Monday, August 27, 2012

CHADEMA kumfikisha Nape wa CCM Mahakamani?????





Kufuatia agizo la CHADEMA Nape wa CCM (Pichani) kuomba radhi.




* Agoma kuomba radhi, asema tuhuma atazithibitisha mahakamani



* Amtaka Dk. Slaa kuandaa bilioni 3 na shilingi moja



* Ni kwa kudai CCM inaingiza silaha nchini.












KATIBU wa Halmashauri Kuu ya Taifa Itikadi na Uenezi CCM, Nape Nnauye amewataka Chadema kwenda mahakamani haraka badala ya kusubiri kuombwa radhi kama walivyotaka ili kusafishwa dhidi ya madai ya chama chao kupewa mabilioni ya fedha na mataifa tajiri.


Aidha amemtaka Katibu Mkuu wa chama hicho Dk. Wilbrod Slaa kuiomba radhi CCM la sivyo itamburuza mahakamani kudai fidia ya sh. bilioni 3 na shilingi moja, kwa kuituhumu uongo kwamba imeingiza silaha kutoka nje ya nchi tena bila kulipia ushuru.


Nape alisema hayo leo Agosti 27, 2012, kweneye mkutano wake na waandishi wa habari, uliofanyika Ofisi Ndogo ya Makao Makuu ya CCM, mtaa wa Lumumba mjini Dar es Salaam.


"Bila shaka mmesikia jana Chadema wakinitaka niombe radhi au wananipeleka mahakamani kudai fidia ya sh. bilioni 3, kwa madai eti nimesema Chama hicho kinapata mabilioni ya fedha kutoka kwa mataifa tajiri. Mkubwa hatishiwi nyau, nawataka waende haraka mahakamani wala wasisubiri hizo siku saba", alisema Nape.


Alisema, CCM inao ushahidi wa kutosha kuhusu madai aliyotoa Nape dhidi ya Chadema na kwamba huyo tayari kutoa uthibitisho huo mahakamani badala ya kuomba radhi."Nadhani wakienda mahakani itapendeza zaidi maana huko ndiko pazuri kutoa uthibitisho kuhusu tuliyosema, na ninawahakikishieni tukishathibitisha na Msajili wa Vyama akaupata uthibitisho huo chama chao kinafutwa", alisema.


Kuhusu CCM kumburuza Dk. Slaa mahakamani, Nape alisema, ameshawaagiza wanasheria wa Chama, kuandaa barua ya kusudio la mashitaka hayo, na Dk. Slaa atapelekewa ili aamue kama ataomba radhi au atakuwa tayari kwenda mahakamani.


"Wakati wanakwenda mahakamani, Chadema wamwambie babu yao ajiandae kuomba radhi au kuburuzwa mahakamani kuilipa CCM fidia ya sh. bilioni 3 na shilingi moja kwa kuizushia CCM uongo kwamba inaingiza silaha nchini tena", alisema Nape.

Sensa, Sensa Makarani wakosa sare Ruvuma, zoezi laendelea














Picha 1: Baadhi ya Abiria wanaosafiri kwenda nje ya Songea wakipanda Gari la Kangaulaya kituo cha Mabasi Songea siku ya Sensa.

Picha 2: Kituo cha Afya Mjimwema Manispaa ya Songea, moja ya eneo litakalo nufaika na matokeo ya Sensa ya Watu na Makazi 2012 ili kiamuliwe kuwa Hospitali ya Manispaa na kupunguza mzigo kw Hospitali ya Mkoa Songea inayolemewa na wagonjwa hata wale wa nje (OPD)


Picha 3: Gari la Wagonjwa lililotolewa zawadi na Mbunge wa Jimbo la Songea Mjini Dkt. Emmanuel Nchimbi (Picha zote na Juma Nyumayo)







Baadhi ya Makarani wa Sensa Manispaa ya Songea mkaoni Ruvuma, wamekosa Sare za kuwatambulisha.




haya yamejiri mkoani hap na taarifa hii Imethibitishwa na Ofisa Habari w Mkoa wa Ruvuma, Bw. Kasimb alipohojiwa na Mwandishi wa Blog hii ya http://www.ruvumapress.blogspot.com/ mbaye alisema zoezi lenyewe limeanza kwa mafanikio makubwa,






Bw. Kasimba amesema Katibu Tawala wa mkoa wa Ruvuma, Bw Hassan Bendayeko aliweza kutembelea Halmashauri za wilaya ya Namtumbo, Songea Vijijini na Manispaa ya Songea kujiridhisha na uendeshaji wa Zoezi hilo muhimu kwa taifa katika eneo lake mkoani Ruvuma.






Naye Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma, Saidi Thabit Mwambungu, ameelezwa kuridhishwa na uhesabuji wa wtu katika Sensa ya watu n Makazi lililoanza 26/8/2012 na kuahidi kuifanyia kazi chagamoto ya Makarani kukosa sare, licha ya kuvaa kitambulisho.




Wakati huohuo, Baadhi ya wajumbe wa serikali za Mitaa mkoni hapa wamelalamikia posho ndogo wanayopata kwa kazi hiyo ya kuwaongoza makarani wa sensa katika maeneo yao.



Mwenyekiti wa Serikali ya mtaa wa Mshangano Manispaa ya Songea, Paul Mangwe amesema Wajumbe hao wamelipwa Shilingi elfu nne tu(4,000/=) kwa zoezi lote la sensa.



Amesema wajumbe hao wanaendelea kufanya kazi hiyo shingo upande.



Sensa ya Watu na Makazi ni zoezi maalum lenye lengo la kupata idadi ya watu wote nchini ambapo taarifa zao za Kijamii na Kiuchumi hukusanywa na kuisadia serikali kufahamu mahitaji ya wananchi wa kila rika, mahali walipo na wenye mahitaji maalum.

Sunday, August 26, 2012

Asante Mbunge Dkt. Nchimbi, Gari l wagonjwa Manispaa ya Songea








Gari la Wagonjwa lililotolewa zawadi na Mbunge wa Jimbo la Songea mjini, Dkt Emmanuel Nchimbi linavyoonekana kwenye picha, hapo likiwa limeegesha Kituo cha Afya Mjimwema likisubiri dharura za wagonjwa.

