Pages

Sunday, April 11, 2010

Dkt.Emmanuel Nchimbi awakabidhi Sekondari wananchi!





























(Maelezo ya Picha Dkt. Nchimbi akimkabidhi Ufungua DC wa Songea Thomas Ole Sabaya Picha ya Pili DC Thomas Ole Sabaya akifurahia kukabidhiwa Tuzo ya Uongozi Bora Dunia ( Global Leadership Award) kwa niaba ya wananchi wa Songea, Tuzo hiyo alitunukiwa Dkt. Emmanuel Nchimbi Mbunge na Naibu Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa na kuitoa kwa wananchi wa Songea kwa heshima na upendo wao kumwezesha kufanya kazi iliyoonerkana na kuthibitika kimataifa kuwa yeye ni kiongozi Bora Duniani, Picha ya Tatu wananchi wakiwa katika foleni kungoja wali mweupe na pilau kujichana kufurahia kukabidhiwa shule ya Mkuzo. Mjumbe wa UWT pia Naibu Meya Elizabeth Ngongi, akimkabidhi fedha taslimu zaidi ya Shilingi 200,000 Dkt Nchimbi ya kuchukulia fomu ya kugombea Ubunge Muda ukifika, UWT wilaya ya Songea Mjini imeridhishwa sana na kazi zake Mbunge huyo Msomi Kijana. Picha Mashabiki wa Dkt Nchimbi wakifurahia jambo walipokutana na Msaidizi wake Naibu Waziri, Meja na Aliyesimama amevalia mavazi ya Kijani Sio Mwingine, Ni Mwenyekiti wa CCM wilaya ya Songea Mjini Hemed Dizumba akimwaga salamu za CCM kwa utekelezaji wa Ilani ya CCM uliofanya na Dkt Emmanuel Nchimbi Mbunge wao Picha zote na Juma Nyumayo wa Ruvuma Press)

WANANCHI wa Manispaa ya Songea wamekabidhiwa majengo ya shule ya sekondari ya Kidato cha tano hadi sita yenye thamani ya zaidi ya shilingi milioni 112 toka kwa Mbunge wa jimbo hilo jana.
Mbunge huyo, Dkt Emmanuel Nchimbi, ambaye pia ni Naibu Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa katika hotuba yake kabla ya kukabidhi shule hiyo alisema ametekeleza ahadi yake kwa wananchi wa Songea ambao kwa muda mrefu walikuwa nyuma katika maswala ya elimu hasa ya sekondari.
" takwimu zinaonyesha wanafunzi darasa la saba waliofaulu ni 1373 lakini waliopata nafasi ya kujiunga na sekondari walikuwa 480 tu," aliwakumbusha wananchi waliohudhuria hafla hiyo huko Mkuzo nje kidogo ya Manispaa ya Songea.
Alijivunia harakati za kujenga shule za sekondari katika kata zte 13 za Manispaa ya Songea na kuruhusu asilimia 100 ya wanafunzi wote 3074 waliofaulu mwaka jana kujiunga na masomo ya sekondari .
" Sekondari kidato cha 1-4 tunazo za kutosha sasa, shule hii itasaidia wanafunzi kidato cha tano na sita," alisema Dk Nchimbi na Kufafanua kuwa itakuwa na uwezo wa kuchukua wanafunzi wasichana na wavulana 400 kwa wakati mmoja na ikikamilika itaweza kuwachukua wanafunzi 800.
Hata hivyo Dk Nchimbi alizitaja changamoto kubwa ambazo amevalia njuga kuzishughulikia ni pamoja na upungufu wa walimu, vifaa na kuboresha majengo na miundombinu ya shule.
"Changamoto nyingine ni kuwalipa haki zao walimu na kujenga chuo kikuu," alisema Nchimbi ambaye alishangiliwa na wananchi wa Manispaa kwa salamu zao jukwaani na sanaa za maonesho.
Nao Mwenyekiti wa CCM wilaya ya Songea Mjini, Hemedi Dizumba, Meya wa Manispaa ya Songea Gerald Ndimbo na DC wao Thomas Ole Sabaya, wamesema katika hotuba zao kuwa kitendo alichokifanya Mbunge huyo ni cha kijasiri kinachomthibitishia ni msomi aliyetekeleza agizo la Baba wa taifa Marehemu Julius Nyerere kuwa waliopata elimu wawasaidie wenzao.
Mwisho

Saturday, April 3, 2010

Manispaa ya Songea yaanzisha ubinafsishaji shughuli za Afya!


