Pages

Monday, December 16, 2013

WAPINGA MAENDELEO YA ELIMU MBINGA KUKIONA


Mkuu wa wilaya ya Mbinga mkoani Ruvuma, Senyi Ngaga akitoa msisitizo wake mbele ya Wadau wa elimu wa wilaya hiyo(Hawapo pichani) katika ukumbi wa Umati uliopo mjini hapa, juu ya Katibu wa CWT wilaya humo kuwa ni kikwazo cha maendeleo ya elimu. 


Na Kassian Nyandindi,
Mbinga.

MKUU wa wilaya ya Mbinga mkoani Ruvuma, Senyi Ngaga amemshukia Katibu wa Chama cha Walimu Tanzania (CWT) tawi la Mbinga Samwel Mhaiki, akidai kwamba ni kikwazo cha maendeleo ya elimu wilayani humo, kutokana na katibu huyo kupenda kuendesha migogoro na kuchonganisha walimu mashuleni.

Ngaga alisema hayo alipokuwa akizungumza na Wadau wa elimu, Kata ya Mbinga mjini juu ya kukuza maendeleo ya sekta ya elimu wilayani humo, katika hafla fupi iliyofanyika ukumbi wa Umati uliopo mjini hapa.

Alisema kuwa katibu huyo amekuwa kinara namba moja wa kupita mashuleni na kushinikiza walimu waache kufundisha (Wagome) hadi watakapolipwa madai yao, jambo ambalo alilieleza kuwa limekuwa likileta mgogoro usio na tija katika jamii.

Alieleza kwamba licha ya Mhaiki kuitwa mara nyingi ofisini kwake na kumtaka aache kuendeleza migogoro hiyo, anashangaa kumuona bado akiifanya.


“Tumemuonya mara nyingi huyo Mhaiki, lakini amekuwa bado akitusumbua kwa kuandika mabarua na kusambaza mashuleni akishinikiza walimu wagome waache kufundisha….tulimwambia serikali inashughulikia madai ya hawa walimu na watalipwa malumbano haya anayoyaendeleza sasa ningelikuwa na uwezo mimi kama Mkuu wa wilaya hii ningemhamisha, kwa sababu ni kikwazo kwa maendeleo ya elimu hapa wilayani, leo walimu wakigoma watoto wetu watafundishwa na nani”, alisema Ngaga.

Mkuu huyo wa wilaya awali alisema wilaya hiyo hivi sasa imejipanga katika kukuza kiwango cha elimu kwa shule za msingi na sekondari, ambapo kwa kushirikiana na ofisa elimu wa wilaya hiyo Mathias Mkali wamekuwa wakiendelea na mfumo wa watoto kujisomea wakati wa likizo (Makambi) kwa kila kata wilayani humo, hususani kwa watoto wa darasa la sita ambao wanaingia darasa la saba mwakani.

Alisema wazazi wameitikia wito kwa kiasi kikubwa juu ya suala hilo na kukubaliana kutoa michango ya chakula, katika vituo hivyo ambavyo watoto wao wanasoma wakati huu wa likizo.

Alisisitiza kuwa mtu yeyote atakayeonekana anakwamisha mikakati waliyojiwekea ya kukuza kiwango cha elimu wilayani Mbinga, yupo tayari kumwajibisha ili iwe fundisho kwa wengine wenye tabia kama hiyo

No comments:

Post a Comment