Mji wa Songea unakuwa kwa kasi kama unavyoona msongamano katika picha hiyo ya tatu, shughuli za uchumi, kijamii na siasa zimekuwa wakati za kiutamaduni zikidorora kwaajili ya watu kuiga mitindo, na utamaduni wa nje unaoenezwa kwa nguvu na vyombo vya habari na bidhaa za kutoka nje.

Ni nadra sasa katika mji huu kuziona ngoma, makundi ya vijana wenye adabu zao kama zamani ya miaka ya 1980/ 90.

Kutokana na ongezeko la watu, huduma za Gari la wagonjwa limepokelewa kwa mikono miwili.

(Picha zote na Juma Nyumayo)

















Saturday, August 25, 2012

HOTUBA YA RAIS JK, KUHAMASISHA SENSA



HOTUBA YA MHESHIMIWA DK JAKAYA MRISHO KIKWETE, RAIS WA JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA, KWA WANANCHI KUHAMASISHA SENSA YA WATU NA MAKAZI,
TAREHE 25 AGOSTI, 2012
Ndugu wananchi;
Imekuwa ni mazoea yetu kuwa Rais huzungumza na taifa kila mwisho wa mwezi. Lakini, leo nazungumza nanyi siku saba kabla ya mwisho wa mwezi kwa sababu maalum. Sababu yenyewe si nyingine bali ni Sensa ya Watu na Makazi itakayofanyika kwa siku saba kuanzia kesho Jumapili tarehe 26 Agosti, 2012. Shabaha yangu ni kutaka kuwakumbusha Watanzania wenzangu wote kuhusu wajibu wao wa kujitokeza kuhesabiwa siku hizo. Naomba kila mmoja wetu ahakikishe kuwa anakuwepo kuhesabiwa na kujibu maswali yote yatakayoulizwa na makarani wa sensa kwa ufasaha.
Ndugu wananchi;
Katika historia ya nchi yetu, Sensa ya mwaka huu itakuwa ni ya tano tangu Uhuru wa Tanganyika mwaka 1961, Mapinduzi ya Zanzibar ya tarehe 12 Januari, 1964 na kuzaliwa kwa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania tarehe 26 Aprili, 1964. Sensa nyingine zilifanyika mwaka 1967, 1978, 1988 na 2002. Kumbukumbu zinaonesha kuwa kwa upande wa Tanzania Bara wakati wa ukoloni zilifanyika Sensa mwaka 1910, 1931, 1948 na 1957. Kwa upande wa Zanzibar wakati wa ukoloni na utawala wa Sultan kulifanyika Sensa mara moja mwaka 1958.
Ndugu Wananchi;
Kama ilivyokuwa kwa Sensa zilizotangulia, madhumuni makubwa ya Sensa ya Watu na Makazi ya mwaka 2012 ni kujua idadi ya watu, mahali walipo, jinsia zao, umri wao, elimu, shughuli wazifanyazo, vipato vyao, upatikanaji wa huduma mbalimbali pamoja na makazi. Taarifa hizi hutumiwa na Serikali kupanga mipango ya maendeleo, kutengeneza programu mbalimbali na kubuni miradi ya maendeleo ya kiuchumi na kijamii nchini. Aidha, huisaidia Serikali kupanga na kupeleka huduma za kiuchumi na kijamii kwa wananchi kwa kuzingatia mahitaji halisi ya maeneo yao wanayoishi kwa mujibu wa idadi yao na mgawanyiko wao kijinsia, kiumri na huduma zinazohitajika. Hivyo basi, idadi halisi isipojulikana kuna hatari ya wananchi kukosa huduma wanazohitaji kwa kiwango kinachostahili. Vilevile, takwimu hizi hutumiwa na Serikali katika kufikia uamuzi wa kugawa majimbo ya uchaguzi na maeneo ya utawala kama vile mikoa, wilaya, kata, vijiji na vitongoji vipya.
Ndugu wananchi;
Pamoja na umuhimu huo wa jumla wa Sensa kwa maendeleo ya nchi yetu, Sensa ya mwaka 2012 ina umuhimu wa aina yake. Taarifa zake zitatumika kufuatilia na kutathmini utekelezaji wa Dira za Taifa za Maendeleo za Tanzania Bara na Zanzibar; Mkakati wa Kukuza na Kupunguza Umaskini Tanzania Bara (MKUKUTA II); Mkakati wa Kupunguza Umaskini Zanzibar (MKUZA II); na Mpango wa Maendeleo wa Miaka Mitano wa 2011/12 – 2015/16. Vilevile taarifa zitakazopatikana zitatumika kupima maendeleo ya utekelezaji wa Malengo ya Milenia (Millenium Development Goals) yaliyowekwa na Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa mwaka 2000. Kama tujuavyo, itakapofika mwaka 2015 ndicho kilele cha utekelezaji wa Malengo hayo hivyo kujua hatua tuliyofikia sasa itasaidia kujipanga vizuri katika miaka mitatu iliyosalia.
Ndugu Wananchi;
Pamoja na faida hizo, taarifa za Sensa hii zitasaidia kufanikisha zoezi linaloendelea sasa, la kuwapatia Watanzania vitambulisho vya taifa. Baadhi ya maswali yatakayoulizwa kwenye Sensa ya Watu na Makazi yatasaidia katika kuhakiki maombi ya vitambulisho vya taifa. Bila ya shaka sote tunatambua vyema manufaa ya vitambulisho vya taifa, hivyo basi ndugu yangu, shiriki zoezi la sensa ili kuirahisishia Serikali kazi ya utoaji wa vitambulisho kwa raia wake.
Ndugu wananchi;
Shughuli yoyote kukabiliwa na changamoto mbalimbali ni jambo la kawaida. Lakini, tofauti na miaka ya nyuma, Sensa ya mwaka huu imekabiliwa na changamoto ambazo hazijawahi kuwepo. Kuna baadhi ya wenzetu wamekuwa wanafanya jitihada za makusudi za kutaka kulivuruga zoezi la Sensa nchini. Wamekuwa wanawashawishi watu wasishiriki kuhesabiwa, kwa sababu ambazo baadhi yake hazina uhusiano wo wote na Sensa. Zipo sababu nyingine ambazo hata haziingii akilini. Kwa mfano, wapo watu wanaodai kuwa hawatashiriki Sensa mpaka mjusi aliyeko kwenye Jumba la Makumbusho kule Berlin, Ujerumani atakaporudishwa. Kinachozungumzwa hapa ni mabaki ya mifupa ya mnyama wa kale aliyekuwepo hapa nchini zaidi ya miaka milioni 200 iliyopita. Mwaka 1906 wana sayansi wa Kijerumani waliyagundua mabaki hayo kule Tendaguru, Lindi, wakayafukua na kuyapeleka Ujerumani ambako yamehifadhiwa tangu wakati huo.
Ndugu Wananchi;
Kudai mifupa hiyo irejeshwe nchini si jambo baya, watu wataona wanyama wa kale waliokuwepo wakati huo wanafananaje. Huenda pia kikawa kivutio cha utalii. Hata hivyo, kugeuza kurejeshwa kwa mabaki hayo kuwa sharti la kushiriki Sensa ni jambo ambalo mantiki yake siielewi. Watu wakisusia Sensa kwa sababu hiyo itakuwa siyo tu haieleweki wala haielezeki, bali hata watu wengine nchini na duniani watawashangaa. Lakini, jambo ambalo ningependa wajiulize ni kuwa hivi hasa wanamsusia nani? Mjerumani au wanajisusia wenyewe? Hivi kweli mtu uko tayari kuacha manufaa yako ya maendeleo yapotee au yaathirike kwa sababu ya mjusi ambaye hata akirejeshwa huna manufaa ya moja kwa moja? Hasara anapata nani sisi au wao? Nawasihi, Watanzania wenzangu, tusiwasikilize watu wanaoeneza maneno yahusuyo Mjusi au mambo mengine ya upotoshaji na uvurugaji wa mambo yenye maslahi makubwa zaidi kwetu binafsi na nchi yetu. Tuachane nao hawatutakii mema na wala hawaitakii mema nchi yetu. Nawaomba tusitumie vibaya uhuru wa kutoa maoni.
Ndugu Wananchi;
