, mwezi wa tatu mwaka huu, NECTAilikanusha kutumika kwa utaratibu mpya wa upangaji wa madaraja na matokeo. Je, NECTA ilisema uongo? Au je, ni kweli kuwa Tume ya Waziri Mkuu ya kuchunguza matokeo ina ushahidi usiotia shaka kwamba utaratibu mpya ulitumika na ndio chanzo cha wanafunzi kufeli hivyo? Uamuzi wa serikali umehamishia lawama zote kwa Baraza la Mitihani.

Hata hivyo, si Baraza peke yake linalohusika na kushuka kwa ufaulu katika matokeo ya mitihani ya kidato cha nne mwaka 2012 na miaka mingine kabla ya hapo. Kwa kuzingatia ukubwa wa tatizo, Asasi zinapendekeza kuwajibishwa kwa viongozi wakuu wa Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi na taasisi zake, kuanzia na Waziri mhusika Mh. Dk. Shukuru Kawambwa kwa kuisababishia hasara serikali na kwa kutangaza matokeo “yasiyo sahihi”, kuharibu taswira ya elimu nchini na kukosa ushawishi na mikakati ya kuboresha elimu nchini.

5. Kwa kuwa serikali imeagiza kwamba matokeo yarekebishwe na hatimaye kupangwa upya kwa kutumia utaratibu wa 2011, Asasi zinashauri zoezi hili lifanyike kwa uwazi kwa kushirikisha wadau wengine wa elimu ili kujiridhisha na uhalali wa alama za wanafunzi zitakazokuwa zinarekebishwa (kufanyiwa standardisation) na siyo uchakachuaji, katika njia za urekebishaji na upangaji wa matokeo katika madaraja. Wadau hawa ndio watakaoongeza uwezekano wa zoezi hili kuaminika kuliko likifanywa na Baraza na vyombo vya serikali peke yake.

6. Utafiti wa HakiElimu wa mwaka 2012 uitwao, Je wanafunzi wanafeli mitihani, au mitihani inawafelisha?, uliokuwa umejikita kwenye matokeo mabaya ya kidato cha nne mwaka 2011, ulieleza bayana kwamba Baraza la Mitihani limeweka usiri mkubwa hasa kwenye matumizi ya alama za maendeleo ya mwanafunzi toka shuleni (continuous assessment), kiasi ambacho sio rahisi kwa wadau na watafiti kujiridhisha.

Huenda usiri huu wa Baraza umechangia kutufikisha hapa. Mbaya zaidi, mitihani haiendani na kile kinachofundishwa shuleni. Hivyo basi, Baraza liwatumie walimu wanaofundisha katika mazingira tofauti nchini kutunga maswali yanayotumika kwenye mitihani ya Taifa. Mpaka sasa kwa mfano, walimu wengi nchini hawajui tofauti ya mtaala mpya wa 2005 uliojikita kwenye umahiri (competence) na ule wa zamani wa maarifa (content). Wanafundisha kama zamani kwa kuwa wizara ya elimu haijafanya jitihada za makusudi kuwajengea uwezo. Hivyo, kutunga mitihani kwa maelekezo ya mtaala mpya siyo sahihi-mpaka pale ambapo walimu watakuwa wanauelewa mtaala huo.

Ni muhimu kwa maamuzi mbalimbali ya Baraza kuwekwa wazi mapema ili wananchi na wadau wa elimu nchini wayafahamu na kuyafanyia kazi. Suala la kuwa na madaraja mapya kwa mfano linapaswa kushirikisha wadau wote, na taarifa zisambazwe nchini kote na kwenye shule zote mwaka mmoja kabla madaraja hayajaanza kutumika.

7. Kwa mara nyingine, Asasi za Kiraia zinaitaka Serikali kuweka mikakati thabiti ya kuboresha ufundishaji shuleni na kupunguza changamoto za elimu nchini kwa kuanza na zile zinazoathiri ufundishaji. Matokeo mabaya ni ishara kwamba kuna tatizo kubwa zaidi linalosababisha matokeo kuwa hivyo. Siyo rahisi na haitawezekana kushughulikia dosari za elimu nchini kwa kurekebisha matokeo peke yake. Matokeo ya darasa la saba mwaka jana yalipokuwa mabaya, serikali ilishusha alama za ufaulu mpaka kufikia alama 70 kati ya 250. Uamuzi huo, ulisababisha na utaendelea kusababisha kuandikishwa wanafunzi shule za sekondari wasiokuwa na sifa.

Baadhi yao wameenda sekondari pasipo kujua kusoma na kuandika. Aidha, idadi ya watanzania wasiojua kusoma wala kuandika inazidi kuongezeka kila siku. Hii ina maana kuwa kuna tatizo pana zaidi katika mfumo wetu wa elimu, na wala si usahihishaji tu au upangaji wa madaraja. Hivyo, ni dhahiri kuwa wanafunzi wanapofeli kwa wingi, serikali haipaswi kustuka; kwani imeweka pembeni viwango vya ubora kwa makusudi; kisha ikaondoa mchujo wa kidato cha pili.

Wanafunzi waliofanya mtihani wa kidato cha nne mwaka 2012 hawakuchujwa walipokuwa kidato cha pili. Hata wale wa miaka ya 2009 mpaka 2011 nao hawakuchujwa. Ni kipi kinachoifanya serikali kutarajia matokeo bora kuliko haya yaliyopatikana? Kushusha alama na viwango vya ufaulu katika ngazi zote kunaondoa ushindani na kudunisha ubora wa wahitimu.

Ni muhimu sasa serikali izingatie kutumia mfumo bora zaidi wa kutahini na kupima uwezo wa wanafunzi katika ngazi zote za elimu. Mfumo huo ukidhi vigezo vyote vya kitaalam vinavyotumika ndani na nje ya nchi. Aidha, serikali iazimie kwa dhati kuwekeza katika elimu ya watanzania ili kuhuisha jitihada za kuiletea maendeleo nchi yetu na kutowapotezea muda vijana kwa kuwaweka shuleni pasipo kuelimika. Pia Serikali inapaswa itafute sababu zinazochangia watoto kufaulu mitihani ya kumaliza elimu ya msingi pasipo kujua kusoma wala kuandika.

Tamko hili limetolewa na Policy Forum, HakiElimu, Sikika, TEN/MET na TGNP.
 


Source: http://www.wavuti.com

No comments:

Post a Comment