Pages

Friday, April 12, 2013

Auawa na Tembo akikagua shamba lake


Na Steven Augustino, Tunduru
MKAZI wa Kijiji cha Daraja mbili katika kata ya Namwinyu Tarafa ya Matemanga Wilaya ya Tunduru Mkoani Ruvuma ameuawa na tembo.
Mkazi huyo  aliyefahamika kwa jina la Chalamanda  Masapi (65) amefariki dunia baada ya kuvamiwa ghafla na kushambuliwa na Tembo ambaye alikuwa na mtoto  wakati akikagua uhalibifu wa mazao uliofanywa na kundi la wanayama hao katika shamba lake lililopo nje kidogo ya kijiji hicho.
Mtoto wa Marehemu Chalamanda, Rashidi Chalamanda ambaye alikuwa ni miongoni mwa Shuhuda wa tukio hilo,  alisema kuwa yeye na marehemu babayake wakishirikiana na kundi la wananchi wanaolima katika eneo hilo walikwenda katika mashamba yao kushiriki katika zoezi la kuwafukuza tembo hao ambao pia walivamia Kijijini hapo na kufanya uharibifu mkubwa wa mazao yao.
Alisema katika tukio hilo la kushitukiza marehemu  alijikuta akiwa mikononi mwa mnyama huyo ambaye hakuwa hana hata chembe moja ya huruma ambaye baada ya kumkamata kwa kutumia mkonga wake  alimrusha juu na kumpiga katika mti uliokuwa karibu na eneo hilo kabla ya kumkanyaga na kumsaga na baadae kumpiga kwa kutumia Pembe zake na kumtoboa toboa vibaya mbavuni na tumboni.
Katibu uchumi wa CCM Wilaya ya Tunduru, Bw.Yasini Masapi, akizungumzia hali na mwonekano wa mwili wa marehemu Chalamanda  alisema kuwa ama kweli mnyama huyo alimpania kumtoa uhai kwani pamoja na kumtoboa kwa kutumia pembe hizo pia Tembo huyo alimparua na kumkanyaga kanyaga na kuuvuruga kabisa mwili kiasi cha kutomtambka kabisa .
Afisa Wanyama pori wa Wilaya hiyo Bw. Peter Mtani, amekiri  kuwepo kwa tukio hilo. Amesema kuwa tayari idara yake imepeleka askari wenye silaha ili waende kuandaa mtego ambao utafanikisha kuuawa kwa Tembo huyo.
Bw. Mtani, aliendelea kueleza kuwa  matukio ya Tembo hao kuvamia na kifanya uharibifu katika mashamba ya wakulima wa Wilaya hiyo yamekuwa yakijitokeza mara kwa mara na kwamba kutokana na hali hiyo idara yake imekuwa ikifanya kazi ya ziada kuwafukuza wanyama hao  ili wasiendelee kuharibu mazao ya watu.
Alisema pindi inapo bainika kuwa Tembo hao wanazidi kufanya mashambulizi ya kuzulu mwili ama kufanya mauaji kama ilivyo tokea idara hiyo pia imekuwa ikichukua hatua za kuwasakaa na kuwaua tembo hao haraka iwezekanavyo  ili wasiendelee kusababisha madhara kwa watu wengine.
Akizungumzia hali na muonekano wa mwili wa marehemu huyo Mganga  katika hospitali hiyo Dk. Gearge Chiwangu, alisema kuwa Marehemu alifariki dunia kutokana na kutokwa na damu nyingi zilizo sababishwa na kutobolewa matundu manne ubavuni na tumboni mwake.
Dk. Chiwangu aliendelea kueleza kuwa  sambamba na hali hiyo pia mwili wa marehemu ulikutwa ukiwa umevurugika vibaya huku shingo yake ikiwa imevunjika na kichwa kupasuka hali ambayo onesha kuwa hata kama asingefariki katika eneo la tukio uwezekano wa kumsaidia kuokoa maisha yake usinge kuwepo.
Kamanda wa polisi wa Mkoa wa Ruvuma Bw. Deusidedit Nsimeki, amethibitisha kuwepo kwa tukio hilo na kueleza kuwa jeshi hilo bado linaendelea na uchunguzi wa kina ili kujiridhisha chanzo cha kifo hicho.
Mwisho
 
 


No comments:

Post a Comment