Wapo ndugu zetu wengine wanaotaka liongezwe swali la dini ya mtu katika orodha ya maswali yatakayoulizwa katika Sensa ya mwaka huu. Wahusika wakuu hasa ni baadhi ya viongozi na wanaharakati wa Kiislamu. Wao wanasema bila ya swali hilo kuwepo, Waislamu wasikubali kuhesabiwa. Wamekuwa wanafanya juhudi kubwa ya kuwashawishi Waislamu wawaunge mkono katika msimamo wao huo. Nimesoma baadhi ya nyaraka na vipeperushi vyao kuhusu madai hayo. Nilipata pia bahati ya kukutana na kuzungumza na baadhi ya wanaharakati na viongozi wa harakati hizo. Nia yangu katika kufanya hayo ilikuwa ni kutaka kuelewa kwa undani hoja na madai yao. Yako mambo kadhaa yanayotajwa kama sababu, lakini ukweli ni kwamba jambo linaloweza kuhusishwa moja kwa moja na Sensa, ni lile la takwimu za idadi ya Waislamu, Wakristo na Wapagani zilizotolewa na Baraza la Maaskofu Katoliki, Shirika la Utalii na Shirika la Utangazaji Tanzania.
Hawazikubali taarifa hizo kwa hoja kwamba, Waislamu hawajawahi kuhesabiwa na watoaji wa takwimu hizo. Kwa sababu hiyo hawaelewi ni kwa vipi watoe idadi ya kuwa ni asilimia fulani Watanzania. Hawana ugomvi nao kuhusu takwimu za Wakristo na Wapagani kwani huenda waliwahesabu. Kwa maoni yao, taarifa hizo si za kweli na ni upotoshaji unaofanywa maksudi kwa sababu wanazozijua watoaji wa taarifa hizo. Ili kuondoa upotoshaji huo, wanaharakati na viongozi hao wa Waislamu wakataka swali la dini liwepo katika Sensa hii ili ukweli ujulikane.
Katika mazungumzo yangu na baadhi ya viongozi wa Waislamu niliwaambia kuwa naelewa sababu na hoja za wao kukasirishwa na kutokuzikubali takwimu hizo. Vile vile, niliwaeleza kuwa takwimu hizo si za Serikali bali ni za mashirika hayo. Nilisisitiza kuwa takwimu za Serikali kuhusu idadi ya watu hutolewa na Ofisi Kuu ya Takwimu na si chombo kingine chochote cha Serikali. Bahati nzuri Ofisi Kuu ya Takwimu haijatoa takwimu hizo na wala siyo chanzo cha takwimu zilizotolewa na mashirika hayo. Walikozipata wanajua wenyewe. Taarifa hizo hazina ithibati yo yote na ndiyo maana zinatofautiana. Niliwasihi waachane nazo, wazipuuze na wakipenda watoe tamko la kuzikataa.
Ndugu Wananchi;
Niliwaambia pia kuwa kuelekeza lawama kwa Serikali kwa ajili ya taarifa hizo ni kuionea na kutoitendea haki. Vile vile kuibebesha dhima ya kuongeza swali la dini ili kuyajibu mashirika hayo ni kuipa mzigo usiostahili. Napenda, kutumia nafasi hii kuwasihi wale wote wanaotoa takwimu za namna hiyo kutambua unyeti wake na kuepuka kufanya hivyo. Zinatuletea mifarakano isiyokuwa ya lazima kama ilivyo sasa.
Ndugu Wananchi;
Kwa upande wetu, yaani Serikali, imekuwa vigumu kukubali maombi ya kuliingiza swali la dini katika Sensa hii kwa sababu za kisera na kiutekelezaji. Wakati wa ukoloni maswali ya rangi, dini na kabila la mtu yaliulizwa katika Sensa. Baada ya uhuru, maswali hayo yaliulizwa katika Sensa ya kwanza ya mwaka 1967 kwa vile ilikuwa bado inafuata misingi ya kikoloni. Baada ya hapo ulifanyika uamuzi wa kisera wa kutokuuliza maswali hayo kwani nia ya wakoloni kuuliza maswali yale ilikuwa ni kwa sababu ya sera yao ya wagawe uwatawale. Walitoa huduma kwa ubaguzi, sera ambayo Serikali zetu ziliachana nayo baada ya Uhuru na Mapinduzi. Huduma hazikuwa zinatolewa kwa ubaguzi wa rangi, kabila wala dini, bali kwa msingi wa haki ya uraia na ubinadamu wake.
Ndugu Wananchi;
Sera hiyo pia ilikuwa na lengo la kudumisha umoja na mshikamano wa taifa letu na watu wake. Badala ya watu kubishana juu ya watu wa dini ipi ni wengi na hivyo kufarakana kwa kutokubaliana na takwimu zilizotolewa, sera mpya inawataka watu wajivunie uwingi wao kama Watanzania.
Ndugu Wananchi;
Nionavyo mimi Sera hii ni nzuri na kwamba ulikuwa ni uamuzi wa busara na hekima kubwa. Tuendelee kuidumisha na kuienzi. Kufanya vinginevyo, na hasa kuingiza sera ya kutoa huduma kwa misingi ya dini zetu ni kuliingiza taifa letu ambalo lina sifa ya amani, upendo na utulivu, katika migogoro isiyokuwa ya lazima. Ni migogoro inayoweza kuepukika kwa kuenzi na kudumisha sera yetu hii nzuri na sahihi.
Ndugu Wananchi;
Sababu ya pili inayotupa ugumu kiserikali ni ya kiutekelezaji. Imechukua miaka kadhaa ya maandalizi mpaka kufikia hatua hii ya sasa ya kuwa tayari kutekeleza zoezi la Sensa ya Watu na Makazi ya mwaka 2012. Isitoshe Sensa ya majaribio imeshafanyika kwa kutumia vifaa, madodoso na maswali yaliyopo na marekebisho kufanywa baada ya hapo. Kuingiza mambo au jambo jipya sasa itakuwa viguku kiutekelezaji. Kutachelewesha zoezi zima na kusababisha hasara kubwa kwa taifa.
Kwa vile watu wote hawataulizwa swali la dini na kwa kuwa dini si kigezo cha kutoa huduma kwa wananchi, hakuna ulazima wa kusisitiza swali hilo liwepo. Napenda kuwasihi ndugu zangu wanaokereketwa na jambo hili waache kuling’ang’ania na badala yake wajitokeze kuhesabiwa. Tujitokeze kuhesabiwa ili na Waislamu nao wawemo katika idadi ya wananchi wa Tanzania.
Ndugu Wananchi;
Sioni ulazima wa kuunda Tume Huru ya Sensa yenye uwakilishi sawa wa Wakristo na Waislamu. Tangu mwaka 1931 kazi ya Sensa imekuwa inafanywa na Ofisi Kuu ya Takwimu nchini na ndipo ujuzi na maarifa yote yapo. Hata ukiamua uiite Tume bado utawatumia watu hao hao, hivyo mabadiliko hayo hayana sababu. Vile vile, sioni haja ya kuwa na mgao wa wafanyakazi wake kwa msingi wa dini kwa sababu Sensa siyo kwa ajili ya kujua Wakristo na Waislamu. Huduma hazitolewi kwa misingi ya dini za watu.
Ndugu Wananchi;
Katika maelezo yao kwangu, hivi karibuni Kamishna wa Sensa, Hajat Amina Mrisho Said na Mtakwimu Mkuu wa Serikali ya Muungano, Mama Albina Chuwa walinieleza kwamba kwa kawaida katikati ya Sensa moja na nyingine, hufanyika utafiti wa kidemografia, yaani Demographic Survey. Huu ni utafiti wa kina unaofanywa katika ngazi ya kaya ambapo taarifa za mambo mengi yahusuyo watu ambazo hazikusanywi, katika Sensa hukusanywa. Mara ya mwisho utafiti huo kufanyika ilikuwa mwaka 1973, yaani baada ya Sensa ya mwaka 1967 na kabla ya ile ya mwaka 1978. Ni makusudio ya Ofisi ya Taifa ya Takwimu kuanzisha tena utaratibu huo mwaka 2016 ambapo baadhi ya masuala yaliyoachwa yanaweza kujumuishwa. Subira yavuta heri.
Ndugu Wananchi;
Nimehakikishiwa na mamlaka zinazohusika kuwa maandalizi ya sensa yamefikia hatua nzuri na zoezi liko tayari kuanza siku ya Jumapili, tarehe 26 Agosti, 2012. Lakini, mafanikio ya zoezi lenyewe yatategemea sana ushiriki wa watu ambao ndiyo walengwa na wadau wengine. Naomba nitumie fursa hii kuwataka Wakuu wa Mikoa na Wilaya na Wenyeviti na Wakurugenzi Watendaji wa Halmashauri za Wilaya na Miji na wadau wengine wa kisiasa na kiutendaji wa ngazi mbalimbali waendelee kusimamia utekelezaji wa shughuli zote za Sensa katika maeneo yao ya uongozi. Hawana budi kuhakikisha kuwa zoezi linakuwa na mafanikio makubwa. Wale wote wanaofanya vitendo vya kuvuruga zoezi hili wachukuliwe hatua stahiki za kisheria.

