Pages

Friday, June 21, 2013

UNGA WAWAPELEKA JELA MIAKA 15 UGHAIBUNI


Mabondia waliohukumiwa

Mabondia wanne wa Tanzania wafungwa miaka 15 jela nchini Mauritius kwa makosa ya kuingiza dawa za kulevya aina ya heroin.

Mabondia hao ni Case Ramadhani Fills, Nathanael Elia Charles, Ally Rajabu Msengwa na Petro Charles Mtagwa.
 
Wakati kesi hiyo ilipoanza kusikilizwa, wote walikiri makosa ya kuingiza mihadarati hiyo nchini Mauritius wakati walipokwenda kushiriki mashindano ya ndondi barani Afrika mwaka 2008.
 
Wakiwa mbele ya Jaji, waliiambia mahakama kuwa walilazimika kuingia katika biashara hiyo haramu kutokana na hali zao za maisha kuwa maskini.
 
"Tunaomba radhi kwa taifa la Mauritius", waliiambia mahakama.
"Tu watu maskini na tunategemewa na familia, watoto na wazee wetu wanaotugemea."
 
"Kwa dawa hizi tungepata kiasi cha Pauni £4,000". walisema

Jaji Benjamin Marie Joseph alisema katika kutoa adhabu hiyo yote hayo ameyafikiria, kwani walitoa ushirikiano mzuri wakati wote wa uchunguzi wa kesi hiyo, kulikowezesha hata wafanyabiashara hiyo, raia wa Mauritius kukamatwa.
 
Wamekuwa mahabusu kwa siku 1,722, sawa na miaka mitano, hivyo watatumikia miaka kumi iliyobakia jela. Pia watatakiwa kulipa faini ya pauni £1,600 na gharama nyingine za uendeshaji wa kesi hiyo.
 
Kwa mujibu wa mwandishi wa habari wa BBC nchini Mauritius Yasine Mohabuth in Mauritius, Jaji aliwashutumu kwa kuukosea umma wa Mauritius kwa kuingiza dawa hizo za kulevya aina ya heroin.
 
Mabondia hao waliwasili Mauritius tarehe 10 Juni 2008 na kuweza kupita uwanja wa ndege bila kunaswa hadi walipokamatwa katika hoteli waliyofikia ya Quatre Bornes.
 
Kwa pamoja walimeza gram 4639.04 za heroin zikiwa katika vifuko 358 vijulikavyo kama pipi.
 
Chanzo: BBC-Swahili

No comments:

Post a Comment