Pages

Tuesday, April 16, 2013

PROF. MBELE WA hapakwetu.blogspot.com HAPENDI UMBUMBUMBU, ASISITIZA WATU WASOME KWA MAENDELEO

Na Juma Nyumayo, Songea

Nimekuwa Msomaji mzuri wa Blogu ya Prof. Joseph Mbele.
Makala nyingi anazoandika, picha anazopost na mazungumzo yake anasisitiza sana watu kuelimika. watu wajifunze mila na desturi mbalimbali kwa maendeleo yao.

Prof. Mbele husafiri na wanafunzi wake (Wamarekani) kuja nao nchini na kutembelea maeneo mbalimbali. Wanajifunza kwa vitendo. Mimi licha yakuwa Mwandishi wa habari kitaaluma, ni mwalimu pia.

Tumesisitizwa na wataalamu wa elimu (Walimu wetu) na tunaendelea kusisitiza ili kujifunza vyema na kujenga kumbukumbu ya kudumu, elimu kwa vitendo itumike zaidi kuliko nadharia. Vitendo vinahusisha milango mingi zaidi ya fahamu.

Prof. Mbele katika Blogu yake ya hapakwetu.blogspot.com  anafundisha mengi, nimeona jinsi anavyotembelea maonesho hakosi kupiga picha mabanda yanayoonesha vitabu. Katika Blogu yake anaonyesha machapisho mbalimbali na vitabu vipya.
Kulikoni Prof. Mbele kupendelea zaidi vitabu, kunani kwenye vitabu. Tabia iliyoibuka ya baadhi ya watanzania kujiingiza kwenye mijadala mizito wakati wao ni 'weupe'. Weupe kwakuwa hawana hazina kichwani iliyotokana na kusoma vitabu vya mijadala husika. Inapotosha watu na nchi kwa ujumla.
Hapa nitaweka baadhi ya kazi zake chache. Hajaniruhusu lakini natanguliza kuomba radhi.

Hii ni kwa manufaa ya wasomaji wetu waweze kutembelea Blogu ya hapakwetu.blogspot.com kuchota maarifa.

Angalia kazi hizo, na uingie mwenyewe mtandaoni uone Falsafa yake. Kweli Prof. Mbele ni Mwalimu wa watu, kwaajili ya maendeleo ya watu na ulimwengu kwa ujumla.





Sunday, January 29, 2012


Mwandishi Shafi Adam Shafi

Tanzania tuna waandishi wengi maarufu katika lugha ya ki-Swahili. Mmoja wao ni Shafi Adam Shafi, kutoka Zanzibar, ambaye anaonekana nami pichani hapa kushoto. Tulikuwa New Africa Hotel, Dar es Salaam mwaka 2004 wakati wa tamasha la vitabu.






Shafi Adam Shafi anafahamika sana kwa riwaya zake. Riwaya aliyoichapisha kwanza ni Kasri Ya Mwinyi Fuad (Tanzania Publishing House, 1978). Ilikuwa maarufu tangu mwanzo. Sikupata muda wa kuisoma. Halafu, mwaka 1980 niliondoka Tanzania, kuwenda masomoni Marekani, hadi mwaka 1986.

Baada ya kukaa Marekani miaka sita hiyo, nilivyorejea Tanzania nilifanya juhudi ya kujipatia vitabu vya ki-Swahili. Nilinunua nakala ya Kasri Ya Mwinyi Fuad tarehe 28 Oktoba, 1987, ikasainiwa na Shafi Adam Shafi tarehe 29. Nina risiti ya kununulia kitabu, kutoka Tanzania Publishing House. Kwa hivyo, nina ushahidi kuwa nimeonana na Shafi Adam Shafi mara mbili.

Ingawa mara kwa mara ninapoongelea vitabu katika blogu zangu huwa naandika kuhusu yaliyomo, na uchambuzi wangu, leo nimependa tu kuchangia kumtangaza Shafi Adam Shafi na kazi zake. Nitakapokuwa nimezisoma kazi zake, Insh'Allah, nitaweza kuandika kwa undani zaidi.

Shafi Adam Shafi ameandika pia Kuli (Dar es Salaam: Tanzania Publishing House, 1979) , Vuta N'kuvute (Dar es Salaam: Mkuki na Nyota Publishers, 1999), na Haini (Nairobi: Longhorn Publishers, 2003).

Kuna taarifa ya mahojiano ya kina baina ya Shafi Adam Shafi na Freddy Macha ambayo unaweza kuyasoma hapa.
 

 

2 comments:

  1. Asante sana kwa kuweka taarifa zangu hapa kwenye blogu yetu pendwa. Mimi ni msomaji makini wa blogu hii.

    Nashukuru kwa uamuzi wako, kwani unanisaidia mimi ambaye ni mwalimu, kusambaza kwa walimwengu yale ninayoandika. Ndio wajibu wa ualimu, na narudia tena shukrani zangu kwako.

    ReplyDelete
    Replies
    1. Asante saana Prof.Mbele. Tupo pamoja. Maaandishi yako na Maelekezo unayoyatoa ni hazina kubwa. Tutaendelea kufuatilia katika Blogu ya hapakwetu.blogspot.com kuchota hazina hiyo kwa maendeleo yetu. Asante kwa yote.

      Delete