Nawaomba viongozi wa kisiasa na kijamii nao waendelee kuwahamasisha na kuwaelimisha wananchi kuhusu umuhimu wa kujitokeza kuhesabiwa na kushirikiana na Makarani wa Sensa watakapokuwa wanafanya kazi yao. Wakumbusheni kukataa kuwasikiliza au kuwafuata watu wanaowashawishi wasijitokeze kuhesabiwa. Watu hao si wema wao na wala hawaitakii mema nchi yetu.
Ndugu wananchi;
Nitakuwa mwizi wa fadhila kama sitawapongeza Hajat Amina Mrisho Said, Kamishna wa Sensa wa Tanzania Bara na Ndugu Mwalim Ameir, Kamisaa wa Sensa Zanzibar kwa kazi kubwa na nzuri wanayoendelea kuifanya ya kutoa uongozi wa kisiasa, kusimamia na kuratibu zoezi la Sensa nchini. Nawapongeza pia Mkurugenzi Mkuu wa Ofisi ya Taifa ya Takwimu na Mtakwimu Mkuu wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar pamoja na watendaji wengine wa Sensa katika ngazi mbalimbali katika Mikoa, Wilaya, Majimbo, Tarafa, Kata, Mitaa, Vijiji na Shehia kwa kazi nzuri ya matayarisho na uendeshaji wa Sensa ya mwaka 2012. Nawatakia mafanikio mema katika kazi hii muhimu na adhimu kwa nchi yetu na watu wake.
Ndugu zangu, Watanzania wenzangu, nawaomba sote tuwaunge mkono ndugu zetu hawa kwa kushiriki katika zoezi la Sensa kuanzia siku ya Jumapili tarehe 26 Agosti, 2012. Haya shime sote tujitokeze kuhesabiwa kwani kujitokeza kwetu ndiyo ukamilifu na mafanikio ya Sensa ya Watu na Makazi ya mwaka 2012. Ewe Mtanzania mwenzangu shiriki Sensa kwa maendeleo yako na ya taifa letu.
Mungu Ibariki Tanzania!
Mungu Ibariki Afrika!
Asanteni kwa kunisikiliza