Manispaa ya Songea bila hiyana wala haya imewaalika wadau wake wapatao 300 kuzungumzia kubinafsisha shughuli za kuuweka mji safi. hivi karibuni Mwandishi wa habari Mwandamizi Adam Mzuza Nindi, Katika Safu ya Nionavyo aliandika Makala ya kudorora na kuporomoka kiusafi na kupoteza kabisa maana ya kuitwa Manispaa. Wadau walialikwa wakakutana kwenye Ukumbi wa Songea Club wakiongozwa na Mkuu wa Wilaya Thomas ole Sabaya, watu maarufu, watendaji, wafanyabiashara, wakuu wa taasisi zote na Mashirika ya dini yote walielekezwa nini cha kufanya na kusikiliza mada na matokeo ya tafiti za kutoka kule Manispaa ya Morogoro. Pichani Afisa Mipango Miji na Mratibu wa Mpango wa Uendelezaji wa Miji na Usimamizi wa Mazingira(UDEM) Edward Alfred Kandonga, akitoa mada mbele ya washiriki hao 300.

KAMATI ZA KUFUATILIA MATUMIZI YA FEDHA ZA UMMA ZAUNDWA





KAMATI tano za Kufuatilia matumizi ya fedha za umma (PETS) zimeundwa mkoani Ruvuma, baada ya washiriki 55 toka wilaya zote tano kuhitimu mafunzo ya kujenga uwezo kwa jamii ya kufuatilia matumizi hayo.

Mafunzo hayo ya siku tano yaliyoendeshwa na Baraza la Hiari la vyama vya Maendeleo ya jamii TACOSODE katika Manispaa ya Songea kwa lengo la kuendesha zoezi hilo ili kuimarisha uwajibikaji, huduma zinazotolewa na nguzo ya utawala bora wa rasilimali za umma.

Kamati hizo zinatarajiwa kufanya kazi katika halmashauri za wilaya ya Songea, Mbinga, Tunduru, Namtumbo na Manispaa ya Songea na zitakua na jukumu la kufuatilia matumizi ya fedha za umma katika sekta ya afya kufuatia mipango na bajeti iliyokamilika mwaka uliopita.

Akizipatia maelekezo kamati hizo kuwa zikashirikiane vyema na serikali za halmashauri hizo ili kuleta ufanisi unaokusudiwa, Katibu Mtendaji wa TACOSODE, Theofrida Kapinga, (anaye sisitiza jambo pichani) alisema kamati hizo zizingatie maadili na miongozo ya kufanya ufuatiliaji na si kuchochea migogoro katika jamii.

“Ninyi sio Polisi wala wakaguzi wa hesabu, mkashirikiane kama tulivyowafundisha,” alisema Kapinga.

Wajumbe wa kamati hizo walifundishwa mbinu mbalimbali za kufuatilia matumizi ya fedha za umma ikiwa ni pamoja na kushawishi na kuitetea jamii kutekeleza wajibu na kufuatilia haki zao.
Eneo jingine ni kuhamasisha wananchi katika kushiriki shughuli za maendeleo na kuwa walinzi wa rasilimali zinazotumika kuboresha miundombinu mbalimbali ya kutolea huduma katika sekta mbalimbali.

Akitoa mada ya wajibu wa asasi za kiraia na wajibu wake, Mwezeshaji toka TACOSODE Abdalah Shamte alisema asasi zinawajibu mkubwa wa kufuatilia fedha za miradi ya Serikali kwa kufanyia utafiti na kutoa ripoti kwa Halmashauri husika pamoja na kutoa mchanganuo wake wa mapato na matumizi ya fedha hizo za maendeleo ikiwa moja ya njia ya kuwabana viongozi wa Serikali.

Alisema mafunzo hayo yatasaidia kuwajengea uwezo jamii kupitia Asasi zao kujua wajibu wao wa ufuatiliaji wa fedha za umma kwa kuanzia hatua ya kwanza mpaka ya mwisho kwa kufanyakazi ya kuhoji pale wanapoona shaka kabla ya kuchukuliwa hatua za kisheria.

Naye Makamu Mwenyekiti Mtandao wa Azaki Mkoani Ruvuma (Runeciso) Adam Nindi alisemamafunzo hayo yatakuwa ya msaada mkubwa sit u kwa wananchi bali kwa serikali za mitaa na serikali kuu katika kuboresha swala la utawala bora.
“Kwa kweli Serikali kupitia Mashirika yake ya Kiraia imekuwa na mipango mizuri ya kufanyakazi ya kumwelewesha mwananchi wa ngazi ya chini na ufuatiliaji wa fedha za miradi zinazoingia katika Halmashauri utawafanya wananchi wawajibike zaidi,Alisema.

Mafunzo hayo yanaendeshwa na TACOSODE kwa ufadhiri wa Foundation for Civil Society la jijini Dar es Salaam ambao wamekuwa wakitoa mbinu ya ufuatiliaji wa fedha za Serikali.

MWISHO.