Pages

Tuesday, April 16, 2013

LEO NI SIKU YA KUPAZA SAUTI, JE WABUNGE WANAWEWESEKA AU WANATUKANA KWELI?


Mwenyekiti wa MOAT, Dkt. Reignald Mengi.

 
 
Na Juma Nyumayo, Songea

WAKATI naelekea kazini leo Asubuhi, nikasikia ni Siku ya Kupaza Sauti.
Nikajiuliza ni namna gani sauti zipazwe. Swali hili lina msingi mkubwa. Kwa maana mara nyingi watu wamepaza sauti zao zisikike. Lakini zisikike na nani? Akisikia iweje? na je anayepaza sauti naye anasikia? Anasikia kama ni kelele au muziki au ujumbe? Nimejiuliza sana maswali mengine mengi bila kupata majibu.

Jana Dkt. Regnald Mengi, alisema Waandishi wa habari wawasaidie kupaza sauti wasio na sauti. Nikajiuliza tena hivi ni kweli waandishi wenyewe wanayo sauti kupaza? Au wamepewa tu ili wapaze kwa wengine?

Naam, kama wenye mali namaanisha MOAT, wanaomiliki vyombo vya habari hapa nchini, wanaowaajiri waandishi na kuwalipa hicho kinachowafanya wapaze sauti hata wakoromee Dola,  wanaamini waandishi si wanyonge, wanasauti kubwa na husikika kwa watoa maamuzi kama ujumbe na si kelele au muziki wa kuwabembeleza.

Waandishi tunajukumu zito la kulifanya. Jukumu la kulitekeleza katika nchi ambayo tayari kulikuwa na jaribio la kutaka Bunge letu katika vikao vyake  lisiende "Live" ili wafanye madudu, watukanane na watutukane walipa kodi nao waendelee kuitwa waheshimiwa.  
Jana hiyo hiyo,Naibu Spika wa Bunge letu pale Mjengoni, Mhe. Job Ndugai, amewaonya wabunge tabia ya kutumia lugha mbaya, matusi na kuacha kilichowapeleka Bungeni.
Hili nalo ni jukumu la waandishi kupaza sauti isikike. Wakati mwingine ni kosa la waandishi kuwapigia debe, kuwapazia sauti watu wasiostahili kuchaguliwa kuwa Wabunge, Madiwani, wenyeviti wa Serikali za Mitaa na vyeo vingine kibao.
Methali za Kiswahili zinafundisha, "Kichwa cha kuku hakistahili kilemba," lakini Kichwa hicho kikipaziwa sauti kitavalishwa kilemba na Kuku huyo atapata taabu kuchakura chakura. Msishangae kuwaona baadhi ya wabunge watu leo, hawawezi kuchakura matatizo ya wananchi, badala yake vilemba tulivyowavesha vinawasumbua sana hadi wanaweweseka kwa kutukana ovyo ovyo pale mjengoni.
Jiulize Mbunge anayetukana ovyo mjengoni, mahala penye utaratibu na Kanuni, akiwa nje na wapiga kura wake hufanya nini? Je huwa na ubavu wa uvumilivu kusikiliza shida zao na changamoto kibao zinazowakabili kimaendeleo.
Tuache kupaza sauti bila utafiti, uchunguzi wa kitaaluma.
Kijiko kibaki kuwa kijiko, na sepetu (chepe) ibaki kuitwa chepe na wala si kijiko kikubwa. Huo ndio uandishi wa habari unaozingatia Ukweli  (Truth and Fairness) kwaajili ya maendeleo ya watu wote.
Tuwaambie wabunge, wananchi hawafurahii hata kidogo wanachokifanya Bungeni hasa Lugha wanayotumia ya Matusi. Matusi hayana tija kwa kulijenga taifa. Huko ni kuishiwa sera na mipango binafsi katika kuwatumikia watu.
Mwisho

No comments:

Post a Comment