Tulipokwenda Kutalii Mikumi, Tukajionea wenyewe

Wajumbe wa Bodi ya Union of Tanzania Press Clubs UTPC, Tulibahatika kwenda Mikumi kuona wanyama na vivutio vingine, kwa lugha uliyozoeleka tulikwenda kutalii. Tuliingia pale na gali letu tukalipia pesa kidogo sana. Wanyama tuliowaona na maelekezo tuliyopewa kuhusu wanyama na tabia zao, ulaji, kuzaana, kutengana pia kujilinda kwao, ni maelekezo adimu kupatikanabila kutembelea maeneo hayo na kukutana na wataalamu wanaowafahamu wanyama hao kwa taaluma na kuishi nao miaka nenda rudi. Tulifaidika sana. Rais wa UTPC na baadhi ya wajumbe wa Bodi wametoa wito kwa waandishi na wananchi kutembelea hifadhi/mbuga na Bustani za wanyama hapa nchini kukuz uelewa na kufaidi Maliasili na rasilimali za Taifa.

Picha 1: Alama ya Taifa ni Twiga ambaye tulimkuta katulia akitushangaa wakati tunampiga picha,
Picha 2: Baadhi ya wajumbe mra baada ya kuteremk toka Hiace kwenda Ofisi ya mapokezi hapo Mikumi,
Picha ya Tatu ni mimi Juma Nyumayo kwenye kibao cha Mikumi National Park.




























Waislmu wakubali kuhesabiwa Ruvuma

Wakati Taifa liningia ktika zoezi muhimu la Sensa, Waislamu hapa mkoani Ruvuma wamelegeza msimamo wa kukataa kuhesabiwa hasa wale wa kata ya Ruvuma ambao walitangaza kutojihusisha na zoezi hili. juhudi za Mkuu wa mkoa wa Ruvuma said Thabit Mwambungu na baada ya Mufti wa Tanzania, Sheikh Issa Bin Shaaban Simba kutoa msimamo thabiti wa waislamu kuwa sensa ni muhimu kwao wakati wa Sherehe za Idd El Fitri kitaifa mkoani Ruvuma, aliwaomba waislamu waitendee haki serikali yao kwa KUHESABIWA. ZOEZI HILO LINAANZA USIKU HUU katika maeneo maalum kama Stendi, kwenye Guest House na maeneo yaliyoelekezwa. Tutaendelea kuwajulisha yatakayojitokeza



Wednesday, August 22, 2012

SIKU SABA GAZETI LA MWANAHALISI KUWA HURU?


WANAHARAKATI SALAAM!

Hatua zilizochukuliwa jana za kuitaka serikali ilifungulie Gazeti la Mwanahalisi na kuipatia siku saba kufanya hivyo, tunaziunga mkono kwa dhati.
Mwanahalisi lifunguliwe hata kabla ya hizo siku saba.
Waswahili husema Muungwana akivuliwa ngua, huchutama.

Serikali ilitakiwa ichutame, kwa kutolifungia Gazeti la Mwanahalisi lililosaidia walao serikali iwatambue watakaosaidia kuwakamata watuhumiwa.

Ndio uungwana. Serikali sikivu italitekeleza hili, haitataka kutunisha misuli kwa jambo kama hili. Viongozi watambue jukwaa pekee wakishatemwa madarakani ni kwenye vyombo vya habari. wasivibane, wanajibana wenyewe.


www.ruvumapress.blogspot.com
TANZANIA KWANZA

Adhabu ya kifo siyo adhabu, ni uhalifu mwingine, Soma hii

Naona kuna mkondo wa kuua.



Sasa tuachane na wanaharakati na watetezi wa haki za binadamu. Tujaribu kufikiri bila vivuli vyao.



Twende kwenye hoja ya kuua:ANAYEUA ANASTAHILI KUUAWA.



Hicho ndicho kilio cha wachangiaji wengi. Kapoku kamuua Sadoko.



Sasa wanataka Kapoku auawe. Wanataka mahakama iamue kuwa Kapoku auawe mpaka afe. Mahakama inaamua hivyo. Serikali inayosimamia utekelezaji inatoa panga, msumeno, kamba au umeme na kuua Kapoku.


Nani sasa ameua Kapoku? Kwa ufupi mchinjaji ni serikali/utawala.
Twende mbele. Hoja ya wachangiaji wengi ni kwamba ANAYEUA AUAWE. Hivyo serikali iuawe. Kuua ni kuua - awe ameua masikini au tajiri, mtu binafsi au serikali. Ni uharamia tu.
Tutafute adhabu kwa aliyeua.


KIFO SIYO ADHABU. Kifo ni kuondosha maisha ya yule ambaye angefanya adhabu.


Tena angefanya adhabu angejutia alichofanya, angejifunza na jamii ingejifunza.


Aliyekufa hajifunzi. Hajutii kosa lake.


Kama Kapoku ameondoa maisha ya Sadoko na serikali imeondoa maisha ya Kapoku; hakika wote ni WAUAJI. Si vema kuishi katika dunia ya wauaji.
ndi.



