Pages

Saturday, April 3, 2010

KAMATI ZA KUFUATILIA MATUMIZI YA FEDHA ZA UMMA ZAUNDWA





KAMATI tano za Kufuatilia matumizi ya fedha za umma (PETS) zimeundwa mkoani Ruvuma, baada ya washiriki 55 toka wilaya zote tano kuhitimu mafunzo ya kujenga uwezo kwa jamii ya kufuatilia matumizi hayo.

Mafunzo hayo ya siku tano yaliyoendeshwa na Baraza la Hiari la vyama vya Maendeleo ya jamii TACOSODE katika Manispaa ya Songea kwa lengo la kuendesha zoezi hilo ili kuimarisha uwajibikaji, huduma zinazotolewa na nguzo ya utawala bora wa rasilimali za umma.

Kamati hizo zinatarajiwa kufanya kazi katika halmashauri za wilaya ya Songea, Mbinga, Tunduru, Namtumbo na Manispaa ya Songea na zitakua na jukumu la kufuatilia matumizi ya fedha za umma katika sekta ya afya kufuatia mipango na bajeti iliyokamilika mwaka uliopita.

Akizipatia maelekezo kamati hizo kuwa zikashirikiane vyema na serikali za halmashauri hizo ili kuleta ufanisi unaokusudiwa, Katibu Mtendaji wa TACOSODE, Theofrida Kapinga, (anaye sisitiza jambo pichani) alisema kamati hizo zizingatie maadili na miongozo ya kufanya ufuatiliaji na si kuchochea migogoro katika jamii.

“Ninyi sio Polisi wala wakaguzi wa hesabu, mkashirikiane kama tulivyowafundisha,” alisema Kapinga.

Wajumbe wa kamati hizo walifundishwa mbinu mbalimbali za kufuatilia matumizi ya fedha za umma ikiwa ni pamoja na kushawishi na kuitetea jamii kutekeleza wajibu na kufuatilia haki zao.
Eneo jingine ni kuhamasisha wananchi katika kushiriki shughuli za maendeleo na kuwa walinzi wa rasilimali zinazotumika kuboresha miundombinu mbalimbali ya kutolea huduma katika sekta mbalimbali.

Akitoa mada ya wajibu wa asasi za kiraia na wajibu wake, Mwezeshaji toka TACOSODE Abdalah Shamte alisema asasi zinawajibu mkubwa wa kufuatilia fedha za miradi ya Serikali kwa kufanyia utafiti na kutoa ripoti kwa Halmashauri husika pamoja na kutoa mchanganuo wake wa mapato na matumizi ya fedha hizo za maendeleo ikiwa moja ya njia ya kuwabana viongozi wa Serikali.

Alisema mafunzo hayo yatasaidia kuwajengea uwezo jamii kupitia Asasi zao kujua wajibu wao wa ufuatiliaji wa fedha za umma kwa kuanzia hatua ya kwanza mpaka ya mwisho kwa kufanyakazi ya kuhoji pale wanapoona shaka kabla ya kuchukuliwa hatua za kisheria.

Naye Makamu Mwenyekiti Mtandao wa Azaki Mkoani Ruvuma (Runeciso) Adam Nindi alisemamafunzo hayo yatakuwa ya msaada mkubwa sit u kwa wananchi bali kwa serikali za mitaa na serikali kuu katika kuboresha swala la utawala bora.
“Kwa kweli Serikali kupitia Mashirika yake ya Kiraia imekuwa na mipango mizuri ya kufanyakazi ya kumwelewesha mwananchi wa ngazi ya chini na ufuatiliaji wa fedha za miradi zinazoingia katika Halmashauri utawafanya wananchi wawajibike zaidi,Alisema.

Mafunzo hayo yanaendeshwa na TACOSODE kwa ufadhiri wa Foundation for Civil Society la jijini Dar es Salaam ambao wamekuwa wakitoa mbinu ya ufuatiliaji wa fedha za Serikali.

MWISHO.

No comments:

Post a Comment