Friday, June 11, 2010

Miss Ruvuma 2010 huyu hapa

Huyu ndo Miss Ruvuma 2010, Furaha david miaka 20, alipatikana pale viwanja vya Makumbusho ya Taifa ya Majimaji mjini Songea anasubiriwa kwa hamu kama kweli atashinda Miss Tanzania mwaka huu. Dkt. Mayunga wa Ores Tanzania amemuajiri mara moja kufanya kazi za kusaidia yatima na alijinyakulia kitita cha Shilingi laki nne. Hongera saaanaaa! (Picha Na Juma Nyumayo)

Sunday, June 6, 2010

Furaha David aukwaa Miss Ruvuma 2010

Juma Nyumayo, Makumbusho ya Taifa Majimaji Songea

Mlimbwende Furaha David (20) mwenye elimu ya Kidato cha nne ameibuka mshindi wa kwanza wa mashindano ya warembo ya Miss Ruvuma 2010.
Mlimbwende huyo licha ya kuvalishwa taji lake na aliyekuwa Miss Ruvuma mwaka jana, Glory Nicholous, alipewa zawadi ya kitita cha shilingi laki nne taslimu na ajira katika shirika la Ores- Tanzania linalohudumia watoto yatima na wanaoishi katika mazingira magumu.
Tukio hilo la kihistoria kwa warembo hao lilitokea usiku wa manane kuamkia Jumapili Juni 6, 2010 ambapo mgeni rasmi alikuwa Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma, Dkt Christine Ishengoma akiwakilishwa na Kaimu Katibu Tawala Mkoa wa Ruvuma Dkt. Anselm Tarimo.
Awali, Maelfu wa wakazi wa Manispaa ya Songea waliojitokeza kwenda kushuhudia mpambano huo katika viwanja vya wazi vya Makumbusho ya Taifa ya Majimaji eneo la Mahenge walipewa maelekezo na Mkurugenzi wa COTN Promotion & Entertainment, Miss Emmy Mssanja kuwa kulikuwa na washiriki 11 wenye vipaji na mategemeo tofauti ambao wataleta ushindani mkubwa ikilinganishwa na mwaka 2009.
Majaji watatu kutoka Dar es Salaam, wakiongozwa na Neema Kileo waliwasaidia watu kumpata mshindi huyo katika mpambano uliokuwa mgumu kutabiri kwani walimbwende hao waliokuwa na vipaji mbalimbali na urefu unaokimbiliana waliwaacha wakazi wa mjini hapa na vitongoji vyake kushindwa kumpata mshindi kabla ya saa 9.15 usiku.
Licha ya kupatikana kwa mlimbende huyo atakayepeperusha bendera ya ruvuma katika mashindano ya kanda na baadaye taifa, majaji hao waliridhika na Lilian Mbise (20) kuwa mshindi wa pili nakujinyakulia zawadi ya fedha taslimu shilingi laki tatu, na watatu aakawa mlimbwende Najat Makangila ambaye alijinyakulia donge la Shilingi laki mbili na ajira katika Shirika la COTN.
Mshindi wa nne na watano walipewa zawadi ya shilingi laki moja na nusu na wengine kifuta jasho cha shilingi laki moja kibindoni ikiwa ni zaidi ya ile ya mwaka jana ya shilingi elfu ishirini tu kwa kila mmoja.

Saturday, June 5, 2010

Utekelezaji Ilani Dkt. Nchimbi na Dkt. Kamala, meza moja Songea

Na Juma Nyumayo, Songea

ZIARA ya Waziri wa Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Dkt. Diodorus Kamala mkoani Ruvuma imemkutanisha meza moja na Mbunge wa Jimbo la Songea Mjini, Dkt. Emmanuel Nchimbi wakati wa kuelezea mafanikio ya Utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi wa CCM.
Baada ya maelezo Dkt. Kamala alitoa wito kwa WAKULIMA wa Mkoa wa Ruvuma kuleta ushindani katika kuzalisha mazao ya chakula na biashara katika kulikabili soko la jumuia ya Afrika Mashariki.
Waziri wa Ushirikiano wa Afrika Mashariki , Dkt Diodorus Kamala alitoa wito huo wakati akiongea na wadau wa maendeleo wa mkoa wa Ruvuma katika Ukumbi wa Songea Club Manispaa ya Songea katika siku yake ya kwanza ya kuelezea mafanikio ya utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya CCM 2005.
Alisema wakati tunaendelea na ushirikiano wa jumuia hiyo wakulima wa Ruvuma mwanayo nafasi kubwa katika kuzalisha na kuuza mazao yao.
“Urasimu uliokuwepo wa kuuza mazao nje sasa haupo tena, “ alisema Waziri na kufafanua kuwa kikwazo hicho kimependekezwa kuondolewa hivi karibuni katika kikao cha Baraza oa Mawaziri la Afrika Mashariki.
Alisema kuwa soko hilo litasaidia sana kuwapatia kipato wananchi wa mkoa wa ruvuma ambao ni wakulima wazuri wa nafaka na mazao ya biashara kwakuwa soko hilo ni kubwa.
Alizitaja jumuia za nchi za Afrika Mashiriki(EAC), COMESA, SADC zinatarajia kuweka saini mkataba wa soko la pamoja ambao utawawezesha wananchi wanaoishi katika nchi hizo kuopata huduma bora ambazo zitapatikana kutokana na kubadlishana bidhaa na kuweza kudhibiti mfumuko wa bei unaotokana na uzalishaji mdogo wa viwanda vya ndani.
Dk Kamala alisema wakulima wa Ruvuma ambao wameongezewa ruzuku ya pembejeo toka sh billion 3 hadi Sh Bilioni 10.6 katika kipindi miaka mitatu wanafursa kubwa ya kulitumia soko hilo endapo watazalisha kwa wingi na ubora unaohitajika.