(Nimeichukua hii toka http://www.ndimara.blogspot.com/ nasikitika sikuomba idhini toka kwake nimekosa kwa hili Juma Nyumayo)

Tuesday, August 21, 2012

KUFUNGIWA KWA GAZETI LA MWANAHALISI


Watetezi wa haki za binadamu, asasi za kijamii na wadau wakuu wa habari nchini, leo wameipa serikali siku saba kufungulia gazeti la MwanaHALISI, vinginevyo wataitisha maandamano ya kupinga hatua ya serikali kufungia gazeti hilo kwa muda usiojulikana, kuminya uhuru wa habari, haki za binadamu na utesaji wa wanaharakati.
Asasi ambazo zimetoa tamko la kutaka serikali ifungulie MwanaHALISI ni MISA, Legal and Human Rights Centre, Tanzania Human Rights Defenders Coalition, Human Rights National Association of Educators For World Peace and Citizen Rights Watch.
Tamko la asasi hizo ni kama ifuatavyo hapa chini:
TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI 22 Agosti 2012
YAH: KUFUNGIWA KWA GAZETI LA MWANAHALISI

KWA mara nyingine tena, tumewaiteni hapa kuwaomba mtufikishie ujumbe wetu huu kwa watawala. Ujumbe wenyewe unahusu kufungiwa kwa gazeti la kila wiki la MwanaHALISI na kauli ya Waziri Mkuu Mizengo Kayanza Peter Pinda aliyoitoa bungeni, Alhamisi tarehe 16 Agosti 2012. Kama mnakumbuka vema, wakati akijibu swali bungeni siku hiyo, Waziri Mkuu Pinda alisema, “Serikali imechukua wajibu wake kulifungia gazeti hilo, na kwamba kama wahusika hawakuridhika na hatua iliyochukuliwa na serikali wana haki ya kukata rufaa kwa mamlaka za juu.”

Awali ya yote, tuseme wazi, kuwa hatukuridhika na majibu ya Waziri Mkuu kuhusu kufungiwa kwa MwanaHALISI. Majibu ya Waziri mkuu Pinda yamelenga kuahirisha tatizo, siyo kutatua. Kwanza, Waziri Mkuu anatetea uamuzi huo uliofanywa na sheria katili na kandamizi ya magazeti. Sheria inayonyang’anya uhuru wa kufikiri, uhuru wa kutoa maoni na uhuru wa kuwasiliana. Pili, Mheshimiwa Pinda anatumia sheria hiyo kutaka kuliangamiza gazeti hili ambalo limesifiwa kwenye ripoti mbalimbali za ndani na nje ya nchi ikiwamo ile iliyotolewa majuzi na Baraza la Habari Tanzania (MCT) inayochambua Mwenendo wa vyombo vya Habari nchini kwa mwaka 2011 inayosema katika ukurasa wa tisa:

“Pamoja na kusakamwa na serikali, MwanaHALISI limesimamia uandishi wake wa kuikosoa serikali.”

Serikali imelituhumu gazeti hili kwa kuchapisha habari ambazo inasema “zinakiuka” vifungu 32(1) (a), (c) – (d); 32(1)(c) na 36(1) vya Sheria ya Magazeti Na. 3 ya 1976. Habari hiyo inahusu kutekwa, kuteswa kinyama na hatimaye kutupwa katika msitu wa Mabwepande kwa kiongozi wa madaktari nchini, Dk. Steven Ulimboka. Hii ndiyo habari ambayo serikali inaita ya “uchochezi.” Yaani badala ya serikali inayojigamba ina mkono mrefu wa kumfikia yeyote kuutumia mkono huo kutafuta watuhumiwa waliotajwa na gazeti kuwa walifanikisha kutekwa kwa Dk. Ulimboka, imeamua kutumia mabavu kulifungia MwanaHALISI huku wakiacha maisha ya Dk. Ulimboka na wanaharakati wengine njia panda.

Serikali imechukua hatua hiyo, huku wakijua kuwa Ibara ya 18 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, 1977 kama ilivyorekebishwa na Sheria ya Mabadiliko ya 14 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania (2005), ilipanua haki ya kutoa, kutafuta, kupokea, na kusambaza habari. Mabadiliko hayo yaliondoa kivizo cha “kwa mujibu wa sheria” Kila mtu- anao uhuru wa kuwa na maoni na kueleza fikra zake; anayo haki ya kutafuta, kupokea na kutoa habari bila ya kujali mipaka ya nchi; anao uhuru wa kufanya mawasiliano na haki ya kutoingiliwa katika mawasiliano yake.

Aidha, mabadiliko hayo yanatoa haki kwa kila raia ya kupewa taarifa wakati wote kuhusu matukio muhimu mbalimbali kwa maisha na shughuli za wananchi na pia kuhusu masuala muhimu kwa jamii. Hivyo basi haki na uhuru wa kujieleza, kupokea na kutoa habari haina vipingamizi ambavyo serikali inadai kuwamo katika Sheria ya Magazeti ya Mwaka 1976.

Vilevile, kuwekwa kwa Vipengele vya Haki za Msingi na Wajibu wa Mwanadamu (Bill of Rights) katika Katiba ya nchi yetu kulibadilisha sheria zote ambazo zinakiuka haki za binadamu. Vifungu vyote tulivyovitaja hapo juu viliguswa moja kwa moja na Vipengele vya Haki za Msingi na Wajibu wa Mwanadamu. Ibara ya 14 ya Katiba inalinda haki ya kuishi na inaitaka jamii kutoa hifadhi ya maisha kwa kila mtu. Kana kwamba hiyo haitoshi, Ibara ya 26(1) na (2) zinataka kila mtu na serikali kutii Katiba ya nchi na vilevile kuchukua hatua za kuheshimiwa haki na sheria za nchi.

Waziri mkuu anayajua haya vizuri. Anafahamu kuwa sheria iliyotumiwa kufungia gazeti, ni sheria katili na imepitwa na wakati. Kuitumia sheria hii kunaendeleza dhana ya kuwa serikali hii inatumia udhaifu wa Katiba na baadhi ya sheria kukandamiza Haki za Binadamu na Uhuru wa Habari! Mambo haya hayakubaliki.

Kutokana na hali hiyo, sisi watetezi wa haki za binadamu na asasi nyingine za kiraia:
1. Tunarejea wito wetu wa kuitaka serikali kulifungulia mara moja na bila masharti, gazeti hili ambalo limekuwa kipenzi cha wananchi. Tunaitaka serikali ndani ya siku saba (7) kutekeleza hilo kwa kuangalia maslahi mapana ya jamii badala ya kuangalia maslahi ya baadhi ya viongozi wenye maslahi fulani katika kutimiza malengo yao binafsi.

Serikali itekeleze takwa hili haraka iwezekanavyo, na kwamba asasi za kijamii hazikubaliani na kauli ya Waziri Mkuu ya kutaka wahusika waende kwenye vyombo vya juu kwa sababu tatu zifuatazo:

Kwanza, sheria ya magazeti hairuhusu ukataji wa rufaa kwa waziri wa Habari ambaye ndiye aliyetuhumu na kuhukumu gazeti bila kutoa nafasi kwa wahusika kusikilizwa. Pili, Waziri Mkuu Pinda pamoja na sheria hiyo kutomtaja, hakueleza kuwa yuko tayari kupokea malalamiko ya MwanaHALISI. Hivyo kutoelekeza kwake tunakuchukulia kama njia ya kukwepa wajibu wake.

Tatu, hatukubaliani na kauli ya Waziri Mkuu na wengine wanaoitaka MwanaHALISI waende mahakamani kutafuta haki yao kwa kuwa serikali yenyewe haikutumia njia ya mahakama kufungia gazeti. Serikali inataka kuitumia mahakama ili kuchelewesha MwanaHALISI kupata haki yake. Nyote mnajua jinsi mahakama zetu zinavyokabiliwa na gonjwa kubwa la ucheleweshaji wa kesi.

2. Serikali, baadala ya kushughulika na watetezi wa haki na wanahabari wanaofichua uovu, ishughulike na wahalifu waliomteka, kumtesa na hatimaye kumtelekeza Dk. Ulimboka. Ushahidi uliobainishwa na gazeti hili haukuacha shaka yeyote juu ya waliohusika na sakata hili, na kama serikali au watendaji wake waliotajwa (na waliohusishwa) wana mashaka wangetumia ushahidi na taarifa zile kutafuta haki zao: kwanini wasiende mahakamani au wajitokeze na ushahidi wa kukanusha yaliyobainishwa?

3. Serikali iachane kabisa na ukandamizaji huu wa haki na uhuru wa habari. Matendo aliyofanyiwa Ulimboka, habari zilizobainishwa na MwanaHALISI juu ya sakata hili na kufungiwa kwa gazeti hili kunaonesha mtiririko wa matukio ya serikali kuminya uhuru na haki.

Ikumbukwe pia kuwa, Kesi Na. 34/2009 iliyofunguliwa tangu 2009 kupinga sheria ya magazeti ya mwaka 1976 iliyotumika kuwafungia MwanaHALISI haijasikilizwa mpaka sasa. Hii inaenda sambamba na serikali kufumbia macho mahitaji ya sheria ya uhuru wa habari na kudharau mapendekezo ya muswada wa habari tangu 2007 bila kupeleka Bungeni.

Kwa hoja hizo, sisi watetezi wa haki za binadamu, asasi za kijamii na wadau wakuu wa habari nchini, tunaendelea kusisitiza kuwa serikali itimize wajibu wake kwa kulifungulia mara moja gazeti hili na kufanyia kazi yaliyobainishwa. Kama ikishindwa kufanya hivyo, tutaitisha maandamano ya kupinga hatua ya serikali kufungia gazeti hili, kuminya uhuru wa habari, haki za binadamu na uteswaji wa wanaharakati na watetezi wa haki na kwamba tukifika hapo tunawaomba waandishi wa habari mtuunge mkono kwa yafuatayo.

i. Msichapishe habari yoyote inayomhusu Waziri wa Habari, Naibu Waziri, Katibu Mkuu wa wizara hiyo, na pia Mkurugenzi wa Maelezo. Tunawasihi wahariri wasiwatume waandishi katika Ukumbi wa Habari Maelezo kwa ajili ya kuchukua habari kama ilivyo kawaida na badala yake Watanzania wote wahakikishiwe kupata habari kwa njia nyingine mbadala.
ii. Tunawasihi wadau wote wanaoweza kutuunga mkono mara tutakapohitaji msaada wao ikiwa ni pamoja na kushiriki kwenye maandamano na kupata mawakili ambao watasaidia katika uendeshaji wa shauri letu mahakamani.
iii. Tunawasihi wanaharakati wote wasichoke wala wasirudi nyuma katika azma hii ya kutetea haki, uhuru na ulinzi kwa haki na watetezi wake.

Marcossy Albanie
Mwenyekiti wa Kamatifor
Asasi ambazo zimetoa tamko la kutaka serikali ifungulie MwanaHALISI ni MISA, Legal and Human Centre, Tanzania Human Rights Defenders Coalition, Human Rights National Association of Educators For World Peace and Citizen Rights Watch.
mwisho


Ndimara TegambwageInformation and Media ConsultantP.O. Box 71775, Dar es SalaamTel: 255 (0)713614872e-mail: ndimara@yahoo.comwww.ndimara.blogspot.com

Sunday, August 19, 2012

Sikukuu ya IDD EL FITR KITAIFA Songea 2012

Habari za Idd el Fitri katika Picha, Picha zote na Juma Nyumayo wa www.ruvumapress.blogspot.com













































Picha Na 4: Mgeni Rasmi wa Idd el fitr kitaifa Mkoani Ruvuma, Said Thabit Mwambungu (Katikati) ambaye ni Mkuu wa Mkoa huo akipokelewa na viongozi wa Msikiti Mkuu wa mkoa wa Ruvuma uliopo Manispaa ya songea

Picha Na3: Mufti wa Tanzania, Sheikh Issa Shaaban Simba akiingia ndani ya Msikiti wa Mkoa wa Ruvuma Manispaa ya Songea kuhudhuria ibada ya Idd el fitr kitaifa nyuma yake akifuatiwa na Mkuu wa mkoa wa Ruvuma Said Thabit Mwambungu

Picha Na 2: Immam wa Msikiti wa Mkoa wa Ruvuma Manispaa ya Songea, Shekh Shaaban Mbaya akitoa hotuba ya Idd el fitr kitaifa mkoani Ruvuma wakati waumin wakimsikiliza

Picha Na1: Baadhi ya waumin wanawake wakiwa wamesimama nje ya msikiti mara baada ya kumaliza swala ya Eid el Fitr kitaifa mkoani Ruvuma.

Sikukuu ya Eid El Fitr kitaifa Songea - Ruvuma

HALI YA HEWA imebadilika hapa Songea, ni manyunyu ya Mvua yanayoambatana na baridi, hali ya utulivu, waumini wa kiislamu na wakikristu wakipishana kwenye mitaaa kadhaa hapa mjini Songea wakielekea kwenye nyumba za Ibada katika siku hii ya leo ya kumaliza Mwezi mtukufu wa mfungo wa Ramadhani 2012.
Watoto wadogo wakiwa wameshikwa mikono na walezi wao bado pia tunakumbuka, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Jakaya Mrisho Kikwete kumshika mkono Rais wa Malawi Joyce Banda mwishoni mwa mfungo wa Mwezi huu wa Mfungo na kuwahakikishi wananchi wa nchi hizo mbili kuwa hapatakuwa na vita ya kugombea mipaka.
Hapa Songea umetolewa wito kwa waislamu wote nchini kuhakikisha kuwa wanauendeleza uadilifu na mafundisho ya dini hiyo ili kudumisha amani na usalama wa watanzania na majirani zao hpa duniani.

Maombi hayo yalikuwa ni sehemu ya Ibada ya swala ya Idd el fitr ilyofanyika katika Msikiti wa mkoa wa Ruvuma uliopo mjini Songea iliyohudhuriwa na maelfu ya waumini wa Dini hiyo wakiongozwa na mufti wa Tanzania Sheikh Issa Shaaban Simba na Mgeni Rasmi kitaifa Mkuu wa mkoa wa Ruvuma Said Thabit Mwambunga.

Immam wa Msikiti huo, Sheikh Shaaban Mbaya katika maombi maalum ya kuliombea taifa na viongozi wake wapate afya njema na uwezo wa kuwatumikia watanzania ili wawe na amani, alisema kuwa waumini wa kiislamu hawatakiwi hata kidogo kumbagua muislam au asiye kuwa muislam katika maisha yao ya kila siku.

Alisema, mafundisho ya dini hiyo yana sisitiza upendo na amani ili kuenzi uumbaji wa mwenyezi Mungu, ambaye ni mwingi wa rehema na kwamba viumbe vyote vya ardhi, majini na hewani ameviumba yeye mwenyewe bila ubaguzi kwa manufaa ya viumbe kwakuwa vinategemeana.

Alieleza zaidi kuwa waumini hao wafuate mafunzo toka kiongozi wao, Mtume Muhammad (SAW) ambaye aliweza kuwatunza mayatima na watu wasiokuwa na uwezo kiuchumi ambao wasiowaislamu na waislamu ili wapate furaha ya maisha yao ya kila siku licha ya shida na upweke waliokuwa nao.

"Ndugu waumin haina maana wakati huu wa sikukuuu mkajipamba kwa nguo safi na mkala vyakula vizuri wakati mioyo yenu na matendo yenu hayampendezi mwenyezi mungu," alisema Immam Sheikh Shaaban Mbaya na kusisitiza kuwa ni vyema wakaona umuhimu wa kuendeleza mafundisho waliyoyapata mwezi Mtukufu wa ramadhani kwa manufaa ya watu wote.

Aidha, Sheikh Mbaya alisema, Uchoyo na tamaa za mali, matendo mabaya na uroho wa madaraka na kudhalilisha wengine ndiyo chanzo cha kuvuruga amani iliyopo kuanzia ngazi ya familia, kijiji wilaya taifa na kimataifa.

Saturday, August 18, 2012

TANZIA

TANZIA - MWANDISHI MBOGORA AFARIKI DUNIA
Wakuu,
Habari za leo, habari za Jumamosi,
Tumepata taarifa kutoka Baraza la Habari Tanzania (MCT) kwamba mmoja wa maofisa wake na Mwanahabari na Mhariri wa siku nyingi, Alfred Mbogora amefariki Dunia leo saa 11.00 alfajiri katika hosipitali ya Taifa ya Muhimbili.
Katibu Mtendaji wa MCT, Kajumbi Mukajanga amesema kwamba Mbogora alilazwa Muhimbili tangu Jumanne baada ya kuwa ameanguka katika eneo la Tegeta, mara baada ya kupata chakula wakiwa njiani kwenda Bagamoyo kwa shughuli za kikazi.
Kabla ya kuanguka, Mbogora alikuwa akilalamika kwamba anasikia kuishiwa nguvu kwenye mguu na mkono na alipojaribu kusimama ili kutembea kutokana na hali aliyokuwa akiisikia mwilini alianguka.
Tangu wakati huo (baada ya kuanguka) alikata kauli na hakuwa kusema chochote hadi hapo alipokata roho leo alfajiri. Ni pigo kwa sekta ya habari nchini, kumpoteza mwanahabari mwenzetu ambaye ametoa mchango mkubwa katika sekta yetu ya habari.
Inasadikiwa kwamba msiba wa Mbogora uko nyumbani kwake Segerea, lakini taarifa zaidi tutazipata kadri tutakavyoendelea kuwasiliana na MCT pamoja na familia ya marehemu.
Tunachukua fursa hii kuwapa pole wafiwa wote, kwanza ni familia ya marehemu, MCT na wanahabari wote nchini. Bwana alitoa na Bwana ametwaa jina lake luhimidiwe, Amen.--
Neville C. Meena,
Secretary General,
Tanzania Editors Forum - TEF,
Dar es Salaam - Tanzania.
Cell: +255 - 787 - 675555
+255 - 753 - 555556

Thursday, August 16, 2012

Maandalizi ya Sensa, Cheki Bango

KILA  MMOJA  WETU ANAPASWA  KUSHIRIKI  SENSA AGOST 26Sensa kwa maendeleo, hivi sasa nchini Tanzania wimbo ni mmoja tu. Sensa kwa Maendeleo, Jiandae Kuhesabiwa.

Majimaji yajengewa uzio

Kaimu Muhifadhi Kiongozi wa Makumbusho ya Taifa ya Mashujaa wa Majimaji Songea, Balthazar Nyamusya (Kulia) akimkaribisha Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma, Said Thabit Mwambungu alipotembelea makumbusho hayo kwa maraq ya kwanza tangu ateuliwe kuwa mkuu wa Mkoa huo, nyuma ya Mwambungu ni Chief wa wangoni,  Emmanuel Xavery Zulu Gama.
Makumbusho haya sasa yanajengewa uzio, yanapendeza kwelikweli. Hongera Shirika la Makumbusho ya taifa kwa kazi nzuri inayosimamiwa na Bw. Balthazar Nyamusya hapa Songea.